Ndugu asimulia Marco wa Zabron Singers alivyopambania uhai wake

Ndugu asimulia Marco wa Zabron Singers alivyopambania uhai wake

Dar es salaam. Familia ya aliyekuwa mwimbaji wa kundi la Zabron Singers Marco Joseph imesema chanzo cha kifo cha ndugu yao ni tatizo la moyo lilitokea ghafla akiwa nchini Kenya.

Mjomba wa marehemu Emanuel Zabron leo Agosti 22, 2024 ameliambia Mwananchi kuwa tatizo hilo lilitokea ghafla Jumapili Agosti 11,2024, akiwa nchini Kenya alipokwenda kwa ajili ya huduma yake ya uimbaji.

“Tatizo hili lilitokea ghafla sana wakati anaendesha gari na ndipo alipaki na kuita wenzake,” amesimulia.
Tangu agundulike apatwe na ugonjwa huo hadi anafariki dunia jana Agosti 21, 2024, zimepita siku 10 za maumivu kwake huku akipatiwa matibabu katika hospitali kadhaa.

Ameeleza baada ya tatizo hilo hakuweza kuendelea na huduma ilibidi arudi Mwanza na Ijumaa Agosti 16, 2024 alienda kufanyiwa vipimo katika Hospitali ya Bugando ndipo majibu yalionesha ana shimo kubwa kwenye moyo ambalo ndilo lililopelekea mshtuko huo akiwa nchini Kenya.

“Baada ya majibu hayo ilibidi aje siku hiyo ya Ijumaa jioni na kwenda moja kwa moja Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa vipimo zaidi, tulivyofika vipimo vilikuwa changamoto kwa sababu ilikuwa wikiendi ilibidi turudi hospitali siku ya Jumatatu ili kupata huduma.

"Baada ya vipimo kufanyika alipangiwa Jumatano kwa ajili ya upasuaji. Baada ya upasuaji madaktari walituita wakasema mgonjwa anatokwa damu nyingi baada ya kuwekewa kifaa maalumu cha kusaidia katika upumuaji,"amesema ndugu huyo wa marehemu
Hata hivyo, amesema awali marehemu hakuwahi kuwa na tatizo hilo la moyo wala maumivu ya aina yoyote hadi lilipotokea ghafla.

Marco ameacha mke na watoto wanne. Ibada ya kuaga mwili itafanyika leo Agosti 22, 2024 saa 11 jioni Hospitali ya Taifa Muhimbili kisha mwili utasafirishwa kuelekea Kahama kwa ajili ya mazishi ambayo bado tarehe haijatajwa.

Kati ya nyimbo zilizoimbwa na Zabron Singers ni Moyo, Uko Singel?, Naogopa, Mkono wa Bwana, na Sweetie Sweetie






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags