Chama Wataalamu na Wanataaluma wa Ustawi wa Jamii Tanzania (Taswo) kimempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kitendo cha kuonyesha nia na umuhimu wa kuitenganisha Idara ya Kuu ya Maendeleo ya Jamii na Afya.
Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa Taswo Awadh Mohamed ambapo alisema hatua hiyo aliyoichukua Rais Samia itasaidia kuboresha utekelezaji wa majukumu ya hizo idara mbili kwa kuwa zimebeba majukumu makubwa.
Taswo wametoa pongezi hizo ikiwa ni siku moja imepita tangu Rais Samia kutangaza uamuzi huo ili kutoa msukumo katika utekelezaji wa mipango na sera za masuala ya usawa wa jinsia.
Mohames alisema kutenganishwa kwa sekta hiyo ni wakati muafaka kwa sekta ya ustawi wa jamii kupewa uzito wa kipekee kuanzia ngazi ya taifa hadi Mamlaka za serikali za mitaa na kujenga kizazi chenye usawa kama yalivyo malengo ya Rais na malengo ya dunia.
Alifafanua kuwa utekelezaji, ufuatiliaji, usimamizi na uratibu wake umekuwa na changamoto katika kuwafikishia huduma bora za ustawi wa jamii wananchi hasa makundi maalum na watu wenye uhitaji hali inayosababisha kukosa kizazi chenye usawa.
Mohamed alisema katika kufanikisha malengo ya Rais Samia ikiwemo kuwepo kwa "Kizazi chenye usawa" kama sehemu ya Tanzania kutekeleza lengo la maendeleo endelevu kidunia na kuboresha huduma za ustawi wa jamii na maendeleo ya Jamii nchini.
"Katika idara kuu ya maendeleo ya Jamii kwenye awamu ya sasa kumekuwa na majukumu mengi zaidi mbali na afya ikiwemo huduma za ustawi wa jamii ambazo ni kubwa kwa majukumu yake," alisema
Mohamed alisema kimsingi huduma za ustawi wa jamii zimekuwa ni huduma mtambuka toka Uhuru na ni muhimu katika kuzuia matatizo ya kijamii yanayoweza kuathiri jamii na hasa makundi maalum.
Aidha, alisema kwa miaka mingi sekta ya ustawi wa jamii nchini haijapewa nafasi inayostahili kimuundo na hivyo kuathiri huduma za ustawi wa jamii kwa makundi yote yaliyotajwa licha ya kuwa na sera, sheria na miongozo mbalimbali inayoongoza utoaji wa huduma hizo.
"Kwa mfano kutokuwepo na idara kamili ya ustawi wa jamii katika ngazi ya Halmashauri imesababisha kukosa kifungu maalumu cha kupangiwa bajeti ya kutosha kumekuwa na changamoto ya kuwasilisha masuala ya ustawi wa jamii kwenye timu ya menejementi ya Halmashauri kwa ukamilifu," alisema Mohamed.
Leave a Reply