Sababu, njia ya kuondoa harufu mbaya mwilini

Sababu, njia ya kuondoa harufu mbaya mwilini

Tatizo la harufu mbaya mwilini inayohusisha jasho, ni changamoto inayowakabili wengi na huwa kero kwa wale wanaomzunguka mtu mwenye tatizo hilo.

Wengi wenye matatizo haya, hukosa kujiamini na mara nyingi hutengwa na watu kutokana na hali hiyo.
Ili kukabiliana na hali hiyo, wengi wenye matatizo haya wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali kulikabili tatizo, ikiwemo kutumia marashi, kuoga mara kwa mara bila kupata mafanikio.

Kuwa na harufu mbaya mwilini wakati mwingine huweka shakani mahusiano baina ya wapendanao na wengine kukimbiwa na marafiki.
Kinyume na wanavyoeleza wataalamu kuwa harufu mbaya mwilini ni tatizo, Bahati Laizer, mkazi wa Gongolamboto, anachofahamu wenye matatizo hayo chanzo chake pekee ni uchafu.

Anasema wapo watu hurudia nguo mara nyingi, hali inayochangia kuwa na harufu ambayo huwa kero kwa walio karibu nao.
Alex Fadhili, mkazi wa Tabata anasema marafiki zake aliowashuhudia kukumbwa na shida hiyo hukosa furaha.
Anaeleza kuwa wengi aliwaona wakitumia njia mbalimbali kukabili tatizo hilo, ikiwemo kupaka ndimu kwenye kwapa bila mafanikio ya kuondoa harufu hiyo.

“Baadhi niliowashuhudia bado waliendelea kubaki na matatizo hayo kwa sababu wanadanganywa mara tumia kitu fulani, mara hivi, unakuta wanakata tamaa wanabaki hivyo, wametumia gharama kubwa na sio kwamba ni wachafu, hapana. Mwili tu unaonekana kuwa na tatizo, akifanya kazi kidogo mwili unaanza kutoa harufu,” anaeleza.

Dk Happiness Biyengo anasema harufu mbaya mwilini ambayo huhusiana na jasho la mwili ni tatizo ambalo kitaalamu hufahamika Bromhidrosis au Osmidrosis.
“Kawaida jasho la mwili halitakiwi kutoa harufu na hii harufu mbaya hutokea pale tu jasho linapovunjwa na bakteria waishio mwilini,” anaeleza.
Anaeleza kuwa harufu mbaya haina kiwango, lakini inakuwa shida pale ikimkera mtu mwenyewe, watu wanaomzunguka, kuingilia kazi zake za kila siku na uwezo wa kuchangamana na jamii yake.

Anasema ngozi ya binadamu ina aina mbili za tezi zinazohusika na kutoa jasho, ambazo huitwa apocrine na eccrine na tezi hizi huhusishwa na harufu mbaya mwilini, ingawa apocrine huchukua nafasi kubwa zaidi.
“Tezi za apocrine hupatikana sehemu za kwapani, chini ya matiti na sehemu za siri. Jasho inapotoka kwenye tezi hii haina rangi wala harufu hadi pale ikiingiliwa na bakteria waishio kwenye ngozi.

“Tezi hizi huanza kufanya kazi hasa katika umri wa kubalehe na hii ndiyo sababu tatizo la harufu mbaya husumbua zaidi kundi la vijana,” anasema na kuongeza;
“Eccrine hupatikana sehemu zote za mwili, pia zenyewe hutoa jasho lisilo na rangi wala harufu, na mara nyingine hutoa jasho la harufu ya vyakula ambavyo mtu anaweza akawa amekula kama vitunguu swaumu, pombe, sigara na baadhi ya dawa,” anaeleza.



Chanzo cha harufu mbaya
Dk Happiness anaeleza mtu kutokuwa na usafi binafsi kama kusafisha mwili mara kwa mara, kuvaa nguo chafu, maambukizi ya vijidudu kwenye ngozi au vinyweleo vya ngozi ni sababu ya kuwepo kwa tatizo hilo.
Pia anasema utafiti unaonyesha tatizo la harufu mbaya ya mwili linaweza kurithiwa, akitaja magonjwa wa kisukari, tatizo la figo na ini.
“Aina ya harufu ambayo imekuwa ikiwakumba wengi ni harufu mbaya isiyoisha mwilini, kuwa na harufu mbaya muda mfupi baada ya kuoga, harufu kama samli au nyama mbichi kutoka kwapani,” anasema.


Nini cha kufanya ukiwa na tatizo
Kwa wenye tatizo hilo, Dk Happiness anashauri usafi binafsi kama kuoga na maji na sabuni angalau mara mbili kwa siku, pia kuondoa nywele zinazoota hasa sehemu za siri na kwapani.
“Mbali na hayo, mbinu nyingine anayotaja ni kutumia sabuni zenye uwezo wa kuua bakteria (antibacterial soaps), kuzingatia usafi wa nguo na kufua nguo vizuri,” anasema.

Pia kuepuka kurudia nguo chafu, kuvaa nguo zenye malighafi ya pamba, kuepuka kuwa na ngozi yenye unyevunyevu muda mwingi, yaani kukausha ngozi vizuri hasa sehemu za mikunjo,” anabainisha.

Dk Happiness anasema endapo mtu kahakikisha usafi na maelekezo yote ya awali na harufu kuendelea kuwepo, anatakiwa kuonana na daktari kwa uchunguzi zaidi, akitaja uwepo kwa tiba mbalimbali hospitali, ikiwemo kuondoa tezi zenye shida, dawa za kupaka na kutoa vinyweleo kwa ‘laser’.

Maeneo mengine
Akizungumzia maeneo mengine yenye kutoa harufu mwilini, Dk Ernest Winchislaus anataja kuwa ni mdomoni, sehemu za siri, miguu na shingoni.
Dk Winchislaus kutoka Idara ya Mafunzo na Utafiti na Magonjwa ya ndani Hospital ya Kanda ya Rufaa Mbeya, anaelezea harufu eneo la mdomo unatokana magonjwa, meno kutoboka,usafi na fangasi.

“Pia kwa maeneo ya siri, tatizo hili linatokea zaidi kwa wanawake chanzo nayo ni usafi kuwa mdogo na ugonjwa wa maambukizi kwenye via vya uzazi (PID),” anasema.

Eneo lingine ni makwapani, shingoni na miguuni anayotaja nako harufu inachangiwa na matatizo ya ngozi na usafi.
Pia Dk Winchislaus anaeleza shida nyingine ni mtu kuwa na harufu mithili ya samaki, “Trimethylaminuria( fish odor syndrome) - ni ugonjwa nadra sana ambao mtu hutoa harufu kama ya samaki aliyeoza, ni ugonjwa wa kurithi unaotokana na matatizo katika vinasaba za muhusika,” anaeleza






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags