Video za Bongo Fleva zenye stori kali

Video za Bongo Fleva zenye stori kali


Peter Akaro

Ukweli ni kwamba video nyingi za muziki wa Bongo Fleva kwa sasa hazina stori yoyote ndani tofauti na hapo awali, waandaji (music directors) na wasanii wenyewe wamejikita zaidi kwenye ubora wa picha na rangi za kupendezesha.

Hapo awali, Director kutoka Visual Lab, Adam Juma aliwahi kueleza hilo limekuwa tatizo ambalo linazidi kukua kwa kasi ingawa bado halijaoneka kama tatizo.

Kwa kuzingatia hilo, makala haya yanaenda kuzitambua baadhi ya video za Bongo Fleva ambazo zina stori kali ndani yake na ujumbe wake wa picha unasimulizi nzuri.

1. Dangerous - Joh Makini

Rapa huyo kutoka kundi la Weusi aliamua kuweka visa viwili vya kibabe katika chupa hili, ni kitu kilichosadifu jina la wimbo wenyewe, Dangerous (hatari). Anaelezea kuwa na mwanamke ambaye anampenda kweli ila matukio yake ndio hatari ila hajali hilo ingawa mwishoni anamchezea mchezo hatari.

Mrembo huyo wa Joh Makini anaonekana akiwa katika duka la Sonara, anatumia ujanja na kuamua kuiba mkufu wa dhahabu, mlinzi wa mlango anamuona na kuamua kumngojea atoke ili kumkamata. Ila unajua nini, wakati anatoka anapishana na Joh akiingia ambaye anapitisha mkono mfukoni na kumuibia ule mkufu, sasa Mrembo alipotoka nje na kupekuliwa hana kitu!.

Baadaye Joh anaenda kumzawadi mkufu huo wakiwa wote kwenye Mgahawa, ilikuwa kama 'suprize' kwa Mrembo huyo kwani ni kitu alichopigania ila akakikosa pasipo kuelewa licha kuchanga karata zake vizuri. Na hapo ndio unakuwa mwanzo wa penzi lao kwani wamekutana wote ni watu mishe za kibabe tu, kwa lugha rahisi Joh alitumia ule mkufu kumpata huyu Mrembo.

Haikuishia hapo, Mrembo anacheza tukio lingine hatari pale anapomuibia Mzee mmoja, vijana wa mjini wanamuita 'Sponsa' kadi ya Benki (ATM Card), huku Joh Makini akiwa pembeni akiusoma mchezo. Wanaondoka wote, kisha Joh anavaa kininja (kuziba sura) na kwenda kutoa fedha za kutosha, na baadaye Mrembo anarudisha kadi ya watu na kumuaga yule Mzee.

Sasa hatari yenyewe ni pale Joh Makini anapoenda kulala na huyo Mrembo, huwezi amini Mwamba wa Kaskazini anashtuka asubuhi kapigwa pingu kwenye kitanda na Mrembo kasepa na fedha zote, huku nje magari ya Polisi yanapiga ving'ora. Video imetoka Julai 16, 2021 na imeongozwa na Director Ivan.

2. Gwaji - Mwana FA

Video hii inakuhitaji kuitazama kwa makini sana ili kuweza kuielewa kwa maana stori yake imeandikwa kikubwa zaidi, ni utapeli wa kutumia akili kubwa, ukizubaa umeachwa feri.

Mwanzoni Gwiji mwenyewe (Mwana FA) anakutana na Nyoshi El Saadat aliyeshirikishwa katika wimbo na kumkabidhi mkoba (Briefcase) uliyojaa fedha, ni kama alienda katika kiwanda kununua kitu. Baada ya hapo FA anaenda kukutana na Bosi wa Nyoshi ambaye amezungukwa na Walinzi kibao.

Wakati majadiliano yakiendelea, FA tayari kashatuma watu wake kwenda kuiba zile fedha alizomkabidhi Nyoshi na wanafanikiwa licha ya mule ndani kuwa na walinzi wengi na Bondia mwenye mkanda wa WBF Intercontinental Super Welterweight, Hassan Mwakinyo akijifua vilivyo.

Sasa katika kikao cha pili cha kibiashara ili kukabidhiana mali, Nyoshi anaulizwa na Mabosi wake ziko wapi fedha alizokabidhiwa na Mwana FA, anajibu zimeibiwa. Nyoshi hana jinsi zaidi ya kumfuta FA na kumuuliza kuhusu hilo, kwani alipatiwa jibu sasa!, tayari kashaachwa feri na Gwiji.

FA anawaeleza hilo halimuhusu kashapewa chake na kuamua kuondoka zake, mwishoni wale aliowatuma wanamrudishia fedha zake zote zikiwa hazijapungua hata senti mia, hivyo anakuwa ameua ndege wawili kwa jiwe moja. Video imetoka Juni 17, 2021 na imeongozwa na Director Hanscana.

3. Aya - Marioo

Hii ni video ambayo ukitoa sauti na kuitazama pekee utaelewa kila kitu kilichopo ndani yake, ni muziki uliokutana na filamu fulani fupi na kali kimtindo. Marioo mapenzi yanamtesa sana hadi anafikia hatua ya kutaka kumeza vidonge ili kujiondoa uhai kutokana na yale aliyoshuhudia kwa mpenzi wake.

Akiwa chumbani kwake na vidonge juu ya meza, huku mpenzi wake kalala, anakumbukia yale aliyoyana, nayo ni mpenzi wake kuingia katika chumba fulani akiwa na mtu mwingine na kumsaliti. Aisee! inachoma, anageuza shingo upande wa pili na kumtazama Bibie haamini kama ndio kafanya hivyo, anaishia kusema, Ahaaaaya! .

Mpenzi wake anarudia nyumbani na kujitazama kwenye kioo na kuamua kutoka nje tena na kumuacha Marioo kalala, kumbe naye kalala kimtigo. Marioo anamfuta nyuma kwa kunyatia, anashuhudia tena Bibie akikutana na yule jamaa kisha wanaongozana hadi bwawani.

Huko bwawani mambo sio poa kabisa, kumbe Bibie ana mpenzi mwengine, ugomvi ni mkubwa hadi watu anatoleana mapanga, hapo Marioo anagundua mpenzi wake amekuwa akimsaliti kwa wanaume wengi. Akiwa pale kitandani naye mkononi ana kisu ila hana cha kufanya, basi Marioo anaona isiwe tabu, anabeba begi lake na kupanda gari na kuondoka zake. Video imetoka Februari 4, 2020 na kuongozwa na Adam Juma.

4. Mpaka Kesho - Harmonize

Hii ni video ambayo Harmonize kamshirikisha Mimi Mars kama 'Video Queen' na imefanyika katika Hifadhi ya Taifa ya Manyara, kutokana na ujumbe aliotaka kuutoa hakuwa hana budi kufanya hivyo.

Harmonize akiwa anafanya shughuli zake za kupasua kuni huko hifadhini analetewa barua na mtoto mdogo, anaisoma barua hiyo, inamtaarifu kuwa mpenzi wake (Mimi Mars) anaolewa na raia mmoja wa kigeni mwenye fedha nyingi.

Lakini mpenzi wake hakuwa tayari kwa hilo ila familia hasa mama yake mzazi ilishinikiza kutokana walipatiwa kiasi kikubwa cha fedha kama mahari. Hata hivyo wakati mipango hiyo ikifanyika, walikuwa wanajua fika binti yao yupo katika mahusiano na Harmonize sema ndio hivyo fedha ina utamu wake.

Basi siku ya harusi, Bibie anamuona Harmonize na kumkumbuka aliwahi kumpa kidani, anashika kifuani kwake na kukikuta kumbe alikivaa siku hiyo muhimu. Basi usiku wake Harmonize kampigia simu Bibie, mume wake alipoona akawaka vilivyo, naye akapiga simu ukweni kwamba mtoto wao kaanza visa.

Haikuchukua muda mashemeji na Baba Mkwe wakaanza kumsaka Harmonize kila kona, mwishowe wakaenda kumkuta akiota moto pekee yake, wakamkamata na kufunga mikono nyuma na kumwagia maji ya baridi na kipigo kikali. Video hii imetoka Julai 20, 2021 na imeongozwa na Director Hanscana.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags