Uvaaji vipini na hereni kwa wanaume ni fasheni

Uvaaji vipini na hereni kwa wanaume ni fasheni

Na Pelagia Daniel

Inaweza kuwa ni ajabu kwa jamii zetu za Kitanzania kutokana na tamaduni wanaume kuvaa vipini puani na hereni lakini katika ulimwengu wa mitindo na utandawazi imekuwa jambo la kawaida.

Zamani kuna baadhi ya jamii zilikuwa zinapinga urembo uliozoeleka kwa wanawake kufanywa na wanaume. Hapo awali ilizoeleka wanawake pekee ndiyo waliokuwa wakivaa hereni na vipini puani.

Baadhi ya jamii katika nchi za Ulaya na Asia urembo wa kuvaa hereni na vipini huchukuliwa jambo la kawaida. Lakini kwa upande wa Tanzania wanaume wameanza kutumia urembo huu wa hereni na vipini puani na imeonekana kuwapendeza vile vile.

Urembo wa vipini umeanza muda kidogo na ulivaliwa sana na wanawake wa pwani na mara nyingi tulizoea kuwaona wanawake wa dini ya Kislaam, siku hizi imekua tofauti haswa miaka ya hivi karibuni staili hii imerudi kwa kasi zaidi na ubora wa hali ya juu.

Siyo watu wa pwani tu wanaotumia urembo huu hata wengine vile vile siyo lazima kutoboa pua. Mtindo umekuja kivingine kwa sasa waweza vaa katikati ya pua ambapo huitwa ‘kisharufu’ au kutoboa kabisa pua na kuweka kipini sehemu zote mbili za pua.

Lakini wengi hupendelea moja na kwa upande wa wanaume ni muhimu kutoboa kabisa ili kuweka muonekano mzuri na wa kuvutia waweza fanya hivyo kwa pande zote mbili za pua au upande mmoja tu na kufanya muonekano wa tofauti zaidi.

Tukumbuke ni asilimia ndogo sana ya watu wanaokubaliana na muonekano huu Afrika haswa hapa nchini kwetu Tanzania pia inaleta ugumu zaidi kwa upande wa jinsia ya kiume, tuwe makini katika hili japo urembo huu ni kama urembo mwingine na umeanza tangu enzi za mababu zetu.
Akizungumza na Mwananchi Scoop Sharifu Hamadi mfanyabiashara wa vipini vya pua na hereni Kariakoo anaeleza kuwa siku hizi soko la bidhaa hizo limebadilika kutokana na wateja kuwa wakiume ingawa na wanawake wananunua.

“Mambo siku hizi yamebadilika wanaume wengi wamekuwa wakipenda urembo kama wanawake tena husani urembo wa vipini vya puani, mara ya kwanza aliwahi kuja mteja wa kiume kuulizia hereni na vipini mimi nilijua huo urembo ni kwa ajili ya mwanamke kumbe ulikuwa wa kwake, baada ya kumuona akivaa mbele yangu.



“Basi kutoka hapo sikushangaa tena nikajua ni mambo ya fasheni na utandawazi tunaoiga kutoka kwa wasanii wakubwa na watu maarufu duniani wanaoenda na wakati na dunia inavyotaka,” amesema Sharifu.

Hata hivyo Sharifu hakuacha kuzungumzia upande wa tamaduni za Kitanzania kuhusu urembo huo
“Unajua kwa maadili ya kwetu kumekuwa na ukakasi kuhusu wanaume kuingilia urembo wa wanawake lakini sisi watu wa fasheni tunaona kawaida pia ni mitindo ambayo imezalishwa hivi karibuni kwa ajili ya kutafuta muonekano” amesema Sharifu.

Hata hivyo kwa upande wake Mwanamvita maarufu kama Mama Abuu mkazi wa Dar es salaam, ametoa maoni yake anavyowachukulia wanaume wanaovaa vipini na hereni kwa kueleza kuwa fasheni hiyo haifai kwa mwanaume.

“ Utandawazi umekuwa ukiwapeleka vijana kwenye dunia nyingine kabisa hasa katika masuala ya fasheni kumekuwa kuna mambo ya tofauti kila siku sasa mwanaume unavaaje kipini cha pua au hereni haifai kabisa.

“Zamani wazee wetu walikuwa wakiwakataza watoto ama vijana kuvaa urembo wa vipini puani na kutoboa pua au masikio tofauti na sasa mambo yamekuwa tofauti” amesema Mwanamvita.

Pia amegusia vijana kuiga urembo wa namna hiyo kwa wasanii na watu maarufu
“Vijana siku hizi wamekuwa wakiiga fasheni kutoka kwa wasanii au watu maarufu kitu ambacho hawafikirii kama kitakuwa na madhara au faida ilimradi waende na fasheni”.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post