simulizi

Simulizi

Na Innocent Ndayanse

“Nimekufanyia hivyo tu kwa kuwa uko na msh’kaji wangu, Kipanga,” Masumbuko alisema. Kisha kama aliyekumbuka kitu, akamuuliza, “Kwani leo umemwacha wapi?”

“Hayupo hapa Dar,” Panja aliongopa. “ Kaenda mikoani. Labda atarudi baada ya wiki moja, hivi.”

Panja hakuwa tayari kugusia mkasa kati yake na Kipanga hata kidogo. Alitaka iwe siri, zaidi aliyejua ni Hilda tu! Nani mwingine ajue? Na kwa nini awepo mwingine wa kujua?

Alitoka hapo huku moyo wake ukiwa umesuuzika. Sasa alijiona kapiga hatua moja mbele katika mafanikio ya utekelezaji wa mpango  wake. Hakupanda tena daladala, badala yake alikodi teksi ya kumrudisha nyumbani, Kinondoni.

Akiwa njiani alinunua magazeti mawili, moja lililoitwa KIMBEMBE likiwa na habari za udaku huku jingine, HAMASA likiwa ni katika daraja la yale yanayoitwa magazeti makini.

Akiwa ameketi kwa utulivu ndani ya teksi hiyo, kushoto mwa dereva, Panja alianza kupitia vichwa vya habari vya magazeti hayo harakaharaka na kujikuta akivutwa na  kichwa cha habari katika gazeti la KIMBEMBE kilichochukua uzito wa juu katika ukurasa wa mbele; ‘BILIONEA’ AGOMBANIWA NA WANAWAKE UBUNGO.

Mara nyingi aliyapenda magazeti ya udaku kwa kuandika habari za ajabu-ajabu mathalani matukio ya fumanizi kwa wanandoa na matukio ya burudani za dansi, bongo fleva  na taarabu.

Akaamua kuisoma habari hiyo  ya ‘BILIONEA’kwa undani kabla ya kuendelea na nyingine.

Ilikuwa ni habari iliyosema kuwa mtu mmoja ambaye amepanga chumba katika ‘gesti bubu’ iliyoko eneo la Ubungo amekuwa akisababisha wanawake wapigane kwa ajili yake katika kile kilichoaminika kuwa ni kugombea penzi.

Ilidaiwa kuwa mtu huyo alikuwa na siku takriban thelathini tangu aingie ndani ya gesti hiyo na alionekana kuwa ana pesa lukuki kutokana matumizi yake makali yaliyohusisha unywaji pombe na uhongaji wa pesa nyingi kwa wanawake.

Mtu huyo alikuwa na desturi ya kutotembea-tembea mitaani na kama alitoka ndani ya gesti hiyo basi hakwenda zaidi ya mita hamsini kununua magazeti. Pia katika matumizi yake hayo ya kutisha, ‘bilionea’ huyo alidaiwa kuwa alikuwa akijichimbia chumbani na kugida bia na kuku kadhaa wa kuoka na nyama ya mbuzi huku akiwa na wanawake wawili, watatu hata wanne ambao mitaani hujulikana bayana kuwa ni watu walio tayari kwa mwanamume yeyote na kwa kutendwa vyovyote kulingana na uwezo wa kiuchumi alionao mwanamume husika.

Kilichomshangaza zaidi Panja ni kiwango cha shilingi 50,000 hadi 100,000 zilizodaiwa katika habari hiyo kuwa ndicho kiwango alichotoa kwa kila mwanamke aliyebahatika kuingia chumbani humo na kumtuliza kiu yake.

Ilikuwa ni habari iliyomshangaza na kumsisimua Panja kwa kiasi kikubwa. Akayainua macho na kutazama mbele, kisha akamgeukia dereva na kusema, “Kuna watu wanaojua kula raha hapa duniani. Wameiweka dunia mikononi mwao.”

Dereva aliachia tabasamu dhaifu bila ya kumtazama Panja. Kisha akahoji, “Kwa nini unasema hivyo? Au umesoma hiyo habari ya kwenye gazeti la KIMBEMBE? ”

“Nd’o maana’ake,” Panja alijibu. “Ukisikia mafisadi, basi huyu ni mmojawao. Mtu huwezi kutumia pesa kwa mfumo huu kama kweli una uchungu nazo. Au vinginevyo, tuchukulie kuwa stori hii ni ya kutengenezwa kibiashara ili gazeti linunulike.”

“Hapana!” dereva alipinga haraka. “Hiyo stori ni ya kweli! Ni ukweli mtupu! Hata mimi namjua huyo jamaa. Majuzi nilimpeleka mteja mmoja kwenye gesti hiyo, nd’o nikasikia watu wakimzungumzia huyo ‘bilionea.’ Kwa bahati, kabla sijaondoka jamaa alitoka nje na kwenda kununua gazeti. Ndipo msh’kaji mmoja akanitonya.

“Sikuweza kuimaki sura yake kwa kuwa alikuwa amevaa miwani mieusi, na hata hivyo sikuwa na haja ya kumjua. Yaani pale kila mtu anamzungumzia. Sijui kazichota wapi pesa za kutupa kiasi kile. Unaweza kukuta ni jambazi au fisadi , nd’o maana kajichimbia gesti muda wote baada ya dili lake kuwini.”

Sentensi hiyo ya mwisho ilimpeleka Panja mbali kimawazo. Akamtazama dereva huyo kwa macho makali. “Unamfahamu?” hatimaye alimuuliza.

“S’o kwamba namfahamu, nilimwona tu pale kwenye gesti. Kwan’vipi?”

“N’na shida naye,” Panja alijibu kwa utulivu.

“Una shida naye?” dereva alishangaa. “Kwani unamjua huyo jamaa mwenyewe?”

“Sina uhakika, lakini nadhani ni huyohuyo anayezungumziwa. Jamaa mwenyewe si ni mrefu?”

“Ndiyo.”

“Pandikizi la mtu?”

“Hivyohivyo! Amekaa kibaunsa-baunsa.”

“Kidevuni yukoje? Ana sharafa?”

“Anaonyesha hivyo, lakini siku nilipomwona hakuwa na ndevu.”

“Una siku ngapi tangu ufike pale?”

“Haijapita hata wiki. Kama siku nne, tano hivi.”

“Kichwani yuko vipi?” Panja aliendelea kudadisi.

“Ki-vipi?”

“Ana nywele au hana?”

“Ana mzinga wa para, mwanangu.”

“Macho yake?”

“Ningeyaonaje wakati nimekwambia alikuwa katinga miwani ya giza?” dereva naye  alihoji huku akibadili gia na kupunguza mwendo. Walikuwa wamekaribia kwenye taa za Usalama Barabarani makutano ya barabara za Rashid Kawawa na Ali Hassan Mwinyi.

“Wakati anatembea ulimwangalia vizuri?”

Dereva aliitika kwa kutikisa kichwa.

“Uliicheki tembea yake?”

Taa ya kuwaruhusu iliwaka. Dereva hakulijibu swali la Panja, akili ilizama barabarani. Wakashika Barabara ya Rashid Kawawa. Mbele kidogo ndipo dereva akaipata sauti yake: “U

meulizia tembea yake, sio?”

Yeah.”

“Anatembea kibabe-babe.Yaani anaonyesha kujiamini sana, kama unavyojua, mtu akiwa na tuvijisenti kidogo, basi anajiona kaibeba dunia mikononi mwake. Wengine huwa hawajui kama kuna suala la kufa duniani.”

Uso wa Panja ulichanua tabasamu kubwa, tabasamu lililofuatiwa na tamko la chini sana: “Ni mwenyewe.”

Ikawa ni kauli iliyomfanya dereva ajenge imani kuwa kuna kazi nyingine ya kumpeleka Panja huko Ubungo. Papohapo akamuuliza, “Vipi, twende Ubungo, mzee?”

Panja alifikiri kidogo kisha akasema, “No. Twende kwanza nyumbani. Suala la Ubungo halikuwa kwenye programu. Limezuka-zuka tu. Kama tutakwenda, basi hilo nitalijua baada ya kufika kwanza home.”

Dakika chache baadaye dereva aliegesha gari kando ya nyumba moja chakavu, jirani na Kanisa la Kilutheri, Usharika wa Kinondoni.

“Subiri,” Panja alimwambia dereva huku akiteremka na kufuata uchochoro uliomwingiza ndani zaidi ya eneo hilo. Alikuwa makini, hakutaka huyu dereva apajue kwake. Bado hakutaka kujiweka wazi kwa kila mtu na hasa kwa akiamini kuwa bado Polisi inamsaka.

Itaendelea……………………….


Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Detricia Pamba

A Digital Journalist, Content Creation Executive at Mwananchi Communications Ltd and Chief Editor of Mwananchi Scoop. I'm also writes stories around Technology, every Wednesday on Mwananchi Scoop. My other famous segments on Mwananchi Scoop include LISTI and WHO’S HOT.


Latest Post