Miaka 25 ya Daz Nundaz na jinsi Ferooz, Daz Baba wanavyokomaa

Miaka 25 ya Daz Nundaz na jinsi Ferooz, Daz Baba wanavyokomaa

Cha kale dhahabu. Muziki wa Bongo Fleva umepita kwenye mikono ya wakali mbalimbali walioacha alama kwa tungo zao zinazofanya waendelee kukumbukwa na mashabiki wa muziki hapa nchi.

Tangu miaka ya tisini kiwanda cha Bongo Fleva kilikuwa na makundi mengi yaliyotisha kwa ngoma zao. Kulikuwa na East Coast Team, GWM (Gangster With Matatizo), Wanaume Family, Hard Blasters, Gangwe Mobb, Mabaga Fresh, Solid Ground Family, Kwanza Unit na mengineyo. Mbali na hayo kulikuwa na hili la Daz Nundaz lililobebwa na wasanii watano Ferooz, Daz Baba, Critic, La'Rumba, na Sajo.

Tungo za wakali hao wa Kundi la Daz Nundaz, zinaendelea kuishi kutokana na ngoma zao ambazo hadi leo zikipigwa watu lazima wasimame, wakumbukie enzi kama ile ya “Nitafanya Nini Sasa” na "Kamanda" inayotumika wimbo wa maombolezo usiochuja.

Daz Nundaz hawakutengeneza jina na ngoma kali tu bali utamu wa nyimbo zao ulibebwa na aina ya tungo zilizowekwa kwa mfumo wa simulizi, na kupelekea mashabiki kutochoka kufuatilia hadi mwisho wa mkasa, yaani hazikuwa nyimbo tu bali zilikuwa na muvi ndani yake, ukitaka kuelewa hilo sikiliza ngoma yao itwayo "Barua".

Ukali wao wakiwa kwenye kundi hilo si kama uliwabeba, bali kila mmoja alikuwa na uwezo wa kutosha kuwaburudisha mashabiki, kama alivyofanya Daz Baba kwenye ngoma zake kama vile "Namba Nane" aliyomshirikisha mkali Farid Kubanda 'Fid Q', Nipe Tano, na hata Wife aliyomshirikisha Albert Mangwea.

Si yeye tu, Ferooz naye alikuwa na makali yake kwa ngoma kama vile "Wema Umeniponza", "Jirushe", "Starehe" na nyinginezo. Ndivyo ilivyokuwa kwa Sajo na wengine pia.

Kundi la Daz Nundaz ambalo safari yao ilianza rasmi mwaka 1999 walipoanza kutumia jina hilo, leo hii tukiwa katika mwaka wa 25, Ferooz na Daz Baba bado wanapambana katika muziki, kwa upande wa Critic sasa ni mchungaji, na La’Rhumba ni mfanyabiashara.

Kwa upande wa Sajo baadaye akaamua kuingia darasani, akapata shahada ya Sanaa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Akaenda Chuo Kikuu Huria na kupata Shahada ya Uzamili ya Maendeleo ya Jamii. Pia ana stashahada ya umahiri (postgraduate diploma) aliyoipata kutoka Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji,kilichopo Mbeya.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Christina Lucas


Latest Post

Latest Tags