MUUZAJI SI ANAJULIKANA!

MUUZAJI SI ANAJULIKANA!

Ilikuwa ni mwaka 1988 nikiwa nimekuja Dar kwa kaka yangu baada ya kumaliza kidato cha nne na kufeli vibaya huko kijijini. Tulikuwa tukiishi kariakoo mtaa wa Sukuma.

Kaka yangu alikuwa amepanga chumba kimoja na alikuwa ni muajiriwa serikalini katika ule mpango wa Direct employment baada ya kumaliza kidato cha sita mwaka mmoja uliopita. Nilikuja ili kaka yangu anisaidie kupata kibarua huku mjini.

Alikuwa bado hajaoa, ingawa alikuwa na rafiki yake wa kike. Kuna wakati huyu rafiki yake alikuwa anakuja kisha wanananiliu, halafu anaondoka, Mara nyingi ilikua ni usiku ambapo ilikuwa ikimlazimu kaka kunipa hela ili niende sinema za usiku pale Odeon au Avalon.

Hizi sinema za usiku zilikuwa zikianza saa sita usiku na kuisha asubuhi. Siku moja kama ilivyokuwa kawaida ya kaka, alikuja huyo mpenzi wake, akanipa hela ili niende hizo sinema za usiku ili wapate muda wa kujivinjari kama ilivyo kawaida yao. Alikuwa anajua kuwa mimi ni mpenzi wa sinema kwa kuwa huko kijijini kulikuwa hakuna hayo mambo ya sinema.

Nilipofika pale Odion nikawakuta wasichana fulani na kwa jinsi walivyokuwa wamevaa nikajua ni wale wasichana wanaojiuza usiku maeneo ya Magoti, Nikiwa bado nina tongotongo za ushamba wa kijijini nikajitutumua na kumfuata mmoja na kumuomba niwe naye kwa usiku ule.

‘Kwa nini unanitongoza kama vile nimekuwa Malaya?’ Aliniuliza baada nya kumwambia shida yangu. Kwa akili yangu ya kijijini nilijua ni Malaya anayejiuza lakini anajifaragua tu. ‘Kwani muuzaji si anajulikana tu. Wewe sema dau lako twende tukamalizane.’ Nilisema kwa kujiamini. 

Yule msichana alikasirika na kuanza kunishushia matusi. Wale wenzake watatu nao wakaingilia. Halafu ghafla ikatokea mijamaa miwili iliyoshiba hasa. Wale wasichana bila kuulizwa wakawa wanashitaki kwa ile mijamaa. Bila hata kuuliza ile mijamaa ikanivaa kutaka kunipiga, nikajifanya nawatishia kuruka sarakasi za Kichina kama Bruce Lee huku nikitoa mlio kama wa Paka.

Weweee…………., ile mijamaa ilivaa na kunitandika kisawasawa, waliokuja kuniokoa ni walinzi wa pale kwenye sinema, lakini nilikuwa nikitoa damu mdomoni na uso ulikuwa umevimba kama kiboko. Wale walinzi waliniuliza ninapoishi nikaawambia, ikabidi wawaombe vijana fulani waliokuwa wanaishi maeneo hayo ya Kariakoo wanisindikize nyumbani, kwani nilikuwa hoi hata kutembea nilikuwa nachechemea. 

Wakati huo ilikuwa ni usiku wa manane. Tulipofika nyumbani wale jamaa waligonga mlango kwa fujo hadi wapangaji wote katika nyumba ile wakaamka.

Miongoni kwa majirani walioamka kulikuwa na mabinti fulani nilikuwa nikiwaringia kwa kiingereza changu cha bush kuwakoga kuwa ni msomi, na walikuwa wananichukia kweli kutokana na tabia yangu hiyo ya kujifanya mjuaji. Nilipowaona wale mabinti niliishiwa na nguvu kwani nilijua kila kitu kitakuwa peupe. Kaka aliponiona katika hali ile alishtuka sana na kuwauliza wale jamaa walionisindikiza, ni kitu gani kimenipata. Wale jamaa walikuwa kama waandishi wa habari, kwani hawakumung’unya maneno, walisimulia kila kitu bila kuficha. Niliwaona wale mabinti wakikonyezana kisha wakacheka kicheko cha umbeya na kusema, ‘leo msomi kakutana na wasomi wenzie.’ Sikujibu kitu nilibaki kuwangalia huku nikiwa nimetahayari.

Kaka alikasirika sana na alinichukua na kunipeleka hospitali kwa matibabu, lakini aliniahidi kwamba nikipona lazima anirudishe kijijini kwani hayuko tayari kuishi na muhuni. Ni kweli kaka alikuwa amedhamiria, kwani baada ya siku tatu nilipata nafuu na alinipeleka stendi pale Kisutu na kunipakia kwenye basi kunirudisha kijijini. Nilirudi jijini Dar mwaka mmoja baadae nikiwa nimepambazukiwa.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Mzee Mtambuzi

A freelance Journalist and also teaching self-empowerment, positive thinking as a means of creating the life you desire including spirituality. He is writing in Mwananchi Scoop every Wednesday Visa na Mikasa.


Latest Post

Latest Tags