Pele kusherehekea christmas hospitalini

Pele kusherehekea christmas hospitalini

Timu ya madaktari wanaomtibu nguli wa soka wa Brazil, Edson Arantes do Nascimento maarufu kama Pele, imesema nyota huyo atabakia hospitali wakati wa siku kuu ya Krismasi akipatiwa matibabu ya saratani yake inayozidi kuwa mbaya pamoja na matatizo ya figo na moyo.

Hospitali anayotibiwa Pele, ya Albert Einstein ya mjini Sao Paolo, imesema Pele mwenye umri wa miaka 82 anahitaji uangalizi wa hali ya juu kutokana na kufeli kwa figo na moyo.

Hospitali hiyo imeripoti kuwa saratani ya Pele imezidi lakini hakuwa katika kitengo cha wagonjwa mahututi.

Pele anayezingatiwa na wengi kuwa mwanasoka bora wa wakati wote, alilazwa hospitali mjini Sao Paulo Novemba 29 kutoka na kile timu yake ya madaktari ilisema kutathmini tena matibabu yake ya mionzi, ambayo amekuwa akipatiwa tangu alipofanyiwa upasuaji kuondoa uvimbe kwenye utumbo mwezi Septemba 2021.

Madaktari pia wamemgundua Pele kuwa na maambukizi kwenye mfumo wa kupumua.

Mapema mwezi huu, mabinti wa Pele, Kely Nascimento na Flavia Arantes walijaribu kuwahakikishia mashabiki kuhusu afya yake, wakikanusha ripoti kwamba Pele alikuwa amewekwa kwenye huduma za mwisho wa maisha, baada ya wafuasi hao kufanya mkesha nje ya hospitali.

Kely Nascimento, mmoja wa mabinti zake alisema watabaki na baba yao hospitali wakati wa Krismasi.

"Tuliamua pamoja na madaktari, kwa sababu nyingi, kwamba itakuwa vyema kwetu kubaki hapa," Kelly aliandika kwenye mtandao wake wa Instagram.

Chanzo DW

 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags