Nguo za marinda zilivyorudi kwa kasi mjini

Nguo za marinda zilivyorudi kwa kasi mjini

Leo katika Fashion tutazungumzia nguo za marinda zilivyo kuwa na wafuasi wengi na imeonekana kipindi cha hivi karibuni ndiyo mtindo ambao umeonekana kuvaliwa sana japo ni vazi la msimu yaani linakuja na kuondoka.

Tunapozungumzia nguo ya marinda hatumaanishi sare za shule bali ni sketi, suruali au gauni iliyotengenezwa kwa kuwekewa marinda aidha makubwa au madogo katika kupendezesha nguo kuwa na muonekano wa kisasa unaoenda na wakati.

Aidha nguo za marinda zinakuwa na msimu zinavaliwa kwa kipindi fulani kisha zinapotea baada ya muda tena zinarudi kwenye soko zikiwa na nakshi mbalimbali ikiwepo mikanda na maua katika nguo husika ili mradi tu ziwe na utofauti, watu huzipenda na huwa ni mtindo ambao kwa kipindi hicho unaonekana kama hauja wahi kutokea.

Basi bhana Mwananchi Scoop haikulaza damu moja kwa moja mpaka kwa mwanamitindo na mfanyabiashara Pili Jongo anasema asilimia kubwa ya mitindo ya sasa inarudiwa kutokana na ubunifu kupungua ila kinachobadilika ni aina ya kitambaa na nakshi mbalimbali zinazo onesha utofauti wa awali anasema.

“Nguo za marinda zilivaliwa kipindi cha nyuma na zilikuwa kwa kila rika lakini baada ya muda zilipotea zikaja nguo zikaitwa mwanamke nyonga na watu wakashona nazo zikapotea usijekushangaa mtindo huo ukarudi tena kutokana na watu kurudisha mitindo ya zamani,”

Alielezea kuwa nguo za marinda hazimkatai mtu na hiyo ni sababu ya kuendelea kutumika kutokana na muonekano unaotokana na mtu akivaa hizo nguo za marinda anasema.

“Kwanza mshono wa marinda anavaa mtu yeyote mwenye ‘shepu’ na asiyenayo kutokana na ukaaji wake mwilini iwe sketi,gauni na suruali kila mmoja anapendeza kwa kutazamwa na jicho la mtu katika jicho la urembo na sio la kukosoa vazi hilo,”

Anasema ili marinda yakae vizuri katika nguo haitakiwi kushonewa na kitambaa kizito hivyo inashauriwa kushonwa kwa kutumia vitambaa vyepesi na visiwe vya mpira kwani havikai marinda na ndiyo sababu ya kupelekea vitambaa vya shifoni kutumika zaidi katika matumizi ya nguo za marinda.

Kama ilivyo ada raha ya fashion bhana haina mwenyewe si ndiyo tukajongea mpaka kwa Queen Patrick mfanyabiashara wa nguo Kariakoo anasema amefungua mzigo wa nguo za marinda ambazo hakutarajia kuona mzigo wake unaisha kwa haraka na kuuliziwa na wateja huku baadhi ya wafanyabiashara kutoka Zambia na Malawi wakiwa wananuna kwa wingi.

“Niliagiza mzigo kutoka China na Uturuki nikajaribu kuweka na nguo zenye marinda ikiwepo sketi ndefu na fupi na magauni machache na nilileta kama mfano tu kuona kama zitakuwa na soko lakini kilichotokea imebidi niagize mzigo mwingine ambao tayari nimechukua fedha za watu,”alisema Queen.

Naye, Riziki Mbwana muuza nguo mtaa wa Kongo/Narung’ombe anasema wadada wanatembea na zinazovuma kutokana na mtindo uliyopo kwa kipindi hicho hivyo wakishafahamu ni msimu wa nguo gani na wao wanachukua mzigo wa kipindi hicho.

“Sisi wafanyabiashara wadogo hatukurupuki kununua mizigo ili isituchachie kwa hiyo tunatembea na mdundo wa wanawake kama kwa sasa wameturudisha shule kila anayepita anaulizia sketi za marinda na ki-top cheupe au cheusi nikijichanganya kuweka nguo nyingine nitazipeleka kijijini kwetu,”anasema Riziki.

Melisa mfanyabiashara wa nguo nchi ya Zambia anasema nguo za marinda kwao zinavaliwa kanisani na kwenye sherehe za harusi ambapo inamfanya mtu anaonekane wa heshima zaidi katika maeneo hayo tofauti na zikivaliwa maeneo mengine.

Labda nikwambie kitu ambacho ulikuwa haukijui kuwa katika fashion vyakale navyo ni dhahabu siku hizi kwenye mitindo ni ubunifu tu lakini fashion walizoanza mabibi zetu zinaendelea ila ni ubunifu tu unaopita kutokana na utandawazi.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Asha Charles


Latest Post