VISA NA MIKASA: Binti wa Kinyalu akatimba ghetto na kudai hazioni siku zake

VISA NA MIKASA: Binti wa Kinyalu akatimba ghetto na kudai hazioni siku zake

Nakumbuka ilikuwa ni mwaka 1992 ndipo nilipopata huu mkasa wa kumtia binti wa shule mimba akiwa ndiyo kwanza ameingia kidato cha nne.

Nilikuwa nimekuja mjini Dar kwa kaka yangu aliyekuwa akiishi maeneo ya Victoria ili kujiunga na masomo ya ufundi katika chuo cha ufundi Chan’gombe. 

Sasa Baada ya kusoma kwa kipindi cha miaka miwili na baada ya kumaliza tulitakiwa kwenda kufanya field yaani masomo ya vitendo viwandani na mimi kwa bahati nzuri nikapangiwa kiwanda cha Bia (TBL) pale Ilala.

Pale kiwandani tulikuwa tunapewa posho kila mwezi, basi nikawa naulamba hasa nikijiona kama vile ni muajiriwa wakati nilikuwa niko kwenye mafunzo ya vitendo ambayo huwa tunafanya kwa miezi mitatu baada ya kumaliza chuo.  

Nilikuwa pia napenda kuvaa miwani ya kibishoo na kunifanya nionekane mtanashati hasa. Basi katika mbilinge zangu za ujana nikaanza mahusiano na huyu binti wa Kihehe ambaye ni mdogo wa mke wa jamaa mmoja aliyekuwa serikalini halafu anaishi geti kali na ni mboga saba. Huyu binti ambaye alikuwa anaitwa Paskalina aliletwa na shemeji yake kwa uhamisho ili asome huku Dar akitokea kijijini kwao mkoani Iringa. 

Pale kwao walikuwa na ng'ombe wa maziwa na walikuwa wanauza maziwa. Sasa mimi kwa zile kazi nilizokuwa nikifanya Kiwandani nilihitaji kunywa maziwa hivyo nikawa naenda kununua maziwa kila siku pale kwao kwa sababu walikuwa na Kioski cha kuuza maziwa ya moto na baridi.

Kutokana na swaga zangu Paskalina akawa amenizimikia balaa... yaani badala ya mimi kuhonga akawa yeye ndiye ananihonga tena pesa ndefu hata sijui alikuwa anamuibia dada yake pesa za maziwa Mhehe yule.

Alikuwa ni mrembo kwa sura na umbo, ingawa alikuwa ni mfupi lakini mwili wake ulikuwa umegawanyika vizuri juu akiwa ni mwembamba, halafu alikuwa na mahipsi yaliyotuna vizuri na makalio yaliyoendana na mwili wake. Alikuwa ni mweusi lakini Weusi wa chocolate na macho makubwa yaliyomfanya awe na mvuto wa pekee. Basi kutokana na mihemko yetu ya ujana ikawa kila akirudi shule namficha gheto kwa mshikaji wangu namla kisha namtoa usiku anarudi kwao.

Sasa mihemko yetu ikatufikisha pabaya akawa sasa baadhi siku haendi shule anajifanya anaenda shule lakini anakuja gheto namfungia kutwa humo ndani. Akitoka anapitia madaftari kwa shogake ili akakopi masomo akiwa kwao.

Hazikupita siku nyingi mchezo wetu huo ukaleta balaa kubwa likanifanya nikimbie mji na kwenda kujificha kijijini tena porini kwenye maboma ya ng'ombe ya baba yangu mkubwa aliyekuwa mfugaji kijiji kimoja kinaitwa Kirinjiko.  Naamini wanaosafiri kwenda Moshi au Arusha wanapajua...

Balaa lenyewe ni baada ya binti yule wa Kihehe kuja Gheto kunipa taarifa za kushtua moyo kwamba hazioni siku zake. Miye pamoja na urijali wangu nguvu ziliniishia. Nakumbuka siku ile wote tulijikuta tukilia kwa sababu yeye alijua lile jambo litaleta shida kubwa katika familia kwa sababu pia baba yake kule kijijini alikuwa ni mchungaji na kwa upande wangu niliona mlango wa jela ukiwa mbele yangu.

Baada ya kutafakari tukaamua aende hospitali akapime ili kuthibitisha. Alikwenda baada ya wiki kadhaa na akathibitisha kwamba ni kweli alikuwa na ujauzito wa mwezi mmoja. Zile habari zilikuwa ni kama msumari wa moto kwenye kidonda.

Nilimweleza Rafiki yangu ninayeishi naye kuhusu ule msala wa Mnyalukolo kuwa na mimba na yeye alishtuka sana. Baadaye tulikaa kikao ili kushauriana nini cha kufanya  tukiwa watatu Pamoja na binti mwenyewe na tukakubaliana mimba itolewe. 

Kwa bahati mshikaji wangu alikuwa na jamaa yake mmoja mtu wa Kijijini kwao huko Kyela Mbeya ambaye alikuwa ni Daktari katika hospitali moja maeneo ya Kinondoni Kwa Msisiri.

Tukakata shauri kwenda kumuona na baada ya mazungumzo na huyo Daktari tukakubaliana kiasi cha kulipa ambapo alitaka kiasi kidogo cha pesa kwa ajili tu ya dawa kwa sababu kazi yenyewe aliamua kutusaidia tu ili kumaliza kesi. Baada ya wiki moja tukapata kiasi hicho cha pesa na baada ya kumjulisha akatuahidi tuende siku ya ijumaa usiku.

Ni kweli tulienda na binti nikiwa na Rafiki yangu na baada ya muda wa saa nzima hivi zoezi likaisha tukaondoka kurudi nyumbani. Kwa kweli nilijiapiza kwa Miungu yangu yota kutotembea na yule binti tena na si yule binti pekee ni kwamba nilijiapiza kujiepusha na wanafunzi kwa ujumla maana niliona kabisa huu ukware wangu nitaishia jela.

Basi binti alirudi kwao lakini kwa taarifa nilizokuja kuzipata baadaye kumbe usiku alianza kuvuja damu kwa wingi na tumbo kumuuma ikabidi wamuamshe dada yake ambapo kutokana na hali yake kuwa mbaya wakamkimbiza hospitali. 

ITAENDELEA WIKI IJAYO…






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Mzee Mtambuzi

A freelance Journalist and also teaching self-empowerment, positive thinking as a means of creating the life you desire including spirituality. He is writing in Mwananchi Scoop every Wednesday Visa na Mikasa.


Latest Post

Latest Tags