Nay anakabiliwa na mashitaka haya BASATA

Nay anakabiliwa na mashitaka haya BASATA

Msanii wa Bongo Fleva, Emmanuel Elibariki, maarufu kama Nay Wa Mitego, ameshitakiwa na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) kwa makosa manne yanayohusiana na wimbo wake wa ‘Nitasema.’

Nay aliwasili nje ya ofisi za Basata jijini Dar es Salaam mchana wa leo, 27 Septemba 2023, ambapo wakili wake, Jebra Kambole, alizungumza na vyombo vya habari, akisema, Basata imemshtaki kwa makosa manne.

Aidha aliweka wazi kuwa shitaka la kwanza linadai kuwa Nay aliachia wimbo huo bila kibali cha Basata na kwamba amevunja kifungu cha 25 cha kanuni za Basata.

Huku shitaka la pili likihusu madai ya kuwa wimbo wa ‘Nitasema’ unachochea machafuko ikidai kuwa serikali inahusika na utekaji nyara na mauaji.

“Wanasema kuna sehemu za wimbo huo zinazochochea machafuko kwa kudai kuwa Serikali inahusika na utekaji nyara na mauaji," alisema.

Kambole alifafanua kuhusu shitaka la tatu, akibainisha kuwa linahusisha kauli potofu zinazoashiria kuwa Serikali imeanzisha miradi lakini imeshindwa kuitekeleza, jambo ambalo Basata linatafsiri kama ukosoaji wa utendaji wa serikali.

“Walisema kosa la tatu linaonesha kuwa serikali haijatekeleza baadhi ya miradi,” alieleza.
Hata hivyo, shitaka la nne linamtuhumu Nay kukashifu mataifa mengine kwa kutaja nchi za Rwanda na Congo katika mistari ya wimbo wake.
“Kuna mistari kwenye wimbo inayotaja Rwanda na Congo. Wanadai kwamba amekashifu mataifa mengine, jambo ambalo linaweza kusababisha migogoro na nchi hizo," aliongeza.

Kwa kuzingatia madai haya, Basata imempa Nay muda wa siku saba, hadi Oktoba 4, kutoa maelezo ya kina kuhusu kila shitaka.
Licha ya utata unaoendelea, Nay amesimama imara katika ahadi yake kwa mashabiki wake na masuala anayoyazungumzia kupitia muziki wake.

“Sina kitu cha kuwalipa mashabiki wangu isipokuwa kuwasemea. Tunachofanya ni haki, na haki huinui taifa lazima niendelee kufanya hivyo," alisisitiza.

Awali, Nay alitoa taarifa kupitia ukurasa wake wa Instagram kuhusu wito huo ingawa Katibu Mtendaji wa Basata, Kedmon Mapana, alikanusha kuwepo kwa wito huo.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags