Ilikuwa ni mwaka 1999 baada ya kumaliza masomo yangu ya kidato cha nne na kuangukia pua ndipo nilipokuja mjini na kufikia kwa shangazi yangu maeneo ya Temeke Mikoroshini Kwa Mpelumbe. Baada ya kusota bila kazi kwa muda mrefu kidogo, niliamua kuhamia ghetto kwa washkaji zangu na kuanza kubangaiza na biashara ndogo ndogo za kimachinga.
Nilimudu kidogo kujikusanyia fedha na kila ninapoenda kijijini nilikuwa najipiga viwalo vya mitumba na kutamba kwamba mimi ni mfanya biashara mkubwa hapa jijini Dar.
Kwa kuwa nilikuwa natembeza nguo za Mitumba, ilikuwa rahisi kwangu kupiga pamba za nguvu hivyo kuweka mazingira ya kuaminika kwamba kweli mimi ni mfanyabiashara mkubwa.
Kwa hiyo kila ninapoenda kijijini najitahidi kuwaonyesha wanakijiji kuwa mambo yangu sio mabaya. Hata hivyo kwenye familia yetu walikuwa wanaujua ukweli kwamba nilikuwa choka mbaya.
Siku moja nikiwa kijijini nikiwa nawanunulia jamaa zangu pale kijijini bia nilikuwa natamba sana kwamba huku jijini Dar ninamiliki maduka ya kuuza spea za magari na wapo niliowaahidi kuwapa ajira.
Kutokana na kutamba kwangu na kumwaga kwangu ofa, nilijikuta nikiwa nimezungukwa na wapambe kibao, huku totoz kama kawa zikiwa nazo hazichezi mbali. Nilikuwa nawabadilisha mabinti kama nguo kwani walikuwa wakinizimikia kutokana na maujiko yangu.
Wakati bado nikiendelea kumwaga ofa za bia huku nikiendelea kujimwagia maujiko mara akaja jamaa mmoja. Duh, umekuja mshkaji, mimi niko hapa tangu wiki jana.' Alisema yule jamaa.
Huyu jamaa tulikuwa tunabangaiza wote mjini na tulikuwa tunaishi ghetto moja tukiwa tumelundikana kama watu sita katika chumba kimoja.
Ukweli ni kwamba sikujua kwamba mshkaji naye ni mwanakijiji wa pale kijijini kwetu, ingawa najua ni mwenyeji wa wilaya yetu. Ni kweli wiki mbili zilizopita alituaga kwamba angesafiri kumuona mama yake.
‘Siku hizi na mimi ni mwanakijiji hapa, mama ameolewa hapa na mzee…..Alimtaja mzee fulani.’
Sasa mzee lete habari maana ngalambe zetu mjini tunazijua wenyewe' Alianza kusema na nilianza kuhisi hatari ikija.
Halafu aliendelea ‘Wazee huyu ni jamaa yangu kabisa. Wiki iliyopita tu tulikuwa tunakabiliana na mama mwenye nyumba tunayoishi.
Tumepewa notisi kuhama kwenye ghetto yetu, si mnajua maisha ya Bongo yalivyo, mtu sita chumba kimoja, mambo magumu washkaji msije mjini'
Kila nikimzuia asizungumze, naona mwenzangu anachanja mbuga tu kutoa siri za maisha yetu ya Dar.
Mwisho wake wapambe wangu wakaanza kuhoji kuhusu anachosema yule jamaa. Jamaa naye bila ajizi aliendelea kusema ukweli kuhusu maisha yetu mjini. Nilipoona vile kwa sababu namjua kuwa ni mgomvi, niliona bora niondoke badala ya kubishana naye.
Kwa kweli kesho yake nikakuta taarifa zile zimeenea kijiji kizima kwamba, huko Dar niliko nabangaiza tu na sina maduka ya spea za magari wala nini. Ilibidi niondoke siku hiyo hiyo na kwenda kulala kijiji kingine cha jirani na kusafiri siku iliyofuata kurudi Dar.
Lakini nashukuru, jamaa alinisaidia. Kwani baada ya pale niliamua kuwa mkweli. Leo hii hata hivyo maisha yangu yamebadilika na yamekuwa mazuri kiasi cha kutosha. Lakini siku zote nakuwa mkweli sitaki kupanda zaidi ya nilivyo katika hali halisi.
Leave a Reply