Nikamkuta walevi wamempa za uso

Nikamkuta walevi wamempa za uso

Nakumbuka ilikuwa ni siku ya sikukuu ya Idi.  Tulikuwa mahali na jamaa yangu mmoja tukizungumza huku tukinywa soda. 

Wakati tukiwa tumekaa hapo kwenye bar, walikuja vijana watatu ambao walikuwa wamelewa sana. 

Mmoja kati ya wale vijana walikuja hadi pale kwenye meza yetu na kuchukua soda ya jamaa yangu na kuinywa yote. Halafu alirudisha chupa mezani na kusema, "haya amua sasa, kama vita ya Aleppo-Syria niko tayari. Siyo mnajifanya nyie watoto wa wakubwa, mnaiba fedha zetu tu na kutanua mjini hapa. "

Niliona jamaa yangu akiinuka, labda kupigana na yule kijana.  Lakini  nilimzuia na akarejea kitini. Halafu yule kijana mlevi alichukua na ile soda yangu na kuinywa yote. Halafu aliniuliza kama ninabisha. Nikamwambia kwamba sibishi. Jamaa yangu alitaka kuinuka tena kumtandika yule kijana mlevi lakini nilimzuia kwa nguvu zangu zote, kwa sababu sikutaka yule kijana mlevi ajue kuwa jamaa yangu anataka kupigana kwa sababu yeye ndicho alichokuwa anakitaka. 

Wale vijana walipoona tumetulia waliamua kuondoka lakini yule jamaa yangu alikuwa amekasirika sana, kiasi kwamba hakusema chochote kwa muda ule. 

Baadaye alianza kunilaumu kwamba nilikosea kumzuia asimfundishe yule kijana mlevi adabu.

Nilimuuliza jamaa yangu kama alishawahi kunywa pombe maishani mwake. Alinijibu kwa mkato, ‘ya kazi gani?’ Nilimwambia kwamba, yule kijana ni mlevi tu, hakufanya yale kwa makusudi. Nilimwambia pia kwamba, yule kijana ni mtu mwenye utashi wake na mitazamo yake ambayo sisi hatuwezi kuibadili ili itufae. Jamaa yangu alionekana kama anasikiliza kelele za mtoto anayejifunza kuzungumza.

Tuliendelea na mazungumzo yetu na kuachana na hilo la yule kijana mlevi na wenzake. Kiasi cha nusu saa baadaye nilishikwa na haja ya kwenda msalani kutabawali. Hapo karibu na meza tuliyokuwa tumekaa kulikuwa na wateja walioonekana kama vile walikuwa tayari wamelewa. 

Walikuwa wanabishana kwamba, mtu asiyekunywa pombe ni masikini, lakini mtu mwenye fedha ni lazima anywe, angalau kidogo.

Bila shaka ulikuwa ni ubishi wa kilevi kwa sababu haukuwa na chembe ya mantiki. Kumbe muda wote wakati watu wale wakibishana, jamaa yangu alikuwa anaumia sana, bali alikuwa akishindwa kuingilia ule ubishi kwa sababu alijua ningemzonga na nisingeruhusu jambo hilo kirahisi.

Wakati niko huko maliwatoni nikijisaidia nilisikia watu wakibishana kwa sauti kali sana. Nilimaliza kujisaidia na kwenda upande wa jikoni ili kuagiza nyama choma. Nikiwa nachagua nyama choma nilizidi kusikia kelele hizo. Lakini nilijua ni wale wateja wanaobishana kuhusu kunywa pombe na fedha.

Wakati naondoka kwenye nyama choma kurudi pale kule nilikokaa na jamaa yangu nikaanza kusikia milio ya chupa na kelele na mtu akiugulia maumivu.

Nawaambia amini usiamini, nilipofika pale nilimkuta jamaa yangu akiwa ameshikwa na watu, damu zinamchuruzika kama maji.

Nilimkimbilia na kuuliza kulikoni. Niliambiwa kwamba yule jamaa yangu alikuwa akibishana na wale wateja wa meza ya jirani na mara akaanza kupigana na mmoja kati ya wale watu akampiga na chupa ya bia kichwani na baada ya kitendo kile wale wateja wakakimbilia kwenye gari lao na kuondoka zao.

Ilibidi nianze kazi nyingine ya kwenda hospitali kwa ajili ya matibabu ya jamaa yangu.

Najiuliza hadi leo, ni kitu gani hasa ambacho kinatufanya tudhani kwamba tunaweza kupigana au kuwazuia watu wote wanaotukera wasitukere? 

Ni kwa nini tunashindwa kujiuliza maswali kabla hatujatenda jambo? 

Nilimzuia rafiki yangu asipigane na wale vijana walevi, lakini baadaye akaamua kuingilia ubishi usio na kichwa wala miguu na kununua majeraha na pengine angepoteza maisha yake.

Katika utambuzi tunajifunza kwamba kabla hatujatenda jambo kuna nafasi ya kujiuliza kama tutende au hapana, kuna nafasi ya kujiuliza tutende nini. 

Ukweli ni kwamba sisi siyo tunaoweza kuwapangia watu kama watuchokoze au wasituchokoze.  Mtu anaweza kukusukuma bila sababu, mtu anaweza kukutukana bila sababu, anaweza kukukashifu bila sababu.

Hatuwezi kumzuia asifanye hivyo hata akili ya kawaida tu, inakwambia hivyo. Unachoweza kufanya wewe ni kuvutwa na kuathiriwa na nguvu hasi zake. Hii huwezi kuifanya kama hukujiandaa, na kujiandaa ni kujua kwamba kabla hujajibu jambo baya ulilofanyiwa kuna nafasi ya kujiuliza ili ufanye jambo jema zaidi. 

Mlevi au mtu mwenye akili zake timamu akikwambia kwamba, huna hela, bila kujali kama ni kweli au siyo, unaumia kitu gani? Unaumia kwa sababu unaamini kwamba, huna hela kweli na unaamini kwamba kukosa fedha kunaondoa thamani yako. 

Kwa hiyo unatafsiri vipi kauli au vitendo vya watu wengine, ndicho kinachokufanya uchukue hatua fulani unapochokozwa, siyo uchokozi ulilofanyiwa.  Kumbuka jambo hilo.

Kama yule jamaa yangu angekuwa makini angejiuliza, "huyu kijana kanywa soda yangu na kashfa na ubabe juu, lakini hata kama asingeinywa, si bado ningeinywa na kuimaliza?" Lakini hakutumia nafasi iliyoko katikati ya tendo na uamuzi. 

Kama angeitumia nafasi hiyo kuhusu wale waliompiga chupa angejiuliza, "hawa wanasema asiye na pesa ndiye ambaye hanywi pombe, kama ni kweli inanipunguzia kitu gani?"

Bila shaka angegundua kwamba haimpunguzii chochote na pengine hata wakati wanaongea hawakuwa wanamwona. 

Ni suala la kuitumia vizuri nafasi iliyo katikati ya tukio na majibu yetu kwa tukio hilo. Tukiitumia vizuri siku zote tunakuwa washindi, tukiitumia vibaya siku zote tunakuwa ni watu wa maumivu. 

Kumbukeni tu kwamba katikati ya tukio na maamuzi kuna nafasi. Itumieni kwa hekima na busara. 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Mzee Mtambuzi

A freelance Journalist and also teaching self-empowerment, positive thinking as a means of creating the life you desire including spirituality. He is writing in Mwananchi Scoop every Wednesday Visa na Mikasa.


Latest Post

Latest Tags