Mrs Energy awahamishia upepo mashabiki wake

Mrs Energy awahamishia upepo mashabiki wake

Na Aisha Charles

Safari moja huanzisha nyingine, ndivyo ilivyo kwa mchezaji dansi Set Fibby, maarufu kama Mrs Energy, baada ya kuamua kujikita katika muziki wa Bongo Fleva, hali ambayo imewashangaza watu waliomzoea katika kucheza nyimbo za watu mitandaoni kama TikTok na kwingineko.

Hivi karibuni msanii huyo ameonekana kutocheza mara kwa mara mtandaoni, hali ambayo imeonekana kuwanyima mashabiki wake ile ladha ya mwanzo lakini kupitia Mwananchi Scoop, Mrs Energy amefunguka sababu.

“Kiukweli sasa hivi nimekuwa sifanyi dansi challenge za watu ila mara nyingi sana kwa wakati huu nimekuwa nikicheza nyimbo zangu tu kwa sababu mimi ndiye mtu pekee wa kuzipromoti,” amesema.

Aidha amesema kuwa hawezi kuwaangusha mashabiki zake katika kudansi kwa sababu ameingia katika muziki na sasa anaimba na kucheza.

“Mashabiki wangu siwaangushi kwa sababu naimba lakini sijasahau kucheza, ila watambue na wakubali mabadiliko yangu,” amesema Mrs Energy ambaye amewahi kufanya kazi na Diamond Platnium.

Hata hivyo, msanii huyo amesema kuwa tangu alivyoingia kwenye muziki ushirikiano na wanamuziki wengine wakubwa umekuwa kiasi tofauti na alivyotarajia huku akidai wanahitaji kumuona kwa ukubwa zaidi.

 

“Sapoti na wasanii wengine wakubwa ambao nimewakuta kwenye muziki ipo kiasi ila kwa sasa wanahitaji kuona 'movement' zangu kwa ukubwa zaidi ndipo mambo mengine yaendelee,”anasema.

Pia dansa huyo amefunguka kuwa muziki unampa thamani kuliko kucheza kwenye mitandao, ambapo amedai kuwa muziki ni hatua nyingine kabisa katika sanaa.

“Kwangu mimi naona dansi inaweza kukupa thamani jinsi utakavyojiweka na utakavyo jitengeneza lakini muziki unakupa thamani kwa sababu ni sehemu nyingine ya mafanikio, vyote vina thamani lakini vinazidiana, muziki uko juu zaidi,” anasimulia.

Utakumbuka Mrs Energy alivyoanza masuala ya muziki kuna baadhi ya watu walidai kuwa hataweza na siyo hadhi yake lakini kwa upande wake anasema kuwa anaichukulia kama changamoto na haimpi shida.

“Hali ya kukatishwa tamaa kwenye maisha ipo kila siku tena ipo kwa ukubwa ila uzuri wangu nikiona hivyo, sioni kama ni changamoto kwa sababu napata nguvu ya kuendelea,” anasimulia.

Mpaka sasa tayari ameshafanya nyimbo tano zikiwemo What is Love, Nimtaje, Maji Maji, Nilale na Taradadi ambayo ina siku tatu tangu itoke.

Utakumbuka amewah kuoneka akidansi kwenye Nyimbo ya ‘Jeje’, ‘Shu’ ya (Diamond Platnumz), ‘Nani’, ‘Honey’, (Zuchu) na nyengine nyingi.
.
.
.
#MwananchiScoop
#BurudikaNasi






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Asha Charles


Latest Post

Latest Tags