Mwaka mmoja tangu Mohbad afariki dunia

Mwaka mmoja tangu Mohbad afariki dunia

Tarehe kama ya leo mashabiki wa aliyekuwa mwanamuziki nchini Nigeria Ilerioluwa Aloba, 'MohBad', waligubikwa na huzuni baada ya kupokea taarifa ya kifo cha msanii huyu kilichotokea katika mazingira ya kutatanisha huku baadhi ya wasanii wakituhumiwa kuhusika.
Kutokana na utata wa kifo cha mwanamuziki huyu nchini Nigeria kulitokea matukio mfululizo yaliyokuwa kwa lengo la kutafuta haki ya MohBad.

Maandamano
Kuanzia Septemba 13, mashabiki na watu mbalimbali walifanya maandamano wakidai haki itendeke kuhusu kifo cha msanii huyo kwani hawakuamini ripoti ya kifo cha msanii huyo.

Baada ya maandamano kushamiri nchini Nigeria polisi walichukuwa jukumu la kufukua mwili wa msanii huyo kwa ajili ya kukamilisha uchunguzi huo ambao ulianza Oktoba 13 mwaka jana katika Mahakama ya Mwanzo ya Ikorodu.

Naira Marley na Sama Larry kukamatwa

Kufuatia na uchunguzi wa kifo cha MohBad, rapa Naira Marley na promota wake Sam Larry waliamriwa kukaa rumande kwa simu 21 kwa lengo la kutoa ushirikiano katika uchunguzi wa kifo cha MohBad.

Wawili hao walikamatwa na polisi mara tu baada ya kufika nchini Nigeria kutokana na kuhusishwa na kifo cha mwanamuziki huyo, hivyo polisi waliwaweka rumande kwa sababu ya mahojiano zaidi na usalama wao.

Aidha wawili hao waliachiwa huru Novemba 2023, baada ya kutimiza masharti ya dhamana ya Naira milioni 20 ambayo ni zaidi ya Sh 59 milioni pamoja na kutokukutwa na hatia.

Mke kukataa kupima DNA

Wakati kesi hiyo ikiendelea kulindima mahakamani baba mzazi wa Mohbad alimtaka aliyekuwa mke wa marehemu Mohbad, Wunmi kupima DNA ya mtoto huyo kutokana na kutokuwa na imani kuwa mjukuu wake.
Hata hivyo mwanadada huyo aligoma kupima DNA huku akidai kuwa hakuwahi kuwa na mwanaume mwingine alipokuwa na marehemu mume wake.

Taarifa ya uchunguzi kutoka kwa daktari
Mbali na hayo mpaka kufikia sasa bado sababu ya kifo cha mwanamuziki huyo hakijatambulika utakumbuka kuwa mwezi Mei mwaka huu Daktari Bingwa wa Uchunguzi wa Kisayansi na Patholojia kutoka Hospitali ya Taaluma ya Chuo Kikuu cha Jimbo la Lagos (LASUTH), Prof. Shokunle Shoyemi alieleza kuwa chanzo cha kifo cha msanii huyo hakiwezi kutambulika kutokana na mwili wake kupelekwa hospitali ya uchunguzi ukiwa umeharibika.

Mohbad alifariki Septemba 12 mwaka jana akiwa na miaka 27 mpaka kufikia sasa ni mwaka mmoja mahakama bado haijatoa ripoti kamili ya sababu ya kifo hicho wala mwili wa msanii huyo ambao ulifukuliwa kwa ajili ya uchunguzi.

Ilerioluwa Oladimeji Aloba ‘MohBad’ alitamba na ngoma kama ‘Peace’, ‘Feel Good’, ‘Egwu’, ‘Ask About Me’ na nyingine kibao.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post