Utafiti: Ulaji parachchi hupunguza hatari ya kupata mshtuko wa moyo

Utafiti: Ulaji parachchi hupunguza hatari ya kupata mshtuko wa moyo

Parachichi ni aina ya kipekee ya tunda. Matunda mengi kwa asili ni wanga lakini parachichi limejaa mafuta yenye manufaa makubwa kiafya.

Tafiti mbalimbali zilizofanyika zimebaini kuwa tunda la parachichi limesheheni manufaa makubwa katika afya ya mwanadamu.

Utafiti mpya uliyofanywa nchini Marekani umeonesha kuwa kula tunda la parachichi kunapunguza hatari ya mtu kupata mshtuko wa moyo.

Matokeo ya utafiti huo yametangazwa wakati ambao ugonjwa wa moyo na mishipa ndio unaoongoza kwa kuua watu duniani kwa kusababisha vifo Milioni 18 kila mwaka kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).

Akitoa matokeo ya utafiti huo, Mwenyekiti wa Baraza la Jumuiya ya Moyo ya Marekani, Cheryl Anderson alisema utafiti huo mpya unaeleza kuwa kula parachichi angalau mara mbili kwa wiki kumeonekana kupunguza hatari ya kupata mshtuko wa moyo kwa asilimia 21.

“Utafiti huu ni ushahidi kwamba parachichi zina manufaa ya kiafya,” alisema Anderson

Naye Mtaalamu wa Lishe Manispaa ya Temeke, Dk Charles Malale anasema ikiwa mtu anapenda kuwa na afya bora kwa kula tunda la parachichi, basi karibu atapata faida nyingi.

 Anasema parachichi ni tunda la pekee ambalo limebeba virutubisho mbalimbali ambavyo ni muhimu kwa ajili ya miili ya mwanadamu.

“Pamoja na parachichi kuwa na virutubisho vingine mbalimbali, bado parachichi lina virutubisho muhimu tunavyovihitaji kutoka kwenye mimea. Virutubisho hivyo ni Carotenoids ambayo inapatikana kutoka kwenye parachichi ina manufaa makubwa kwa ajili ya miili yetu katika kulinda macho dhidi ya matatizo mbalimbali yakiwemo yale yatokanayo na umri,” anasema

Anasema parachichi husaidia kupunguza uzito, Swala la kupunguza uzito linaathiriwa sana na mfumo mzima wa lishe. Hivyo kula vyakula ambavyo vinawezesha mchakato wa metaboli kwenda vyema kutakuwezesha kupunguza uzito kwa muda mfupi.

Ameeleza parachichi ni tunda zuri ambalo huwezesha mchakato wa metaboli kwenda vizuri mwilini.

Parachichi lina Fatty Acid

Anasema Fatty Acid ni asidi itokanayo na mafuta ya parachichi ambayo ni muhimu sana kwa ajili ya shughuli mbalimbali katika miili ya mwanadamu.

“Fatty Acid inahitajika katika uzalishaji wa homoni, ukuaji wa seli pamoja na ufyonzwaji wa virutubisho,” amefafanua.

Dk. Malale anasema parachichi ni tunda ambalo kiwango chake cha sukari hakina athari kwenye mwili. Hivyo utumiaji wa tunda hilo utakuwezesha kuweka kiwango cha sukari mwilini kuwa katika hali nzuri ya wastani.

Pia anasema madini ya potasiamu yanayopatikana kwenye tunda la parachichi kwa zaidi ya asilimia 14 ni muhimu sana katika utendaji kazi wa misuli ya moyo.

“Lakini pia asidi ya Oleic inayopatikana kwenye parachichi, imebainishwa na wataalamu kuwa husaidia kwa kiasi kikubwa kuzuia uvimbe mwilini,” anasema.

Huboresha mmeng’enyo wa chakula

Anasema vyakula vyenye nyuzinyuzi ni muhimu sana kwa ajili ya kuufanya mmeng’enyo wa chakula uende vizuri.

“Parachichi ni tunda lenye nyuzinyuzi kwa karibu asilimia 13 ambazo ni sawa na kiwango cha asilimia 54 unachotakiwa kula. Je bado huoni umuhimu wa tunda hili? Anza kula ili uboreshe mmeng’enyo wako wa chakula sasa,” anasema

Ameeleza kuwa ni muhimu kwa wajawazito kwani kuwepo kwa kiasi kikubwa cha folate, potasiamu, Vitamini C na B6 ambazo ni muhimu kwa ajili ya afya na ukuaji wa mtoto; kunalifanya tunda la parachichi kuwa na umuhimu mkubwa kwa wajawazito.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post

Latest Tags