Inaendeleaa..
Ni kweli yule bwana alionekana kuwa na uwezo pale kijijini, alikuwa na nyumba mbili zilizoko karibu, ng’ombe wa maziwa kadhaa, mashine ya kusaga nafaka na kukoboa inayotumia mafuta, alikuwa na jenereta kubwa na magari mawili, Toyota Canter na Toyota Hilax na pale kwake kulikuwa na duka kubwa la jumla na rejareja akisaidia kuwauzia wafanya biashara wa pale kijijini na vijiji vya jirani bidhaa. Ukweli ni kwamba kwa viwango vya pale kijijini alikuwa ni tajiri mkubwa.
Usiku baada ya kupata mlo wa usiku tulikaa kibarazani kwake kupiga soga kidogo ili kufahamiana zaidi.
Alinidadisi sana ninapotoka na alionekana kutabasamu kila nilipokuwa nikimueleza kuhusu kijiji nilipotoka.
Baadaye alijitambulisha kwangu kwamba na yeye anatokea kijiji hicho hicho, na alinitajia jina lake halisi, kumbe jina alilokuwa akilitumia ni jina jingine kwa sababu alitoroka pale kijijini na kukimbilia Morogoro ambapo slipofika alibadilisha jina na kujiita Mikwambe. Na hata bishara zake zilijulikana kwa jina hilo.
Nilimkumbuka lakini sikusimulia kisa chake cha kujinyea darasani ingawa yeye alikisimulia kwa dhihaka huku tukicheka wote. Alisema kwamba ile kujinyea ndiyo ilikuwa cheti chake cha kumaliza masomo na sasa ameitumia elimu ile ya darasani ya kukejeliwa, kudhihakiwa na kudhalilishwa kuonyesha uwezo wake wa kutafuta fedha na sasa ni tajiri pale kijijini.
Kwa kifupi tu alinieleza kwamba mtaji wake ulikuwa ni nguvu zake mwenyewe, alianza kulima vibarua baadaye akawa anakodisha ardhi na kulima, akafanikiwa kuvuna mazao mengi kwa takriban misimu minne akafanikiwa kununua ardhi na kujiandikisha kama mwanakijiji na kuanza biashara mpaka kufikia hapo alipofikia.
Alinisimulia kwamba wazazi wake walirudi kwao huko sambaani na amefanikiwa kuwajengea nyumba nzuri na alifanikiwa kuwasomesha wadogo zake wote na mwingine yuko nao pale wakimsaidia shughuli za biashara na wengine wako jijini Dar ni watumishi serikalini na mmoja ni daktari hospitali moja ya wilaya mkoa wa Pwani.
Ukweli ni kwamba huyu kijana kwa asili wao walitokea sambaani, na baba yake alihamia kijijini kwetu upareni kama manamba kufanya kazi kwenye mashamba ya mkonge, ni baada ya zao hilo kukosa umaarufu ndipo baba yake akaanza kulima vibarua kwenye mashamba ya wenyeji pale kijijini ili kujikimu.
Tuliongea mengi, lakini kubwa kuliko alitaka kujua wale tuliokuwa tukiongoza darasani wakati ule shuleni tunafanya kazi gani au tunafanya shughuli gani.
Nilimwambia ukweli kuhusu maisha yangu na kazi ninazofanya na nilimweleza kidogo kuhusu wenzangu wengi tuliokuwa vinara darasani kwamba wengi hawana maisha mazuri sana, wachache wameajiriwa kama mimi, wengine wamekuwa madereva wa mabasi na malori na maisha yao bado ni ya kubangaiza, na wengine ni walevi kupindukia tena mmoja ambaye alikuwa ni namba moja mpaka alipofika sekondari bado alikuwa na akili sana, alikuja kufeli kidato cha sita ikawa ndiyo graduation yake ya kuhitimu na kujikita kwenye pombe hadi sasa maisha yake si mazuri.
Alionekana kufurahi kupata habari za kijijini kwetu, alikiri kwamba hakuwahi kurudi pale kijijini zaidi ya kuwatumia wazazi wake fedha na kuwahamishia kijijini kwao huko Sambaani Lushoto ambapo aliwajengea nyumba na kuwafungulia biashara pale kijijini kwao.
Kwa kifupi simulizi yake ilinipa hamasa ya kutokata tamaa katika maisha...
Leave a Reply