Ugonjwa wa ajabu wawakumba wanafunzi wa kike Kenya

Ugonjwa wa ajabu wawakumba wanafunzi wa kike Kenya

Ugonjwa wa ajabu wa maumivu katika magoti na kushindwa kutembea umewakumba wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Eregi iliyopo Kaunti ya Kakamega nchini Kenya ambapo takribani wanafunzi 95 hadi jana usiku Jumanne Oktoba 4, 2023 waliathiriwa na ugonjwa huo.

Hata hivyo, maofisa wa afya na elimu wa kaunti hiyo walivyotembelea shule hiyo walikataa ombi la wadau wengi waliopendekeza kufungwa kwa shule hiyo.

Haya yanajiri huku baadhi ya wazazi wakiruhusiwa kuwaondoa watoto wao shuleni baada ya baadhi ya wanafunzi kufanya fujo na kuharibu magari ya serikali ya maofisa walioenda kuwatembelea shuleni hapo.

Mkurugenzi wa Elimu Kanda ya Magharibi, Jared Obiero alisema baadhi ya wazazi waling’ang’ania kurudi nyumbani na watoto wao, hali iliyosababisha baadhi ya wanafunzi kufanya fujo na kuanza kuwarushia mawe viongozi wa serikali waliokuwa shuleni hapo.

“Baadhi ya vioo vya madirisha ya magari yetu viliharibiwa na tukawaruhusu wazazi ambao walitaka kuwapeleka watoto wao nyumbani kusaini kufanya hivyo. Kwa wanafunzi ambao wazazi wao hawakufika shuleni na wale ambao wazazi wao hawakutaka wasimamishe masomo walisalia na masomo yataendelea kama kawaida kwa wiki tatu zilizosalia.

 

“Kimsingi, shule haijafungwa. Masomo yataendelea kama kawaida isipokuwa kwa wanafunzi wachache ambao walichukuliwa na wazazi wao,” alisema Obiero.

Mkurugenzi wa Huduma za Matibabu Kaunti ya Kakamega, Dk Steven Wandei alisema ugonjwa huo wa kuambukiza unaweza kuangamiza familia nzima ikiwa hautadhibitiwa vyema.

"Tunahitaji kujua ni nini kinawasumbua wasichana wetu na kugundua sababu yake kabla ya kuwaruhusu wanafunzi waliobaki kurudi nyumbani na kuchanganyika na ndugu zao wengine. Itakuwa hatari ikiwa tutaruhusu wanafunzi kurudi nyumbani wakati ugonjwa huo ni wa kuambukiza,” alisema.

Takriban wanafunzi 62 walilazwa katika hospitali mbalimbali kaunti ya Kakamega Jumatatu usiku baada ya kuambukizwa ugonjwa huo.

Ugonjwa huo bado ni mfupa mgumu unaoendelea kuzisumbua shule za Mkoa wa Magharibi ambapo zaidi ya wanafunzi 500 kutoka Shule ya Mukumu wasichana na wavulana 100 kutoka shule ya Butere wavulana kulazwa hospitalini kutokana na kuzuka kwa ugonjwa huo.

Haya yanajiri huku kukiwa na tuhuma kwamba baadhi ya wanafunzi hao walikuwa wakijifanya kuwa wagonjwa kwa hofu ya mitihani ya mwisho wa mwaka.

Mjumbe Mtendaji wa Afya wa Kaunti ya Kakamega, Dk Bernard Wesonga ambaye aliongoza timu ya maofisa wa afya kutathmini shule

hiyo, alisema wanafunzi walioathiriwa walipata maumivu katika magoti yao na hawakuweza kusimama wala kutembea.

“Huu ni ugonjwa wa ajabu sana lakini bado tunachunguza ili kujua chanzo chake. Sampuli za choo zimepelekwa katika maabara za kaunti za Kisumu na Nairobi ili kujua ugonjwa huo na chanzo chake,” alisema Dk Wesonga.
.
.
.
#MwananchiScoop
#BurudikaNasi






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags