Uhusiano ulioko kati ya  kazi na wito

Uhusiano ulioko kati ya kazi na wito

Ohooo!!! Niaje mtu wangu kama kawa kama dawa leo ikiwa ni jumatatu tulivu kabisa baada ya shamrashamra za sikuu ya Christmas hatimaye imepita salama bwana na kama umepitia wakati mgumu Mungu akawe faraja kwako.

Kama ilivyoada leo hua tunakomaa na zile makala za kazi, ujuzi na maarifa bhana katika kuhakikisha unapata mwangaza wa maisha na kufahamu wapi kwakuanzia.

Leo nimekuandalia makala inayozungumzia uhusiano ulioko kati ya kazi na wito karibu kufuatilia makala haya.

Haijalishi uko wapi, unaishi wapi,wewe ni nani, na unafanya nini. Ukweli utabakia kuwa; kila mmoja wetu ana masaa ishirini na nne (24) kwa siku. Na kiasi fulani cha muda huo tumekuwa tukikitumia kwenye mapumziko pamoja na kujishughulisha na mambo kadha wa kadha.

Tumekuwa tukitumia muda wetu katika kufanya mambo kadha wa kadha ambayo kwa namna moja ama nyingine yanakuwa na lengo la kutupatia kipato,kujifurahisha,kujiburudisha,na hata kujisikia wenye kusudi maalumu maishani n.k.

Moja kati  ya maswali ambayo mwanadamu amekuwa akijiuliza mara kwa mara, na ambalo linatawala fikra za wengi,ni lile swali la kutaka kufahamu dhumuni la maisha yake hapa duniani.

Tumekuwa tukijiuliza; Mimi ni nani? kwanini nipo hapa duniani?. Na katika kutafakari huko kuhusiana na dhumuni letu katika maisha, ndipo wengi wetu huwa tunafikiria kuhusiana na kazi au wito wetu.

 Kuna tofauti na uhusiano mkubwa kati ya kazi na wito.

Kazi.

Neno “kazi” linawakilisha aina ya huduma unayoitoa kwa mabadilishano. Kwa kufanya kazi unakuwa unatoa muda wako, juhudi, ujuzi, umakini, maarifa, na ufahamu wako kwa ajiri ya kujipatia kipato.

 Na kitendo hiki ndicho ambacho hujulikana na kufahamika kwa wengi kama ajira, biashara, posho n.k. Unaweza ukawa na sababu nyingi za kwanini kila siku unaenda kufanya kazi. Lakini kama haupo huru kifedha, kujiingizia kipato ndio azimio kuu la kazi.

Wito.

Neno “wito”linawakilisha maslai binafsi, kile anachopenda, kinachomvutia,na kumsukuma mtu. Wito sio kitu ambacho wewe unataka  kufanya bali ni kile ambacho unahitaji kufanya. Hiki ni kitu ambacho huwa kina mguso mkubwa sana ndani yako.

 Lakini licha ya hilo wito nao unaweza ukakuingizia kipato au ukawa kazi pia. Na wito unaweza kuja kupitia maeneo mbalimbali kama vile: sanaa, usanifu, au shughuli zozote zile za kiubunifu (kwa mfano; uandishi,uchoraji n.k.)

Hata hivyo, wito wa kweli na wenye nguvu ni ule wito wa utumishi. Huu ni wito wenye nguvu kubwa sana. Na kupitia wito huu ndipo tunapokutana na huduma kadha wa kadha za kujitolea kama vile kufundisha,kufanya kazi pamoja na watoto na wazee,kutoa misaada mbalimbali ,na hata kutaka kuleta tofauti katika jamii n.k.

Mpaka hapo tunaweza kuona tofauti kuu iliyopo kati ya kazi na wito ni kwamba;kazi ni kwa ajiri ya kipato,na wito ni kwa ajiri ya ukinaifu au utoshelezi. Lakini inaweza ikatokea kuwa ukawa unaipenda sana kazi yako kiasi kwamba upo radhi kuifanya hata bure(kama una uwezo wa kufanya hivyo), katika hali ya namna hiyo hapo kazi huwa inabadilika na kuwa wito. Na ikiwa wito utaanza kuzalisha faida, basi nao unabadilika na kuwa kazi vilevile,Na huo ndio uhusiano na tofauti iliyopo kati ya kazi na wito.

Naam ama kwa hakika nimatumaini yangu kuwa itakua tumefahamiana vizuri kabisa kuhusu uhusiano kati ya kazi na wito.

Usikose kufuatilia magazine yetu kuanzia jumatatu hadi ijumaa utapata mambo mengi ya kujifunza kimaisha nakutakia maandalizi mema ya siku kuu ya mwaka mpyaaa!!!!!!!!!!!!.

 


Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Saphinia Suleiman

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, career, skills development and technology.


Latest Post