Safari ya Bi Star kutoka kwenye Taarab hadi kutesa anga za filamu

Safari ya Bi Star kutoka kwenye Taarab hadi kutesa anga za filamu

Waswahili wanasema vya kale ni dhahabu, watozi na wanagenzi wakafika mbali zaidi na kusema wakongwe hawafi 'legends never die'.

Hii imethibitika baada ya mwigizaji mkongwe Shamila Ndwangila 'Bi Star' kupiga story na Mwananchi Scoop huku akidai sanaa kwa sasa imebadilika tofauti na zamani, wasanii walikuwa wakipita kwenye vikundi ambavyo vilikuwa kama shule.

"Nilianzia kwenye kikundi cha sanaa kilichojulikana kama Tandale Arts Group ambapo nilipelekwa na mume wangu na wakati huo nilijiona ninakipaji cha kuimba zaidi kuliko kuigiza nilishatoa nyimbo kadhaa za Taarab ambazo zilichezwa kwenye vituo mbalimbali vya Radio,"amesema 

Baada ya kufika Tandale Bi Star anasema alikutana na mwigizaji Muhogo Mchungu ambaye alikua na ujuzi zaidi hivyo ni moja kati ya watu waliomshika mkono na kumwambia ana kipaji kikubwa hivyo asiache kupambania ndoto zake.

Hata hivyo baadaye likaanzishwa kundi la Kaole Sanaa Group ambapo Bi Star alikutana na wasanii kama Dr cheni, Kibakuli, Mama Nyamayao, Nyamayao, na wengine wengi. Anasema kaole waliishi kama familia na kazi zao zikaanza kuonekana kwenye televisheni huku akiutaja mchezo wa Fukuto kama uliomtengenezea njia.

Mbali na hayo mwigizaji huyo mkongwe ameonesha kuchukizwa na jinsi wasanii wa sasa wanavyoibuka bila kupita kwenye misingi na kusema wengi hawana vipaji kama ilivyokua kwao, bali wanaingia kwenye tasnia kwa ajili ya kupata kipato kwani sanaa kwa sasa imekua ajira kwa vijana wengi

Bi Star ni mama wa familia yenye watoto watatu wote mabinti lakini anasema licha ya yeye kurithi kazi ya uigizaji kutoka kwa shangazi yake lakini hakuna mtoto wake hata mmoja ambaye amefuata nyao zake kwenye kuigiza licha ya kwamba wote si wageni wa kamera.

Aidha Mwananchi Scoop ilipomuuliza Bi Star kama anafuatilia michezo alisema yeye ni shabiki wa Simba 

"Mimi ni shabiki mkubwa sana wa Mnyama Simba, mume wangu na watoto wangu wawili ni mashabiki wa Yanga lakini mimi naipenda Simba,"amesema

Kati ya mafanikio aliyopata kutokana na sanaa yake anasema ni kujenga ukaribu na watu wengi na kujenga nyumba ambayo anaishi na familia yake kwa sasa






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags