Mwongozo madaraja ya muziki Tanzania

Mwongozo madaraja ya muziki Tanzania

Kanuni na miongozo ni jambo muhimu kwenye sekta yoyote kwa lengo la kuepusha upotoshaji na uvunjwaji wa kanuni na sheria iliyowekwa.

Nchini Tanzania kumekuwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wadau wa muziki kuhusiana na uvunjwaji wa maadili kutokana na kazi za sanaa ambazo zimekuwa zikitolewa na wasanii mbalimbali.

Ili kuepuka uvunjwaji wa maadili katika kazi za sanaa, Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) limeweka madaraja ya kazi hizo ambayo kila msanii na jamii inapaswa kufahamu.

Madaraja ya kazi za sanaa

“WW” sawa na “U”, muziki wa daraja hili unafaa kusikilizwa na hadhira  ya watu wa umri wowote.

“WM13 sawa na U13”, muziki wa daraja hili unapaswa kusikilizwa na watoto  kuanzia umri wa miaka 13 na kuendelea.

“WM16” sawa na “U16” muziki wa daraja hili unapaswa kusikilizwa na watoto kuanzia miaka 16 na kuendelea.

“WZ18” sawa na “A”, huu unapaswa kusikilizwa na  umri kuanzia miaka 18 na kuendelea.

“MM” sawa na “SS” daraja hili ni la maonesho maalumu. Kama vile maonesho ya elimu na mafunzo.

Daraja X, hili hairurusiwi kuoneshwa mahali popote nchini, endapo itafanyika hivyo muhusika atakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Aidha ikumbukwe kuwa hivi karibuni wadau mbalimbali wa muziki Bongo walitafsiri baadhi ya maneno katika wimbo wa mwanamuziki Lavalava uitwao ‘Kibango’ kuwa hauna maadili.

Mfano wa maneno yanayosikika  kwenye wimbo huo ni “Nasikia nyeee nyepesi hii pombe, Nchanganyie Bapa.”

Kutokana na taharuki kuhusu wimbo huo, kupitia tovuti rasmi ya Basata walichapisha taarifa ya kuutolea ufafanuzi kwa kuupa daraja WZ18 sawa na daraja A yaani kusikilizwa na watu wenye umri wa miaka 18.

“Baraza la sanaa la Taifa (Basata) limepitia na kuhakiki mashairi ya wimbo uitwao “KIBANGO” na kuupa daraja WZ18 sawa na daraja A yaani kusikilizwa na watu wenye umri kuanzia miaka 18 na kuendelea na kusikilizwa sehemu maalumu ambako watu chini ya umri huo hawatokuwepo,” imeeleza taarifa hiyo.

Hata hivyo katika uhakiki wa mashairi ya wimbo huo taarifa imeeleza kuwa ngoma hiyo haina shida yoyote kwani imezingatia vitu vyote kuanzia upangiliaji wa vina pamoja na matumizi ya lugha.

“Wimbo ni mzuri kuanzia kwenye upangaji wa vina na mizani, utumiaji wa lugha ya picha na tafsida kama maneno “Hii party ina vijiti”. Ujumbe wa wimbo huu umelenga zaidi watu wanaotumia vilevi mbalimbali na hii imejidhihirisha katika mashairi kama “Naskia nyeee nyepesi hii pombe Nchanganyie Bapa”, lakini pia ujumbe mwingine unahusu mapenzi,” ilieleza taarifa hiyo kwa kina.
.
.
.
#MwananchiScoop
#BurudikaNasi


Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Asha Charles


Latest Post