Ngono katika umri mdogo chanzo cha saratani ya shingo ya kizazi

Ngono Katika Umri Mdogo Chanzo Cha Saratani Ya Shingo Ya Kizazi

Saratani ya shingo ya kizazi ni saratani inayoongoza kwa kusababisha vifo vya wanawake wengi duniani.

Inakadiriwa kuwa asilimia 85 ya vifo hivi hutokea katika nchi zinazoendelea. Kwa Tanzania, wastani wa wanawake 6,241 huugua saratani hii kila mwaka, ambapo 4,355 kati yao hufa, hii ni kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka 2010.

Ripoti hiyo ilibainisha kuwa saratani ya shingo ya kizazi ndio saratani ya kwanza kwa wanawake nchini Tanzania, na Saratani namba moja kwa wanawake walio kati ya umri wa miaka 15 hadi 44.

Kutokana na takwimu hizo madaktari mbalimbali akiwemo Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Dk. Nanzoke Mvungi wanatujuza kwa undani juu ya saratani hiyo.

Dk. Mvungi anasema saratani ya shingo ya kizazi ni mabadiliko hasi (yasiyo ya kawaida) ya chembechembe hai zilizopo kwenye shingo ya kizazi.

Anasema mara nyingi saratani hiyo ikiwa inaanza haionyeshi dalili yoyote hivyo mgonjwa hawezi kuchukua hatua yoyote kukabiliana na tatizo hilo kwa wakati huo.

Dk.Mvungi anasema ni wazi kuwa saratani hiyo nay a matiti zinakuwa kwa kasi hapa nchini ikilinganishwa na miaka ya nyuma kwani kwa takwimu za sasa  za ORCI zinaonesha kuwa saratani inayoongoza kwa upande wa wanawake ni ya shingo ya kizazi kwa uwepo wa wagonjwa kwa asilimia 33 ikifuatiwa na saratani ya matiti ambayo ni asilimia 12 kwa nchi nzima.

“Kwa takwimu hizi inadhihirisha kuwa tatizo ni kubwa sana hapa nchini hivyo tunapaswa kulivalia njuga kweli kweli, kwani wanawake wote wapo hatari endapo tu wataanza kushiriki ngono isiyosalama katika umri mdogo,” anasema

Chanzo/vihatarishi vya saratani hiyo

Anasema ufanyaji wa ngono na wanaume wengi kwa wasichana wenye umri mdogo ni moja ya vihatarishi vya saratani ya shingo ya kizazi.

“Hapa tunaamini kuwa kwa kupitia ngono isiyosalama itakuwa imebeba wadudu wa virusi vya HPV ambao wanaelezwa kuwa na mchango mkubwa wa mabadiriko wa vimelea vilivyopo kwenye mlango wa kizazi wa mwanamke yoyote hasa akiwa katika umri mdogo wa miaka tisa hadi 15,” anasema

Anasema virusi hiyo vikifanikiwa kuingia katika mlango huo wa kizazi vinaweza kufanya mabadiriko hayo kwa muda wa miaka 10 hadi 20 na ndipo mtu ubainika kupata saratani hiyo ya shingo ya kizazi.

“Wakati ule mimi naanza kazi kama miaka 10 iliyopita saratani hizi za shingo ya kizazi zilikuwa zikionekana kwa wanawake wenye umri wa miaka 60, lakini miaka hii ya karibuni yote tumekuwa tukiwaona wagonjwa hata wakiwa na miaka 28, kwahiyo sasa hivi inawahi zaidi.

“Hivyo kuja haja ya kutoa elimu kwa watoto wa kike kujitunza, kutoanza ngono mapema wakati wakiwa na umri mdogo, hii inatokea sana vijijini kwani kuna watoto wanaolewa wakiwa na umri mdogo na kuanza ngono mapema hivyo kumuweka kwenye hatari ya kupata saratani,” anasema

Dk. Mvungi anasema viashiria vingine vya saratani ya shingo ya kizazi ni uvutaji sigara, unywaji wa pombe kupita kiasi, kutokufanya mazoezi, kuwa na magonjwa ya zinaa pamoja na ulaji wa vyakula vyenye wanga zaidi.

“Ndio maana tunashauri watu kula mlo kamili ili kuweza kujikinga na hatari ya kupata saratani hii ya shingo ya kizazi,” anasema

Naye Daktari Bingwa Mbobezi wa Magonjwa ya Wanawake na Uzazi kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Matilda Ngarina anasema kutokana na watu kukosa uelewa usababisha kupokea wagonjwa ambao wamefikia hatua mbaya ya saratani ya shingo ya kizazi.

“Steji ambayo wagonjwa hao uja tunachoweza kuwasaidia ni kuwapa mionzi au Themotherap, lakini watu wangekuwa na uelewa wa haraka wa kuja kufanya vipimo mapema huu ugonjwa ungepungua na kuisha kabisa kwa sababu ukigundulika mapema unatibika na unapona bila shida,” anasema Ngarina

Itaendelea

Usikose wiki ijayo kujua Dalili za saratani ya shingo ya kizazi

 


Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm


Latest Post