Mwanamke Unatoka Mtoko wa Kwanza Halafu Unakutana na karaha hizi….!

Mwanamke Unatoka Mtoko wa Kwanza Halafu Unakutana na karaha hizi….!

Mtoko wa kwanza huwa unawaweka wanawake katika wakati mgumu ukilinganisha na wanaume.

Wakati wanaume kwao sio tatizo kubwa la kuwaumiza vichwa, kwa wanawake huwa wanajiuliza maswali mengi sana kuhusiana na huyo mtu anayekwenda kuonana naye.

Hebu tuchulie mwanamke ametoka na mwanaume kwa mara ya kwanza kwa ajili ya kufahamiana na kuangalia kama anaweza kuwa na muafaka na mwanaume huyo kwa matarajio ya kujenga familia bora.

Lakini kinyume chake anakutana na karaha hizi zifuatazo. Je kama ni wewe mwanamke unakabiliana na hali hii utafanyaje?

  1. Unagundua kwamba mwanaume uliyetoka naye ana mke au ana mpenzi wake.

Baada ya kufika kwenye mgahawa kwa ajili ya kupata mlo wa usiku pamoja, katikati ya maongezi yenu mwanaume huyu anakushika mkono kama ishara ya upendo wakati mkiwa mmekaa mezani.

Unapochunguza vidole vyake unagundua kwamba ana alama ya pete ya ndoa, unapomdadisi anakanusha, lakini baada ya kumbana sana anakiri kwamba anaye mke lakini ndoa yake ina vurugu na inalegalega kiasi kwamba siku yoyote itavunjika.

Au wakati wa maongezi yenu anakiri kwamba anaye mchumba wake, lakini hadhani kama atamfaa ingawa bado wako pamoja. Je utafanya nini?

 

  1. Anakunywa kupindukia mpaka anashindwa kumudu mazungumzo…

Baada ya kupata mlo mnahamia kwenye baa ili kupata vinywaji kidogo kabla ya kuachana, mkiwa hapo baa, mwanaume huyo anakunywa pombe kupita kiasi mpaka anaashindwa kumudu mazungumzo na kuongea pumba tupu.

  1. Anatumia muda wake mwingi kumzungumzia mpenzi wake waliyeachana..

Inawezekana katika mazungumzo yenu unamuuliza sababu ya kuachana na mpenzi wake wa zamani.. mwanaume huyo anatumia muda mwingi kumzungumzia mpenzi wake huyo na anaonyesha dalili za dhahiri kwamba ana m-miss

  1. Baada ya kupata mlo, tumbo lako linaleta kisirani

Labda chakula ambacho umekula hapo mgahawani hakikupatana na tumbo lako, ghafla unapatwa na tumbo la kuhara kiasi cha kujikuta ukipiga trip kadhaa kwenda maliwatoni, mpaka mwanaume huyo anakuuliza kama una tatizo. Je ungejibu nini?

  1. Marafiki zake wanajiunga nanyi..

Wakati mnapata chakula na kuongea kwa bashasha, mwanaume huyo anapigiwa simu na marafiki zake ambapo anawaelekeza mlipo. Ghafla marafiki hao wanakuja na kujiunga nanyi kwa ajili ya kupata mlo mkiwa pamoja. Je ungefanyaje?

  1. Anakuwa na shauku kubwa na mwili wako.

Wakati mkiendelea kupata vinywaji baada a kumaliza kula, mwanaume huyo anaanza kukushika shika mwili wako mara kwa mara hususan sehemu zako za faragha huku akikupiga mabusu motomoto kiasi cha kukukera. Je utafanya nini?

 

  1. Unagundua kwamba siye uliyemtegemea..

Mlipokutana kwa mara ya kwanza ulimuona alikuwa ni mwanaume mzuri wa sura na umbo, mpole kiasi, mcheshi, mwenye utani mwingi na mwenye uelewa mpana.

Na hizo sifa ndizo zilizokuvutia kwa jicho la kwanza na ndio ikawa ni sababu kwako kukubali kutoka naye ili mpate kufahamiana zaidi.

Lakini mkiwa hapo kwenye mghahawa unagundua kitu tofauti. Wakati wa mazungumzo yenu unagundua kwamba si lolole wala chochote.

Jamaa ni mweupe hajui kujieleza ana ubishi usio na maana na anayependa kujikweza tofauti na hali aliyo nayo. Lakini pia unagundua kwamba ni mwongo na asiyepima uzito wa kauli zake. Kwa kifupi ni mropokaji…. Je ungefanyaje?

  1. Mpenzi wako wa zamani mliyeachana kwa kisirani ni mjomba wake…!

Wakati wa mazungmzo yenu hapo mghahawani unagundua kwamba ni mwanaume mwenye muafaka na anayefaa kuitwa mume.

Ni mtu ambaye mnaendana kwa kila kitu, ni msikivu na mwenye subira na asiye na papara.

Lakini katika mazungumzo yenu kuhusu familia zenu unagundua kuwa mpenzi wako wa zamani ambaye mliachana miaka kadhaa iliyopita kwa vurugu kubwa na kuwekeana visasi ni mjomba wake. Huyo mjomba wake anaishi mkoa mwingine na ulikutana naye wakati ulipokuwa ukifanya kazi katika mkoa huo kabla ya kuacha na kuhamia mkoa mwingine. Je utafanya nini?

 

  1. Kila kitu kinaenda kinyume na matarajio yenu…

Kuna wakati huwa tunakutana na visirani mpaka tunajiuliza tulikanyaga mdudu gani siku hiyo… Inaweza kutokea mpenzi wako kafanya booking ya meza kwenye mghahawa kwa ajili ya dinner, lakini mnapofika mnaambiwa meza yenu wamepewa watu wengine, mnaona kuliko kulalamika itakuwa ni kupoteza muda bure kwa kuwa maji yameshamwagika.

Mnaamua kwenda katika mghahawa mwingine, lakini kwa mshangao mnakuta napo pamejaa, manaanza kuingia mghahawa mmoja baada ya mwingine lakini kote mnakuta kumejaa.

Je mtaahirisha au mtaamua kwenda nyumbani kwa mmoja kati yenu kwa ajili ya kuendelea na mtoko wenu?

  1. Unagundua kwamba pamoja na kuwa na mwili mkubwa kumbe jamaa ni mdogo sana kiumri ukilinganisha na umri wako…

Kuna watu wamejaaliwa kuwa na miili mikubwa, ukilinganisha na umri wao. Hiyo iko kote kote, si kwa wanawake wala wanaume. Kwa mfano inatokea mwanaume uliyetoka naye wakati wa mazungumzo yenu unakuja kung’amua kwamba umri wake ni mdogo sana tofauti na muonekano wa mwili wako. Mwanaume huyu anazo sifa muafaka za kuweza kuitwa mume, lakini umri umemzidi sana kiasi cha miaka mitano. Je utaendelea kuwa na uhusiano naye au utajitoa mapema…?.”






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Shaban Kaluse

A Sales and Marketing in the hospitality Industry and also a freelance journalist, writing about love and relationships and educative articles which aims for youths, every Tuesday on Mwananchi Scoop.


Latest Post

Latest Tags