Shamsa (Tudarco): Usipoweza kuendesha biashara ndogo hata kubwa hutaweza

Shamsa (Tudarco): Usipoweza kuendesha biashara ndogo hata kubwa hutaweza

“Usipoweza kuendesha biashara ndogo hata upewe kubwa au uanzishe yenye maji mkubwa hutoweza kuendesha kwa ubora na ufanisi unaotakiwa,”

Hiyo ni kauli ya Shamsa Khalfan, mwanafunzi kutoka Chuo Kikuu kishiriki cha Tumaini Dar es salaam (TUDARCo) ambaye pia ni mfanyabiashara anayeuza manukato (perfume) mbalimbali.

Shamsa anachukua Shahada ya Habari na Mawasiliano kwa Umma ana kampuni yake inayojulikana kwa jina la Fragrance clan wamejikita kuuza na kusambaza perfume za mafuta (oil perfume).

Akizungumza na MwananchiScoop, Shamsa anasema biashara hiyo ni nzuri mno na imeweza kumsaidia kukabiliana na vitu mbalimbali katika maisha yake ya kila siku.

Anasema kupitia biashara hiyo imeweza kumpatia kipato ambacho anakitumia kujilipia ada hivyo kuwapunguzi baadhi ya majukumu wazazi na walezi wake.

“Vilevile hainisaidii mimi peke yangu kwani kwa sasa nimefanikiwa kuajiri watu kama mawakala wanaokuja kuchukua mzigo kwa gharama nafuu kisha wanaenda kuuza na kurejesha fedha na kuchukua tena mzigo mwingine,” anasema Shamsa

Hata hivyo anasema wazo la kufanya biashara hiyo ya manukato alilipata baada ya kuwaza harufu nzuri huongeza hadhi kwa vijana na wazee, pia perfume imekuwa moja ya bidhaa ni muhimu kama vile mafuta ya mwili na sabuni.

“Baada ya kulitambua hilo niliona nisikae mikono mitupu bila kujishughulisha kwani hata waliofika pakubwa walianza padogo, na usipoweza kuendesha biashara ndogo hata upewe baishara kubwa vipi hutoiweza kuiendesha.

“Niliamua kuanza kufanya biashara tena kwa kuanzia chuo, nilianza kwa kutembeza mnamo mwaka 2020, ila Januari mwaka huu 2022 niliweza kuwa na ubia na saloon moja ambayo ninaweka perfume zangu katika duka lao,” anasema

Changamoto

Anafubguka kwa kusema hakuna biashara isiyo na changamoto ila jamii hasa wafanyabiashara wote watambue kuwa kila changamoto inasaidia ukuwaji wa biashara yake na kuifanya ikomae vizuri kwa namna moja au nyingine.

Anasema kwa upande wake wa perfume zina changamoto katika upatikanaji wake kwani anaweza kuagiza mzigo Dubai lakini kuna wakati unaweza kuja ukiwa umekamilika au haujakamilika.

“Vilevile unaweza ukachelewa kufika, hii inakua kero kwa wateja wanaokuamini na inasitisha shughuli za maendeleo, kwa kuwa huwezi kupata fedha kwa wakati na kuziingiza katika mzunguko wa biashara zako zingine,” anasema

Faida alizozipata

Anasema faida alizozipata kupitia biashara hiyo, kwanza imemuwezesha kupata fedha na kukutana na wadau mbalimbali ambapo klupitia kwao wamenipatia elimu ya kidigitali, namna ya kukuza masoko na kutunza fedha.

Pia anasema imemuwezesha kufahamiana na wafanyabiashara wakubwa ambao wanamuhamasisha yeye apambane na afike pale walipofika wao.

“Nimeweza kufanikiwa kupata baadhi ya wawekezaji wanaohitaji kuwekeza katika biashara hii,” anasema

Ushauri kwa vijana

Anasema vijana wanapswa kutambua kuwa hakuna kizingiti katika kufikia malengo aliyojiwekea, hivyo wanapaswa kujituma na kutokata tamaa.

“Hakuna kukata tamaa kwani hakuna mafanikio yanayokuja kirahisi, pia vijana wenzangu msiwe watu wakukaa nakusubiri vije wanapaswa kuvifuata,” anasema

Hata hivyo anasema kitu ambacho anapenda kufanya nikuweza kujaribu na kujifunza vitu vipya mfano kuendesha pikipiki, kujifundisha namna ya utengenezaji wa mafuta ya mwili na shampoo hii inaniwekea nguvu katika kuanzisha biashara mpya.

“Natamani kuja kuwa mfanyabiashara mashuhuri na pia napenda kuja kuwa mwandishi wa habari niliobobea, kwani utangazaji na uandaaji wa makala zenye maudhui kadha wa kadha hunipa furaha,” anasema na kuongeza

“Napenda hivi vitu kwani naona ni vipawa vya Mungu alivyonibariki kwani nilitokea kuvipenda tangu nikiwa mdogo,” anasema






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post

Latest Tags