Namna Ya Kutengeneza Juice Ya Tikiti Na Passion
Wataalamu wa afya wanasema tunda la Tikiti Maji ni chanzo kikuu cha protini, mafuta, nyuzinyuzi, wanga, calcium, phosphorus, chuma, vitamin A, B6, C, Potasium na virutubisho vingine vingi.
Huku baadhi ya wataalamu wa lishe wakieleza faida nyingi zaidi za tunda hilo ambalo husaidia kuimarisha misuli na mfumo wa fahamu na kuusaidia ufanye kazi zake vizuri, pia tunda hilo lina uwezo wa kukuondoa katika hatari ya kupata shinikizo la damu na faida nyingine.
Mbali na kuwa na faida hizo kedekede lakini pia baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakilitumia tunda hilo kama sehemu ya kujipatia kipato katika kutengeneza juisi ambayo inachanganywa na Limao au Passion kwa ajili ya kuleta ladha zaidi.
Kwa kuwa mwaka umeanza na wapo baadhi ya watu wanajiuliza cha kufanya ili waweze kujiingizia kipato basi Jarida la Mwananchi Scoop tumekusogezea fursa hii ambayo inaweza kukupatia maokoto, ungana nasi mwanzo mpaka mwisho kujifunza namna ya kutengeneza juisi ya Tikiti Maji.
Mahitaji
* Tikiti Maji 1 kubwa
* Limao moja au mawili
* Passion 5-10
* Sukari robo
* Tangawizi moja
* Hiriki ya unga nusu kijiko cha chai
NB: Ili juisi yako iweze na ladha ambayo itawavutia watu wengi utachagua kiungo kimoja cha kuweka hapa namaanisha Limao na Passion kwani hautakiwi kuviweka vyote kwa wakati mmoja kutokana na vyote kuwa na ladha sawa ya uchachu.
Namna ya kuitengeneza juisi yako…;
➢ Utachukua tikiti lako utaliosha vizuri kisha utaandaa chombo kikubwa, likate vipande vidogo vidogo vitakavyoweza kusagika vizuri kwenye brenda.
➢ Baada ya kukata matunda yako utachanganya, passion na tangawizi, kisha utaiweka kwenye brenda lako na uanze kuibrendi.
➢ Ukishamaliza kuibrend yote utachukua chujio utachuja baada ya hapo utaweka sukari, hiriki na kama haukutumia Passion kwenye kusaga basi utakamua limao lako na maji yako uweke kwenye juisi yako.
➢ Na mpaka kufikia hapo juisi yako itakuwa tayari hivyo basi utaiweka katika friji na baada ya hapo itakuwa tayari kwa ajili ya kuuza. Na mara nyingi glasi moja ya juisi hii huanzia 1,000 hadi 2,000, unaanchaje okoto kama hili likupite na mwaka mpya huu? Changamkia fursa weweee..!
Leave a Reply