Namba tano ilivyobeba maisha ya msanii Abigail Chams

Namba tano ilivyobeba maisha ya msanii Abigail Chams

Week hii tupo na binti mwenye sauti tamu na uwezo mkubwa wa kucheza na ala za muziki si mwingine bali ni Abigail Chams tumezungumza naye mengi na kaeleza yote ambayo ulikuwa ukitamani kuyafahamu kumuhusu, twende pamoja mwanzo mwisho.

Wiki chache zilizopita rangi ya buluu na namba tano viliwashangaza wengi kwenye kurasa za mitandao ya kijamii ya mwanamuziki Abigail Chams (Abby Chams) huku kukiwa na maswali ya hapa na pale kutoka kwa wadau wa muziki wakitaka kufahamu kuna nini ambacho msanii huyo anataka kukifanya.

Wakati mashabiki wakiendelea kujiuliza maswali juu ya kubadilika kwa kurasa za msanii huyo, naye hakuka  kinyonge akadodosha EP yake iitwayo 5 ikiwa na ngoma sita, kudondoshwa kwa EP hiyo wala hakukumaliza maswali kwa mashabiki wa muziki kwani wengi walibaki wakijadili jina la EP hiyo kupewa jina la namba tano.

Katika mahojiano aliyofanya Abigail Chams na Mwananchi Scoop amejibu maswali yote huku amefichua siri kubwa iliyopo kati yake na  namba tano.

Kama ilivyo kawaida kwa baadhi ya watu kuamini katika namba za bahati ndivyo pia ilivyo kwa msanii huyu ambaye ameeleza kuwa 5 imekuwa namba yake ya bahati kila wakati, na imekuwa ikimaanisha kila kitu katika maisha yake, kama vile Mungu, familia yake, shauku yake kwenye muziki na hata ubora wake.

”Namba tano inanikumbusha juu ya upendo na neema ya Mungu isiyo na mwisho juu ya maisha yangu kwamba yeye yuko pamoja nami kila wakati.

 

Nilizaliwa mwezi wa tano, na ninatoka katika familia iliyounganishwa na watu watano mama , baba, dada, kaka yangu na mimi mwenyewe kwa hiyo namba tano inawakilisha watu hawa ambao ni ulimwengu wangu.” Anasema Abigail

Kama inavyofahamika msanii huyu wengi walianza kumtambua kutokana na kipaji chake kikubwa cha kupiga vyombo mbalimbali vya muziki, ameeleza kuwa navyo vina uhusiano mkubwa na namba hiyo ambayo ni ya bahati kwake.

“Nilijifunza kupiga ala ya muziki ya kwanza nilipokuwa na umri wa miaka mitano, muziki tangu wakati huo umekuwa maisha yangu kwa hiyo namba hii inawakilisha safari yangu ya muziki, na hadi sasa ninauwezo wa kupiga ala tano za muziki.

Kwangu mimi, namba tano inawakilisha ubora wa kila kitu ninachofanya kama ilivyo kwa EP yangu na kila ninachofanya nataka kiwe na ubora kama nyota yangu ya namba 5.” Anasema Abigail

Maelezo ya msanii huyo juu ya namba tano yamesadikika mara baada ya EP yake kutoka kwani ilifanikiwa kuwa albamu namba moja Tanzania na namba tatu Afrika nzima, huku maandalizi ya EP hiyo yakiwa yamechukua miezi sita hadi kukamilika.

Mashabiki wa muziki mara nyingi wamejikuta wakikosa burudani wanazotaka kutoka kwa wasanii wanao wapenda, kutodumu kwenye gemu ya muziki.

Kupitia Magazine hii Abigail amefunguka na kueleza kuwa  kitu pekee kitachofanya aendelee kubaki kwenye muziki ni kuwa na mipango, kutoa muziki mzuri, huku akihakikisha kuwa team yake ipo vizuri katika usimamizi hivyo mashabiki wataendelea kumuona kwa miaka mingi.

Mtazamo wa Abigail juu ya soko la muziki wa Bongo kwa miaka mitano ijayo

“Muziki wa Afrika na wasanii wamekuwa wakitazamwa zaidi kwa sasa, Tanzania tukichukua nafasi hiyo ambayo sasa dunia inautazama muziki wa Afrika tunaweza kusukuma zaidi muziki wa Bongo Fleva na tukafika mbali zaidi kwa miaka mitano na tutachukua tuzo nyingi za Grammy kama tutachukua hatua sasa ” Anasema Abigail

Mitandao ya kijamii ni kati ya vitu vinavyofanya muziki ukue kwa kasi Abigail  anasema kuwa mitandao ni fursa nzuri kwa wasanii na vijana ili wafanikiwe.

“Kuna wasanii wengi nyuma walikuwa wanakwama kusukuma muziki wao lakini mitandao ya kijamii inawafikia wengi na ndiyo maana kuna watu hawafahamiki lakini wakituma nyimbo zao TikTok zinapendwa na wanafanikiwa, nafikiri tusitumie mitandao kucheza tu tunaweza kutumia kwa njia ya kuzalisha pia” Anasema Abigail

Hata hivyo kumekuwa na baadhi ya wasanii kufanya vitu ambavyo si sawa kwa jamii ili waweze kuuza muziki wao, lakini kwa nyota huyo wa muziki imekuwa tofauti kwani anasema kuwa muziki mzuri unajiuza wenye bila ya kufanya vitu ambavyo vinakwaza wengine.

Mbali na hayo mitazamo ya baadhi ya watu pia imekuwa ikiwatazama wasanii kama watu wasiomjua Mungu na wasiofika katika nyumba za ibada hasa kutokana na maisha yao ambayo yamekuwa yakionekana kwenye mitandao ya kijamii bila kujua upande wa wasanii hao. Lakini kwa Abigail anaeleza kuwa katika vitu anavyo ogopa kwenye maisha yake ni kuacha kusali

‘’kitu naogopa kwenye maisha yangu ni kuacha kusali , kwa sababu Mungu ndiye sababu ya mimi kuwepo hapa leo, kwa hiyo siwezi kuacha kusali naogopa sana”. Anasema Abigail.
.
.
.
#MwananchiScoop
#BurudikaNasi






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Asha Charles


Latest Post

Latest Tags