Takriban watu sita wameuawa na wengine 81 kujeruhiwa katika mlipuko katika eneo lenye shughuli nyingi katikati mwa Istanbul, mamlaka ya Uturuki imesema.
Mlipuko huo ulitokea mwendo wa saa 16:20 kwa saa za huko (13:20 GMT) kwenye barabara ya maduka katika eneo la Taksim Square, gavana wa jiji la Uturuki Ali Yerlikaya alisema.
Mshukiwa sasa amekamatwa, Waziri wa Mambo ya Ndani alisema. Makamu wa Rais Fuat Oktay awali alisema mlipuko huo ulidhaniwa kuwa ni shambulio la kigaidi lililotekelezwa na mwanamke. Rais Recep Tayyip Erdogan alisema wahusika wataadhibiwa.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Istanbul, alilaani kile alichokiita "shambulio baya" na kusema kulikuwa na "harufu ya ugaidi".
Waziri wa Sheria Bekir Bozdag aliviambia vyombo vya habari vya Uturuki kuwa mwanamke mmoja alikuwa amekaa kwenye benchi katika eneo hilo kwa zaidi ya dakika 40, na kuondoka dakika chache kabla ya mlipuko huo kutokea.
Siku ya Jumatatu asubuhi, Waziri wa Mambo ya Ndani Suleyman Soylu alisema mtu anayeshukiwa kuacha bomu amekamatwa na polisi, na kukishutumu Chama cha Wafanyakazi wa Kurdistan (PKK) kwa kuhusika.
Kundi la PKK ni kundi la wanamgambo linalotaka kuwepo kwa taifa huru la Wakurdi ndani ya Uturuki. Umoja wa Ulaya na Marekani wanalichukulia kama shirika la kigaidi. Hadi sasa hakuna aliyedai kuhusika na mlipuko huo.
Waziri wa serikali Derya Yanik aliandika kwenye tweet kwamba mfanyakazi wa wizara ya serikali na binti yake mdogo walikuwa miongoni mwa waathiriwa.
Leave a Reply