Rapcha kutoka kutamani upadri hadi kuwa baba kijacho

Rapcha kutoka kutamani upadri hadi kuwa baba kijacho

Msemo wa hatupati tutakacho tunapata tujaliwacho ndiyo unaweza kuelezea ndoto ya mwanamuziki wa hip-hop nchini Cosmas Paul 'Rapcha' ya kutamani kuwa padri ilivyogeuka kuwa baba mtarajiwa maarufu kama baba kijacho.

Msanii huyu ameiambia Mwananchi kuwa wimbo wake mpya uitwayo 'Only God Knows' unaoelezea mzazi akituma ujumbe kwa mwanaye aliye tumboni unamuhusu kwa asilimia mia moja

"Ujumbe uliopo kwenye wimbo wangu ni meseji ya mzazi kwenda kwa mtoto wake aliye tumboni ambaye anasubiri kumuona kwa mara kwanza.

Huo ujumbe ninahusiana nao kwa asilimia 100 kama siyo 99,"amesema

Amesema awali alikuwa na ndoto ya kuwa padri lakini ndoto zake zilikatika na ndipo akaingia kwenye muziki.

"Nilitakiwa kwenda kusoma seminari baada ya kumaliza elimu ya msingi na nilikuwa sijahangaika na kitu chochote maana nilitaka niwe padri mipango yote ilikuwa tayari imekamilika lakini sehemu ambayo nilitakiwa kwenda ikawa imefungwa kwa sababu ambazo zilitolewa kwa kipindi hicho ikabidi niende shule ya kawaida.

"Hapo ndipo maisha ya muziki yakaendelea, kumbe ningekuwa padri nisingekuwa na nafasi ya kuwa na mtoto nisingekuwa na nafasi ya kuonana naye na kuongea naye kwenye ule wimbo kwa hiyo ilitokea nisiwe padri ili nije kukutana naye," amesema.

Kutokana na 'Visualizer video' ya wimbo huo ambao umepandishwa kwenye mtandao wa Youtube siku tano zilizopita ikionesha picha za watu mbalimbali, jumbe ambazo Rapcha aliwahi kuwasiliana na P Funk na hata zile akiwa na Lady Jaydee, Rapcha amesema video hiyo ni maalumu kwa ajili ya kukumbusha watu maisha yake ya nyuma.

"Ile video ni sehemu ambayo inakurudisha nyuma maisha yangu kipindi nikiwa mdogo mpaka kipaji changu hadi hapa nilipo, hata mtoto wangu akija kuona ataona ndugu zangu kuna namna inaonekana nyumba ambayo tunakaa Shinyanga ambayo ilijengwa muda lakini mimi nilikuja kuimalizia baada ya kuingia kwenye muziki kwa hiyo video ina sehemu kubwa katika maisha yangu," amesema

Mbali na hayo amesema baadhi ya mistari ya ngoma hiyo ameiweka kwa lengo la kuwainua watu waliokata tamaa na kujutia nafsi zao kwa waliyowahi kufanya.

"Kuna mstari nimeimba wa kumuinua mtu yeyote ambaye yupo kwenye majuto ambayo amewahi kufanya katika maisha yake hata mimi sitegemei kurudia makosa ambayo niliwahi kukoseka huenda kwa kukusuidia au bahati mbaya na nisingependa yatokee hata kwa mwanangu ambaye nimeongea naye kwenye 'Only God Knows',"amesema

Ikumbukwe kuwa Rapcha anatamba na nyimbo kama vile Lissa I, Lissa 2, 40 Missed Calls, Uwongo, Fungua, Nirudi Home na nyingine






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags