Mitoko (Dating) kwa wanawake wengi ni kama vile kwenda kununua Ice Cream.
Kila mara mwanamke anajaribu aina tofauti ya Ice Cream ili kuangalia ni ipi yenye ladha nzuri itakayomvutia.
Nyingine yaweza kuwa inavutia kwa nje lakini baada ya kuijaribu anakuja kugundua kwamba haina ladha aliyokuwa anaitarajia, nyingine inaweza kuwa haina mvuto kwa nje lakini baada ya kuijaribu anagundua kwamba ni nzuri na ina ladha aipendayo na hivyo inakuwa ndiyo chaguo lake la kila mara apatapo hamu ya kula Ice Cream.
Hivyo ndiyo ilivyo kwa baadhi ya wanawake, pale wanapokuwa katika harakati za kuwinda ili kumpata mwanaume sahihi wa kufunga naye pingu za maisha.
Siku hizi si ajabu kukuta mwanamke anakuwa na mitoko na wanaume tofauti tofauti ikiwa ni katika kujipa nafasi ya kufanya uchaguzi sahihi wa mwanaume wa maisha yake.
Ukweli ni kwamba si vibaya kwa mwanamke kuwa na mitoko na wanaume tofauti tofauti ili mradi tu isiwe ni zaidi ya mtoko.
Kutoka na mwanaume kwa ajili ya kupata chakula cha mchana au cha usiku au hata kama ni kwa kupata vinywaji au kahawa haimaanishi kwamba tayari mmeshakuwa na uhusiano, bali inafungua ukurasa wa kufahamiana ili kila mmoja kumpima mwenzake kulingana na vigezo alivyojiwekea kwa mpenzi amtakaye.
Ninachojaribu kusema hapa ni kwamba, si vibaya kwa mwanamke kuwa na mitoko na wanaume tofauti tofauti kwa sababu kuwa na mtoko na mwanaume haimaanishi kwamba ndio mmeshakuwa wapenzi, kwani hata huyo mwanaume unayetoka naye inawezekana na yeye pia anatoka na wanawake tofauti tofauti katika kutafuta yule atakayemfaa, kwa hiyo hilo siyo jambo la ajabu.
Wapo baadhi ya wanawake wakishakuwa na mtoko na mwanaume mmoja basi hufunga milango kabisa na kukataa mitoko na wanaume wengine kwa hofu kwamba yule mwanaume aliyetoka naye awali akijua anaweza kumuona kama hana msimamo.
Kama mwanamke ni mkweli wa nafsi na ameweka msimamo wake mapema kwa huyo mwanaume aliyeomba mtoko naye, ni lazima ataheshimu makubaliano.
Ukweli ni kwamba kung’ang’ania mtoko na mwanaume mmoja mara kwa mara hutengeneza mazingira ya kutamaniana kimwili na hapo ndipo utakuta mwanaume anatumia nafasi hiyo kutaka zaidi ya mlivyokubaliana na mwishowe mwanamke anajikuta ameingia katika hatua ya kukutana kimwili kabla hajajiridhisha kuhusu tabia na mwenendo wa mwanaume huyo.
Hata hivyo ningependa kutahadharisha, wapo baadhi ya wanawake ambao wanaweza kuwa na mtoko na wanaume tofauti tofauti, lakini kwa bahati mbaya wengi huangalia zaidi uwezo kiuchumi wa kila mwanaume anayetoka naye badala ya kutumia nafasi hiyo kumjua mwanaume huyo kiundani kuhusu tabia na mwennedo wake katika uhusiano.
Kwa muktadha huo unaweza kukuta mwanamke anakuwa na orodha ndefu ya wanaume aliowahi kuwa na mtoko nao na kila akijaribu kumpima kila mmoja kulingana na kigezo cha uwezo wa kiuchumi na atakayeweza kumtimizia mahitaji yake yote anakuta hakuna hata mmoja, anajikuta amepoteza muda wake mwingi na hakuna alichaoambulia.
Unaweza kumkuta mwanamke anakuwa na mtoko na mwanaume lakini kichwani amebeba orodha ya sifa za mwanaume amtakaye, hivyo katika mazungumzo yake na mwanaume huyo bila kujijua anakuwa kama vile anahakiki orodha yake ili kujua kama mwanaume huyo atafaulu vigezo vyake.
Kwa hiyo atakuwa anawekea alama zake kichwani kulingana na kila sifa aliyojipangia na mwisho wa siku anamtosa huyo mwanaume kwa sababu hajafikia viwango alivyojiwekea.
Tatizo ninaloliona kwa wanawake wengi ni kwamba, wanaume wenye sifa wanazozitaka hawajawahi kuwepo hapa duniani, na ndio maana hupoteza muda mwingi wakicheza mchezo wa kupapasa kama vile wanachagua embe.
Sinahitaji muda wa kutosha ili kumjua mtu vizuri zaidi na kama mwanamke akiutumia muda wake vizuri na kwa uhuru bila kusukumwa hakika atapata matokeo mazuri, lakini akisubiri mpaka machweo halafu jamii ikaanza kumnyooshea vidole ikijiuliza ana kasoro gani mpaka umri huo hajaolewa atajikuta anaolewa na yeyote kwa sababu ya kuogopa kunangwa na jamii.
Leave a Reply