Na Magreth Bavuma
Mambo niaaaaje, wanangu wa moyoni, segment yako pendwa kabisa ya unicorner sehemu moja tu ambayo tunapangana na kupanguana, kujifunza na kuelimishana kuhusu dunia yetu ya wanavyuo, Sema hii ya leo ni tuiite kuvuta mtutu.
Kuna wakati tunajikuta tukitamani kuwa wajasiriamali na kubadili mawazo yetu kuwa biashara halisi, Lakini tunashindwa kutokana na kukosa ni wapi pakuanzia, na wakati mwingine kushindwa kujua kwamba tumebeba hazina ambazo jamii inazihitaji.
Embu tuone ni namna gani unaweza kufanya hivyo wakati ukiwa chuoni, lets goooooo!
Kwanza kabisa tambua wazo lako:
Unatakiwa kujua kwamba ujasiriamali huanza na wazo, hivyo kabla ya kuanza safari ya ujasiriamali lazima uwe na wazo zuri, think outside the box na uwe creative, fikiria unataka kufanya nini kwa kuzingatia changamoto au hitaji katika jamii ambalo unataka kulitatua.
Kuna mambo mengi yanayowezekana kama vile kuanzisha bidhaa au huduma mpya, kutoa huduma ya kipekee au hata kuvumbua teknolojia mpya.
Ikiwa unataka kutoa huduma ya ushauri, kuwa mbunifu wa mavazi, kuwa photographer au interior designer wazo ndio msingi na kitu muhimu lakini pia wazo lako liambatane na msukumo wa ndani.
Fanya utafiti na uchambuzi:
Baada ya kubaini wazo lako, itakubidi ufanye utafiti na uchambuzi wa soko. Tambua wateja wako walengwa (targeted customers), tathmini washindani wako, na elewa mahitaji ya soko.
Fanya juu chini ujifunze kila kitu kinachohusiana na sekta unayotaka kujihusisha nayo, tafiti makosa na mafanikio ya watu wengine, hii itakuwezesha kuwa na mpango madhubuti wa biashara yako. Uchambuzi wa kina utakusaidia kuelewa vizuri fursa na changamoto zilizopo na kukupa msingi imara wa kuanza safari yako ya ujasiriamali.
Tengeneza mpango wa biashara (business plan):
Kuwa na wazo tu haitoshi lazima utengeneze mpango wa biashara yako, hapa ndipo unapoweka malengo yako, mkakati wa masoko, muundo wa biashara, na maelezo mengine muhimu.
Weka mpango wako wa biashara kuwa wa kusisimua na wa kuvutia kwa kutumia infographics, chati, na mchoro rahisi, jieleze kwa mtindo wa kipekee na weka msisitizo juu ya nini kinakufanya uwe tofauti na washindani wako.
Kumbuka mpango wako wa biashara ndio unakupa ramani halisi na mwelekeo wa mafanikio ya biashara yako.
Tambua upatikanaji wa rasilimali (access to resources):
Kuanza biashara yako inahitaji rasilimali jua njia za kupata mtaji, hapa kwenye mtaji ndio wanavyuo wengi hukumbana na changamoto kwakuwa wao hudhani mtaji ni mpaka uwe na mamilioni ya pesa au uingie mikopo mikubwa la hasha unaweza kuwatumia ndugu, jamaa, na marafiki kwa kukusanya mtaji wako wa kuanzia, na kama si hivyo basi unaweza kupata mikopo ya benki, wawekezaji, au hata ufadhili wa kitaifa.
Tambua pia rasilimali zingine kama watu wenye ujuzi, washirika, au vituo vya ushauri wa wajasiriamali vinavyopatikana chuoni, jifunze kutumia rasilimali zilizopo kuzidi expectations zako.
Utekelezaji na uendelezaji:
Ni wakati wa kutekeleza wazo lako na kuifanya biashara yako iwe halisi, anza kwa hatua ndogo na usiogope kuthubutu, tengeneza sifa nzuri kwa wateja wako maana ndio watakuletea nyomi ya wateja wengine usiwachukulie poa marafiki wanao amua kukusupport katika biashara yako.
Tumia mitandao ya kijamii kama silaha yako ya kuifanya biashara itambulike zaidi, na shirikiana na watu wanaofanya biashara kama yako. Tumia pia njia kama matangazo kwenye groups za chuo au kuunda ushirikiano na vikundi vya wanafunzi, fanya kazi kwa bidi, uaminifu na kwa furaha.
Usiache kuendelea kujifunza:
Wanavyuo wengi hudhani kwamba kumiliki biashara inatosha lakini acha nikukumbushe ujasiriamali ni safari ya kujifunza kila siku ili upige hatua moja zaidi.
Jitahidi kujifunza kutokana na mafanikio na makosa yako, sikiliza mawazo na maoni ya wateja wako na fanya marekebisho (customer’s feedback matters). Endelea kujiongeza na kuwa mbunifu, jifunze kutoka kwa wajasiriamali waliofanikiwa na kuwa tayari kubadilika na kukabiliana na changamoto kwa uvumilivu na ujasiri.
Amini kwamba wewe ni mjasiriamali mwenye kipaji na dunia inakusubiri, toa wazo lako likafanye mabadiliko katika ulimwengu wa biashara.
Ujasiriamali ni safari ambayo hakuna mtu mwingine anayeweza kuifanya kwa niaba yako jiambie kwamba hakuna biashara isiyokuwa na changamoto, hasara zisikufanye uache kupambana mwanangu keep the energy high na usikate tamaa hata kwa sekunde moja, tunaishi kwenye dunia ambayo watu wanasubiri tu give up wapate cha kutusimangia USIKUBALI PAMBANA MPAKA MWISHO.
Bila nyie hakuna mimi, asanteni kwa kuendelea kuniweka mjini tukutane tena wiki ijayo kwenye corner yetu ya dunia ya wanavyuo “unicorner” tchaaaaaaoooo!!!!!!!
Leave a Reply