Umuhimu wa kuitunza mikono na miguu yako

Umuhimu Wa Kuitunza Mikono Na Miguu Yako

Habari msomaji ni siku nyingine tunakutana tena kupitia mwananchiscoop ambapo ninaamini kuwa u mzima wa afya na unaendelea na majukumu yako ya kila siku ya kulijenga taifa.

Leo hii tutaelezana na  kujuzana mambo mbalimbali kuhusiana na masuala mitindo, urembo na mavazi ambayo najua uwenda unayajua ila mimi nakujua tu zaidi.

Msomaji leo katika safu hii tutaangalia umuhimu wa mtu kuitunza mikono na miguu yako.

Muda mwingi hasa wanawake tumekuwa tunatumia kuhakikisha nywele zetu zipo katika hali nzuri na kichwa kwa ujumla lakini tumesahau kuangalia mikono na miguu ambayo ndio mara nyingi huwa ‘bize’ na kazi kwa muda mrefu.

Sio lazima uende saluni ili kuhakikisha mikono na miguu  yako iko safi na yakupendeza unaweza ukafanya mwenyewe tu nyumbani. Tuangalie jinsi ya kufanya kwa njia rahisi na nyepesi

Ngozi ya viganja vya mikono na miguu ni laini na inaweza kudhurika upesi hasa kama unafanya kazi za kutumia nguvu. Ni vuzuri kuhakikisha unaitunza vizuri ili isipoteze uzuri wake wa asili.

Katika kuitunza mikono na miguu yako ni lazima  uwe na tabia ya kuifanyia usafi maalumu angalau mara moja kwa wiki.

Vitu muhimu ambavyo unapaswa kuwa navyo wakati wa kusafisha mikono na miguu yako ni losheni ya mikono na kucha, taulo ndogo, brash ya mikono, kikata Kucha, tupa ya kucha (nail file), maji ya uvugu vugu na sabuni ya maji ikiwezekana medicated.

Osha mikono na miguu yako vizuri kisha kata kucha kwa urefu unaoona unakufaa na kuzisugua na tupa, baada ya hapo weka maji ya uvugu vugu kwenye beseni dogo na weka matone kadhaa ya sabuni ya  maji kisha loweka mikono au miguu kwa muda wa dakika tano.

Baada ya hapo kama unaosha mikono au miguu isugue taratibu hasa sehemu za kiunganishi cha kucha na kidole maana huwa laini sana. Ukimaliza suuza vizuri na maji ya uvuguvugu, kausha na taulo safi na upake losheni ya mikono au miguu.

Hakikisha unaitunza miguu na mikono yako ili nayo iweze kukutumikia kwa muda wote wa maisha yako haijalishi kama unaitumia kulima, kusuka watu, kuandika au hata kufundishia.

Kama unatumia mkaa hakikisha unanawa na kusugua mikono vizuri mara tu baada ya kumaliza kuutumia. Kwa ushauri tu unaweza kutembea na losheni yako ili kila unaponawa mikono basi uwe unapaka ili kuhakikisha mikono yako haiwi mikavu.

Kama una mtoto mchanga ni vizuri kucha zikawa fupi kabisa kwaajili ya afya na usalama wa mtoto.

Umuhimu wa kutunza mikono na miguu ni mkubwa sana kwani ikiwa misafi mara zote utaonekana nadhifu na wakuvutia machoni pa jamii.

Msichana mrembo au mwanaume mtanashati awezi kuacha vidole vya miguu na mikono yake vinakuwa vichafu hata mara moja muda wote atahakikisha vinakuwa safi.

Ukiwa msafi mara zote unajiamini kukutana na mtu yoyote yule muda na wakati wowote.


Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Janeth Jovin

A writer, reporter, presenter and news anchor for Mwananchi Scoop. Her writings are based on business, money management on Tuesday and health on Thursday on Mwananchi Scoop. Her famous segments on Mwananchi Scoop include KARIA and FASHION.


Latest Post