Msagati akakimbilia morogoro...!

Msagati akakimbilia morogoro...!

Kwenye miaka ya mwanzoni mwa 1980, nikiwa shule ya msingi alitokea kijana mmoja ambaye alikuwa ni mtupu kabisa darasani.

Elimu ya darasani kwa kweli ilimshinda, nadhani alikuwa na tatizo ambalo kitaalamu linajulikana kama dyslexia, (Nilikuja kujua baadaye sana katika tafiti zangu)  hili ni tatizo la mtoto kushindwa kusoma kabisa au kuwa na uelewa mdogo sana wa masomo, ni tatizo ambalo linahitaji waalimu walioandaliwa katika kuwafundisha watoto wenye tatizo hilo ambapo kama wakifundishwa kwa kutumia mbinu zilizopendekezwa na wataalamu wa saikolojia huja kuwa wasomi wazuri huku mbeleni.

Huyu kijana aligeuzwa kuwa kama kituko pale darasani na hata waalimu walikuwa walimtolea mfano mbaya kwamba atakuwa na maisha magumu huko mbeleni kwa sababu ya kushindwa kusoma na kuandika wakati huo tukiwa darasa la nne.

Hakuwa ni mtu mwenye furaha kwa sababu pia hakuwa na marafiki na hata familia alimotoka ilikuwa ni ile ya wazazi kulima vibarua na kuuza mboga pori za majani na kuni ili kumudu kujikimu, na yeye pia alikuwa akiwasaidia wazazi wake kulima vibarua na wakati mwingine alileta ubuyu au ukwaju na kuchuuza shuleni. 

Mara kwa mara alikuwa akirudishwa nyumbani kutokana na kukosa sare za shule na ilikuwa inamchukua muda kupata sare na kurejea shuleni, alizidi kuanguka katika masomo na hakuna aliyeonyesha kujali si waalimu wala wanafunzi wenzie, sana sana tulikuwa tukimcheka kila alipokuwa akipata sifuri kwenye mitihani.

Ilitokea siku moja alipata mchafuko wa tumbo darasani akajisaidia palepale darasani na kujichafua, harufu ya kinyesi ilisambaa darasa zima akawa anatafutwa aliyechafua hali ya hewa na kwa bahati mbaya mwalimu wa sayansi kimu alikuwepo darasani akifundisha alishindwa kuvumilia hali ile ikamlazimu aulize aliyechafua hali ya hewa ni nani. Wanafunzi waliokuwa naye karibu wakamnyooshea vidole.

Kilichotokea ni kwamba yule kijana alitoka mbio huku kinyesi kikidondoka sakafuni. Na sisi wanafunzi tukatoka mbio kumkimbiza huku tukimzomea.

Hakukimbilia kwao, bali alikimbilia upande ilipo reli na huko aliokota mawe na kuanza kuturushia, ikumbukwe kwamba kwenye reli kunawekwa mawe ili kuzuia reli isididimie ardhini.

Tulipoona mashambulizi ya mawe yamezidi tukarudi darasani na kulazimika kusafisha darasa na kipindi kikawa kimeisha.

Ile ilikuwa ndiyo graduation ya kijana yule kwani alitoweka pale kijijini na hakuna aliyejua kaelekea wapi. Hata wazazi wake hawakuonekana kujua alipokimbilia na hakuna aliyeonekana kujali.

Tulimaliza darasa la saba na kile mtu akandelea na masomo kivyake kwa sababu wakati ule kutokana na uhaba wa shule za serikali kufaulu ilionekana kama vile ni miujiza, au bahati nasibu, kwa hiyo wazazi wengi walilazimika kuwapeleka watoto wao shule za sekondari za kulipia.

Miaka ilisonga na maisha yaliendelea.

Miaka 20 baadaye nikiwa katika utafiti wangu wa tiba mbadala kwa kutumia mitishamba, nilijikuta nikiwa Morogoro vijijini, huko sikuwa na mwenyeji nilipanga tu kufikia hata kwa mwenyekiti wa kijiji au katibu kata anipe japo hifadhi kwa muda nifanikishe utafiti wangu.

Nilipogika mwenyekiti wa kijiji kile aliniambia atanipeleka kwa bwana mmoja ambaye angeweza kunipa hifadhi kwa kuwa ana nyumba kubwa.

Nilipofika alinitambulisha kwa jina langu la ukoo, yule bwana akaonekana kushtuka lakini hakusema kitu.

Itaendelea………..

 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Mzee Mtambuzi

A freelance Journalist and also teaching self-empowerment, positive thinking as a means of creating the life you desire including spirituality. He is writing in Mwananchi Scoop every Wednesday Visa na Mikasa.


Latest Post

Latest Tags