Vijana wanavyoitazama sanaa kama sehemu ya kutokea

Vijana wanavyoitazama sanaa kama sehemu ya kutokea

Moja ya biashara ambayo imekuwa na mafanikio makubwa kama utaweka jitihada na nguvu katika kujifunza ni sanaa. Kutokana na hilo, sekta hii imekuwa ikikimbiliwa na vijana wengi hapa nchini kwa ajili ya kutengeneza kipato.

Moja ya sababu kubwa ambayo inaifanya fani hiyo kuwa na soko kubwa la vijana ni kutokana na maendeleo ya teknolojia ambayo mtu yeyote anaweza kuwa mtengeneza maudhui na kuamua kuyauza katika masoko ya mitandaoni.

Hii imesababisha kuwepo kwa wimbi la vijana wanaoshinda studio au location kwa matarajio kwamba ipo siku watakuwa kama wasanii wakubwa ambao wameshatoboa.

Kupitia hayo yote, Mwananchi imefanya mahojiano maalumu na Katibu Mkuu wa Wizara ya Sanaa, Utammaduni na Michezo, Gerson Msigwa ambapo ameeleza kuwa vijana wanaoingia katika sanaa kwa kigezo cha kutoka wanatakiwa watambue sio kila mtu anapaswa kuwa kwenye sanaa.

“Kwanza kijana anatakiwa kufahamu kwamba sio kila mtu anapaswa kuwa msanii, kupitia hilo ndio maana tunapata watu ambao hawazingatii maadili katika sanaa yetu,” amesema Msigwa.

Aidha Msigwa amewataka vijana wanaotamani au wanaoanza kujihusisha na masuala ya muziki kujifunza sanaa hiyo kwa kupata elimu.

“Kama mtu anataka kujihusisha na masuala ya sanaa kuna utaratibu, ni vizuri asiingie kiholela, ahakikishe anapata elimu ambayo inatolewa na Chuo cha Sanaa na Utamaduni (TASUBA), lazima ahakikishe amesaini katika Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) pia kuna makongamano ya sanaa na utamaduni ambayo yatatoa elimu zidi kuhusu sanaa,” amesema.

Kwa upande wa Muongozaji Filamu na Mwanafunzi wa TASUBA, John Music amewataka vijana waangalie vipaji vyao kabla ya kuikimbilia fursa.

“Vijana wanatakiwa waangalie vipaji vyao kwanza kabla ya kukimbilia fursa mbalimbali hasa katika upande wa sanaa ikiwemo vipaji na taaluma, lakini kwa upande mwingine  wasanii wengi hawana elimu bali wana vipaji tu na hata wale waliopata elimu hatuwaoni kwenye ‘mainstream’ wakifuata yale waliyofundishwa,” amesema John Music na kuongeza.

“Siku hizi kumekuwa na kundi la wanaojiita wasanii chipukizi wamekuwa wakishinda studio na kupoteza muda wa kufanya vitu vingine ambavyo vingewapatia mafanikio zaidi na kuokoa muda.”

Pia amewataka vijana kutumia njia mbalimbali wanapotafuta fursa ya kutoka kimaisha ili kufikia malengo.

“ukiwa na malengo na ukaweka 'option' ni vizuri yaani akili yako isilale sana katika sanaa ukidhani ndio kuna njia pekee ya kutoka, ukiwa na machaguo mengi itasaidia sana kwa sababu mpaka leo kuna watu wameganda kwenye sanaa na hawajapata nafasi hata ya kuonekana,” amesema.

Kwa upande wa mwigizaji Sidi ambaye yupo katika Tamthilia ya Jua Kali, amesema vijana wanakimbilia katika sanaa kwa sababu ya tamaa au kuona mafanikio ya staa fulani.

“Vijana wengi wamekuwa wakikimbilia sanaa kwa sababu ya tamaa au kumuona msanii fulani amefika levo ya juu ambayo na yeye anatamani afike kwa muda huo, ndio maana wakishaingia huku ni wepesi kushawishika kwa mambo mengine na kusahau walichokifuata,” amesema.

 Naye mchekeshaji wa Cheka Tu, Masatu Ndaro maarufu Mjeshi Kikofia, ameeleza kuwa kila mtu sasa hivi anatamani kuonesha kile ambacho anacho.

“Sio mbaya kijana kujitafuta katika upande wa sanaa na mimi nina imani kila mtu anacho cha kukionesha katika sanaa kwa sababu sanaa imegawanyika, kama mtu ana kipaji na anaona fursa ipo upande huo hakuna shida, mfano mimi nilikuwa mwalimu lakini niliona huku ndiyo kunanifaa ndio maana nipo mpaka leo,” amesema.

Wadau mbalimbali wamekuwa na maoni tofauti kuhusiana na hili pindi walipozungumza na Mwananchi.

Mwanamuziki Devid Nacho ambaye kwa sasa ameanza kujitafuta huku jina lake la kisanii ni Nachokid, amebainisha kuwa yeye anaamini kupitia kipaji chake atafika mbali na ndio fursa ya yeye kutoka.

“Mimi naamini kupitia muziki nitafanya mambo makubwa na ndiyo itakuwa fursa ya mimi kutoka japo baadhi ya wasanii wakubwa wanashindwa kuamini vipaji vyetu sisi wachanga, kuna muda hadi wanachukua mashairi yetu wanayatumia halafu wanakaa kimya,” amesema na kuongeza.

“Kila mtu anayeingia kwenye sanaa ana uwezo na kipaji ambacho kimemsukuma kufanya hivyo, kwenye sanaa kuna mambo mengi."

Kwa upande wa Tausi Deogratius mkazi wa Temeke, Dar es salaam, amedai kuwa vijana wanajikita katika sanaa kwa sababu ya kuiga, kufuata mkumbo na vishawishi.

“Leo hii unakuta mtu anatamani kuwa kama Zuchu au Alikiba kwa sababu aliwaona wanavaa vizuri au wanasafiri kwenda nje basi na yeye anaamini akifanya hivyo atakuwa kama hao, mimi naita kijidhalilisha tu,” amesema Tausi.
.
.
.
#MwananchiScoop
#BurudikaNasi






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Asha Charles


Latest Post

Latest Tags