Upendo Mwakyusa ni muhitimu katika chuo kikuu cha Dodoma UDOM akiwa amepata shahada ya science ya mazingira kutoka katika kitivo cha science ya dunia na uhandisi.
Licha ya kupata shahada hiyo Upendo anajihusisha na harakati za utunzaji mazingira hususani kuyalinda kupitia taasisi ya call for environment concervation akiwa mwanzilishi na mkurugenzi.
Akizungumza na mwandishi wa makala haya Upendo anasema anajihusisha na kazi ya uandishi akiwa anaandika makala mbalimbali katika magazeti.
Hata hivyo anasema tayari amezindua jarida lake linatambulikwa kwa jina la A call for environment conservation.
Aidha akielezea wazo lake la kuwa muandishi jinsi lilivyokuja binti huyo ameeleza kwamba baada ya kusoma vitabu mbalimbali ndipo alipogindua kuwa anapenda kazi hiyo.
“kiukweli baada ya kufanya observation zangu ndipo nilipogundua kwamba mimi napenda kuandika na ndiyo kitu ambacho ninauwezo wa kufanya vizuri kama ambavyo mtu mwingine angeimba au kucheza” anasema na kuongeza
“Kile kipaji ulichonacho ni vyema ukakitumia kufikisha ujumbe katika jamii ili kuleta mabadiliko kwenye jamii hususani katika sekta ya masuala ya mazingira”anasema.
Aidha akijibu swali la mwandishi baada ya kuulizwa kuwa anawezaje kumaintain mambo yote hayo kwa wakati mmoja majibu yake yalikuwa hivi.
Upendo aliliambia jarida la Mwananchi scoop kuwa kila kitu kinawezekana kulingana na wewe mwenyewe pale ambapo utakapojitathmini na kujua nini unachotaka na unataka kufika wapi.
“Mimi ninaweza kuhandle mambo yote pasi na shida yoyote nina andika ninafanya activities za kwenye organization pamoja na kazi nyingine pia kikubwa ni kuweka utaratibu katika kila jambo unalolifanya”anasema.
Sambamba na hayo akizungumzia changamoto anazokutana nazo kwenye kazi zake alisema kuwa jamii bado haina mitazamo chanya kwa vijana ambao wanachipukia katika kufanya shughuli za kimaendeleo.
“Watu wengi wamezoea kuona watu maarufu au watu wakubwa wakifanya vitu vikubwa kwenye jamii yaani zile sura ambazo zinafahamika hivyo zile sura ambazo ni ngeni au sio maarufu watu hua wanamashaka hawaamini kama unaweza kufanya jambo bado watu wanamitazamo ambayo sio chanya”anasema
Hata hivyo alieleza namna anavyokabiliana na changamoto hiyo na kusema kuwa mara nyingi anajitahidi kuwaelimisha watu na kuendelea kufanya vitu vizuri na vikubwa ili jamii iweze kuamini kwamba hakuna jambo linaloshindikana.
“Njia pekee ninayoitumia ni kuhakiksha kwamba naendelea kutumia ubunifu mkubwa juhudi, maarifa na kusali sana ili kusudi hiyo changamoto itumike kama daraja la mafanikio kwangu na wanaonitazama.”anasema
Unawashauri nini vijana ambao wanachipukia kwenye tasnia ya uandishi?
“Kikubwa nawashauri waendelee kujifunza kwani hakuna kitu kizuri kama kujifunza kupitia watu ambao wanafanya vizuri kupitia sekta ya uandishi”anasema na kuongeza
“Pia nawashauri wawe wabunifu kuja na vitu ambavyo vitakonga mioyo ya watu ili waweze kuvutika kusoma na kufanyia kazi yale ambayo tunayaandika”anasema.
Sambamba na hayo ameeleze malengo yake ya hapo baadaye ikiwemo ni kuhakikisha anatoa makala nyingi , majarida pamoja na vitabu mbalimbali ambavyo vitahusu masuala ya mazingira.
Aidha anasema kuwa kwa asilimia kubwa vitabu na majarida yanayohusu mazingira ni machache sana kwani watu hawajazoea kukutana na vitu kama hivyo .
“Wengi wamezoea kukutana na hadithi za kusisimua, stories maisha ya kila siku, makala pamoja na maandiko yanayomuhusu mtoto wa kike yote haya ni mazuri lakini jamii inapaswa kutambua kwamba pasipo mazingira hakuna kitu kitakachoweza kufanyika katika namna iliyobora” anasema na kuongeza
“Kupitia kazi hii ya uandishi lengo langu kubwa ni kuhakikisha jamii inaelimika na inafahamu umuhimu wa kutunza mazingira na kukabiliana na mabadiliko mbalimbali ya tabia ya nchi”anasema.
Upendo Mwakyusa ni binti aliyezaliwa jijini Mbeya na kufanikiwa kuanza elimu yake ya msingi katika shule ya Mkapa English medium na baadaye kujiunga na elimu ya sekondari katika shule ya Iyanga iliyopo Mbeya, na kufanikiwa kuingia kidato cha sita shule ya wasichana Ngaza iliyopo Mwanza na hatiamye amemaliza elimu yake ya Chuo kikuu mwaka 2020.
Bila shaka kupitia makala haya kijana umepata mengi yatakayokufaa kwenye safari yako ya mafanikio kikubwa uthubutu, kujiamini na kupambania kila unachokifanya hakika utafanikiwa.
Leave a Reply