Muziki na maajabu yake kwenye maisha ya binadamu

Muziki na maajabu yake kwenye maisha ya binadamu

Umewahi kujiuliza kwanini unasikiliza muziki? Au muziki una faida gani kwenye maisha yako? Kama hukuwahi fahamu kuwa muziki unavingi vya kuvutia na umuhimu kwenye maisha yako

Kwanza maana halisi ya muziki ni sanaa ya sauti iliyopangwa katika mtiririko unaovutia, ambayo mara nyingi hujumuisha vipengele kama vile melodi (sauti zinazosikika kuwa kama wimbo), rhythm (mtiririko wa sauti zenye msingi), na hata sauti za zana mbalimbali.

Kwa kawaida, muziki hutumiwa kueleza hisia, kutoa ujumbe, au kutoa burudani. Ni njia ya kipekee ya mawasiliano na uhusiano wa kihisia kati ya wasikilizaji na wasanii.
Muziki unaweza kuwa na athari na faida kubwa kisaikolojia na kimwili kwa wale wanaousikiliza licha ya kuwa hutofautiana kulingana na tamaduni, mitindo, na maeneo ya asili ya utamaduni huo.

Vitu vya kuvutia kuhusu Muziki

Kuzingatia kazi

Muziki unaweza kukusaidia kuzingatia na kuongeza juhudi katika ufanyaji wa kazi, kupitia muziki unaweza kukusaidia kufanya kazi kwa juhudi zaidi tena wakati mwingine bila hata kugundua.
Hili linajidhihilisha kwa baadhi ya watu wanaopenda kufanya mazoezi ya mwili hupata aina ya muziki ambayo huwapa motisha zaidi na kuwafanya wasihisi uchovu na maumivu ya mazoezi.
Aidha katika hili yapo baadhi ya makabila yenye tamaduni ya kufanya kazi kama vile kulima kwa umoja huku wakisindikiza kwa nyimbo mbalimbali

Husaidia afya ya moyo

Watafiti wamebaini kuwa kusikiliza muziki wa aina yoyote unaweza kuleta faida nzuri kwa afya yako ya moyo. Hukuwezesha kupumua vizuri kwa uwiano na mapigo ya moyo wako.

Kwa mfano, wakati unatembea huku ukisikiliza muziki, ni rahisi kugundua kuwa mwendo wako na mdundo vinalingana. Hii ndiyo sababu wanambio hupenda kusikiliza muziki ili kuelekeza moja kwa moja kwenye mapigo yao ya moyo na kuyaweka salama.

Hata hivyo akizungumzia umuhimu wa muziki kwa afya ya moyo Mkuu wa Kitengo cha Utafiti na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo JKCI, Dk Pedro Pallangyo alisema muziki ni tiba kwa wagonjwa hao na tayari njia hiyo inatumika kwa baadhi ya mataifa.

“Kwenye upande wa tiba huku kwetu bado hatujafanyia utafiti lakini kwa wenzetu ni kitu ambacho kimethibitishwa kwa utafiti kwamba kwenye upande wa moyo na maumivu hasa kwa wale wagonjwa kama wa saratani, na kwa ambao moyo umefeli muziki umeonekana kuwa unawasaidia kuondoa maumivu kwa kiasi kikubwa.

“Pia wagonjwa hao wa moyo inawasaidia kuacha kuzingatia dalili ambazo zinawatesa na matokeo yake muziki huwapa amani na kuwapunguzia mateso. Katika mataifa mengine mahospitali zao yamewekewa spika ambazo muziki upo hata Afrika Kusini wodi zote zina spika ambazo miziki imechaguliwa inapigwa na unakuta wagonjwa wanaendelea vizuri wanapokuwa katika mazingira hayo tofauti na wakiachwa,” alisema.

Mbali na hayo alisema mgonjwa wanapokuwa wamelazwa wanakuwa katika hatari ya kupata matatizo ya kisaikolojia hivyo anapokuwa anawekewa muziki inamsaidia afya yake ya akili.

Akimalizia kutolea ufafanuzi suala hilo alisema muziki ambao mgonjwa anaupendelea huwa na msaada lakini kuna aina ya muziki ambao umethibitishwa kwa ajili ya wagonjwa wenye kufariji moyo.

Muziki hubadilisha mitazamo

Hii ni moja ya ukweli wa kuvutia wa kisaikolojia kuhusu muziki, kuhusiana na jinsi unavyoona ulimwengu unaokuzunguka. Nyimbo zenye maneno ya faraja humfanya mtu awe na furaha na wakati mwingine hubadili mtazamo wa ugumu wa maisha kuwa faraja.

Muziki hutunza kumbukumbu

Jarida la utafiti lililochapishwa katika mafunzo ya Kisaikolojia ya Urekebishaji (Neuropsychological Rehabilitation) linataja athari ya muziki. Inaweza kusaidia wagonjwa wenye majeraha ya ubongo (Waliopoteza kumbukumbu) kukumbuka kumbukumbu fulani ambazo ni ngumu kurejesha kwa njia ya kawaida.

Kuimba hupunguza mawazo

Kuimba muziki kunaweza kupunguza msongo wa mawazo pindi unapoimba au kusikiliza muziki uupendao.

Muziki ni lugha ya kitaifa

Profesa Graham Welch, Mwenyekiti wa Elimu ya Muziki, Taasisi ya Elimu ya Chuo Kikuu cha London, alielezea kwamba kuimba na kusikiliza muziki kuna athari za kisaikolojia za kushangaza.

Unafanyika kama njia ambapo watu wanaweza kuunganika, hivyo ni lugha ya kitaifa inayoweza kuongeza na hisia za jamii.

Na katika hilo mifano halisi huonekana hata kwa watu wetu wa karibu kuwaona wakiimba nyimbo za lugha fulani licha ya kuwa hawalewi maana yako.
Wanayosema wapenzi wa muziki

Shabiki wa wa muziki Warda John, mkazi wa Dsm alisema kawaida anasikiliza muziki kwa ajili ya kurudisha kumbukumbu

“Nasikiliza muziki kama burudani, pia kwa ajili ya kurudisha kumbukumbu za matukio muhimu, mara nyingi sana nasikiliza ili nizingatie kufanya kazi vizuri mfano huwa nikisikiliza Bolingo nafanya kazi sana,” alisema

Naye Derick Mchemvu mkazi wa Kigogo alisema hutumia muda wake kusikilia muziki kwa ajili ya kupata nguvu, mzuka na kutuliza hisia.

“Napenda kusikiliza muziki kama njia ya kupata nguvu hasa asubuhi na kupata mzuka wa kuianza siku lakini pia nikiwa kwenye maumivu ya kihisia huwa napenda sana kusikiliza muziki kama njia ya kujiponya,”alisema.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Asha Charles


Latest Post

Latest Tags