Namna ya kukabiliana na mahusiano yasiyotabirika

Namna ya kukabiliana na mahusiano yasiyotabirika

Ukiwa katika mahusiano na mwenza asiyetabirika yanakuwa ni mapenzi yenye maji kupwa maji kujaa yaani kuna muda mnakuwa na furaha na amani lakini ghafla hali inabadilika na kuwa tafrani na kugombana na sababu ikiwa haina kichwa wala miguu.

Kuna kitu wenzetu wazungu wanaita ‘emotional rollercoaster’. Hii ina maana kwamba mnakuwa na mahusiano yasiyotabirika yenye hali kugombana na kutokuelewana na hali ya kuelewana na kuwa na bashasha na mapenzi motomoto kama vile hakuna kilichotokea na hali zote mbili zinaweza kutokea kwa muda mfupi.

Inakuwa ni vigumu kwako kutabiri nini kitatokea muda mfupi ujao kila mnapokuwa Pamoja au nini kitatokea kati ya siku moja au nyingine. Mahusiano kama haya huelezewa na baadhi ya watu kama ni mahusiano yenye vioja na pengine wengine wakayaona kama ni mapenzi yenye upendo, huba na bashasha.

Inayoelezewa na wataalamu wa saikolojia kuhusu mahusiano haya yasiyotabirika  kwamba inawezekana mmoja kati ya wapenzi walioko kwenye mahusiano haya anakuwa hana subira na hawezi kudhibiti mihemko yake. Anakuwa ni mwepesi kukasirika tena kulikopitiliza na anaweza kuanzisha malumbano yasiyo na maana na kuleta kisirani pasipo sababu.

Hakuna sababu moja au mbili zinazoweza kutajwa kama chanzo kinachosababisha watu kuwa na tabia za aina hii katika mahusiano lakini mojawapo ya sababu inayoweza kuchangia mtu kuwa na tabia za aina hii ni kutokana na malezi, hasa kile alichojifunza kupitia kwa wazazi, walezi au watu wake wa karibu kuhusu namna ya kuhusiana na watu hata pale wanapotofautiana.

Inawezekana mtu wenye tabia hizi pia hakuwa na mahusiano mazuri na wazazi au walezi wake utotoni kiasi cha kumuweka katika hali ya tahadhari wakati wote kutokana na kuteswa, kunyayaswa au kubaguliwa waziwazi kiasi cha kuathiri mtazamo wake kuhusu mahusiano na watu wengine anapofikia ukubwani.

Unapokuwa na mahusiano na mtu mwenye tatizo hili la kuhemkwa mara kwa mara na kuwa ni mtu asiyetabirika katika mahusiano inahitaji nguvu nyingi sana kihisia katika kukabiliana na hali hiyo ili kuweza kudumisha mahusiano yenu

Kukabiliana na mtu mwenye hisia chungu mara kwa mara ni kazi kubwa na inayochosha kwa sababu muda huu mko kwenye hali ya furaha na amani na ghafla hali inabadiliaka na kuingia kisirani kisichojulikana kimetokea wapi na pengine hata sababu ikawa haijulikani

Moja ya tatizo kubwa kwa watu wenye mahusiano yasiyotabirika ni kwamba kuna wakati wanaweza kuwa na ukorofi na kisirani cha ajabu kiasi cha kusababisha mwenzi wake kukosa amani na furaha. Lakini wanapobadilika tena baada ya muda mfupi wanakuwa ni watu tofauti sana mpaka mwenzi wake anaweza kushangaa. Watu hawa huwa na furaha, upendo, kufanya mizaha yenye kuchekesha na kumfanyia mwenzi wake mahaba kiasi cha kumfanya asahau kile kilichotokea muda mfupi uliopita.

Mtu mwenye tatizo hili anawezaje kupona?

Mtu mwenye tatizo hili anatakiwa ajijue kwamba anayo shida hiyo na aombe msaada kwa wataalamu wa saikolojia. Lakini hata ile kujua kwamba analo tatizo inaweza ikawa ndiyo nusu ya tiba kabla ya tiba kamili. Halafu baada ya hapo ndipo achukue hatua ya kutafuta mtaalamu wa saikolojia atakayemsaidia kuachana na tabia hiyo inayoweza kumsabishia mahusiano yake kuvunjiaka mara kwa mara.

 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Shaban Kaluse

A Sales and Marketing in the hospitality Industry and also a freelance journalist, writing about love and relationships and educative articles which aims for youths, every Tuesday on Mwananchi Scoop.


Latest Post

Latest Tags