Kama utani vile, imetimia miaka 10 tangu aliyekuwa mwanamuziki wa dansi, Ramadhan Masanja ‘Jenerali Banza Stone’ kufariki dunia.
Leo Julai 17, 2025 ni siku ya kumbukumbu ya kifo cha msanii huyo aliyefariki mwaka 2015 kutokana na ugonjwa wa saratani ya ubongo.
Mkali huyo aliyewahi kutamba katika bendi mbalimbali za muziki wa dansi baada ya awali kutamba kama dansa, alikumbwa na umauti akiwa nyumbani kwao Sinza, jijini Dar es Salaam alipokuwa akijiuguza na kuzikwa Julai 18, 2015 katika makaburi ya Sinza.
Enzi za uhai wake, Banza aliingia katika kitabu cha watu maarufu wenye uwezo wa kutunga nyimbo, kuimba, kurap na kucheza na kujizolea mashabiki wengi hadi kupewa majina yakiwamo ‘Mwalimu wa Walimu’.
Pia Banza alijizolea umaarufu mkubwa kupitia tungo za nyimbo zake kuanzia Mtaji wa Maskini, Elimu ya Mjinga, Angurumapo Simba, Kumekucha, Falsafa ya Maisha na Nilipoanza Mwana Masanja, Mtu Pesa na nyingine ambazo hazichuji masikioni mwa mashabiki wa muziki wa dansi.
Nyota huyo aliyezipigia bendi kama Bambino Sound, African Stars ‘Twanga Pepeta’, TOT Plus na hadi alipokumbwa na mauti, alikuwa ameacha mtoto mmoja aitwaye Haji Ramadhan Masanja, ambaye naye alifariki dunia miaka mitano baadaye.
Familia yajipanga
Mwananchi limeweza kufika Sinza nyumbani kwa familia ya Banza Stone, na kuzungumza kuhusu siku hii ya kumkumbuka mpendwa wao.
Pia lilizungumza na baadhi ya wasanii wa muziki wa dansi kwa nyakati tofauti kuhusu miaka 10 ya kifo cha Banza Stone, muziki wa dansi uelekeo wa muziki huo ukoje tangu ameondoka Banza na mabadiliko gani hapo kuhusu ushindani kama upo.
Akizungumza kwa uchungu, kaka wa nyota huyo wa zamani wa dansi, Hamis anasema siku ya leo hakuna kitu kikubwa watakachokifanya zaidi ni kumuombea tu Banza Stone
“ Ni siku ya kufanya dua, tutamuombea dua Banza kwa Mwenyezi Mungu ampunguzie adhabu ya kaburi, pia dua hii tunaiunganisha kumuombea mama mzazi na mtoto wake Haji,” alisema Hamis na kuongeza;
“Mama alifariki dunia Februari 29, 2016 na mtoto wa Banza, yaani Haji alifariki dunia Juni 9, 2020, hivyo wote tutawaombea dunia katika kumbukumbu hii ya miaka 10 ya Banza Stone.”
“Nikijibu swali lako la kuhusu wasanii wenzake kuja hapa nyumbani kama zamani au kusalimia kwa njia ya simu ukweli wamepotea kabisa hakuna hata mmoja anayekumbuka kufanya mawasiliano nasi.
"Na wapo wengine unawaona wanapita hapa hapa nyumbani, uzuri nyumba yetu iko barabarani na ikitokea mtu amekaa nje anaona wote wanaopita njia, na hatuwalaumu ila kikubwa sisi tunamuombea tu dua ndugu yetu kila wakati,” aliongeza.
Kauli za wasanii
Nyoshi El Saadat
Huyu ni kiongozi na mkurugenzi wa bendi ya Bogoss Musica. Anasema: “Banza Stone alikuwa mwanamuziki mwenye uwezo mkubwa sana kwenye huu muziki wa dansi, enzi za uhai wake alikuwa analeta ushindani mkubwa sana na uzuri kipindi kile dansi lilikuwa bado la moto, ila kwasasa hakuna ushindani wowote zaidi ya kila mtu hufanya kazi zake kutokana na mihemko yake mimi sioni ushindani na kama upo basi hautakuwa kama kipindi kile cha enzi za Banza Stone.”
Chaz Baba
Kiongozi wa bendi ya Twanga Pepeta, Chaz Baba; “Kwanza niseme kumbukumbu yangu kwa Banza Stone ni hili jina la Chaz Baba alinipa yeye kwa hili najivunia sana, kwa wasiofahamu mimi naingia Twanga Pepeta mwaka 2004 nilikuwa naitwa Charles Gabriel lakini baada ya kuingia ndani ya bendi Twanga nilivyoanza kufanya kazi kwa mara ya kwanza Banza alinibadili jina na kuniita Chaz Baba kutokana na uwezo wangu wa kazi ukweli najivunia kila mtu kuniita Chaz Baba.
“Kuhusu tangu afariki dunia Banza Stone, mabadiliko kwenye muziki yapo kulingana na wakati huu uliopo, ila kipindi kile cha uhai wa Banza muziki huu ulikuwa juu zaidi na kulikuwa na ushindi mkubwa sana. Bendi kama FM Academia, Twanga Pepeta, Tam Tam, Msondo Ngoma, Sikinde zilikuwa na wanamuziki kama Ally Choki, Nyoshi El Saadat na Muumini huku nasisi tukipambana na rika letu la kina Khalid Chokoraa, Jose Mara na wengine.”
Kwa sasa dansi limeamka kivyake na kama muziki kuuliwa basi ni sisi wenyewe kwenye bendi, lakini dansi ni muziki mkubwa na una mashabiki wengi wanaibuka kila wakati, ila kwenye suala la kuimba sauti ile ya Banza hakuna mtu mwenye kuziba pengo”.
Juma Katundu
Kiongozi wa Msondo ngoma anasema, “Banza atakumbukwa kwa kuimbaji na kutunga nyimbo zake, kucheza na sauti yake nyimbo zake za kuelimisha maisha, zimekuwa zikiendelea kufanya vizuri hadi sasa hii ni kutokana na kuwa mwanamuziki bora, atakumbukwa kwa mengi ni mtu ambaye alikuwa ni mmoja wa kuleta ushindani kwenye muziki wa Dansi “.
Ally Choki
Kiongozi wa bendi ya Extra Bongo anasema; “Kwenye suala la wasanii kutofanya mawasiliano na familia ya Banza, hii wako sahihi kabisa familia inavyosema mawasiliano hakuna kama alivyokuwepo hai, hii ni asilimia kubwa sisi Watanzania sio Banza tu hata mimi siku Mungu akinichukua familia yangu hawatakuwa na mawasiliano na watu wangu na hii ni kutokana na familia haikuwa karibu na wanamuziki, hivyo imekuwa ugumu wa kuwazoea baada ya kifo cha Banza
"Kwenye suala la ushindani, kwa sasa hakuna ushindani wa kipindi cha Banza alipokuwa hai, hakuna vurugu vurugu za hapa na pale hekaheka za dansi hakuna, huenda pia nyakati zilizopo, si unaona sasa hivi singeli ndio ina nguvu kuliko muziki mwingine japo watu wa dansi tunaendelea kupambana tuurudishe muziki wetu”.
Banza ni nani?
Ramadhani Masanja ‘Jenerali Banza Stone’, alizaliwa Oktoba 20, 1972 katika Hospitali ya Ocean Road jijini Dar es Salaam akiwa ni mtoto wa mwisho katika familia ya Mzee Ally Masanja iliyokuwa na watoto wanane, iliyokuwa ikiishi Lumumba. Alipata elimu yake ya katika Msingi Shule ya Mnazi Mmoja kabla ya kuingia kwenye muziki.
Alikuwa akisoma pia elimu ya dini ambayo aliishika sana na hata akiwa madrasa alikuwa akisoma sana kaswida na akaamua kuanza muziki kwa kushiriki vikundi vya mtaani.
Alianza muziki katika kikundi cha kucheza disko kilichoitwa Octimas kabla ya kuhamia kundi la DBR na mwaka 1989 akaanzisha kikundi binafsi cha Home Boys akiwa na Elvis Danger (mpwa wake), Ashura Mponda na Ras Dee.
Mwaka 1992 akaenda kusoma muziki Chuo cha Utamaduni cha Korea alipomaliza akapiga deiwaka Twiga Band kabla ya kuanza rasmi muziki na kupitia bendi ya Afri Swez. Kipaji kilipozidi kupanda akaenda African Stars ‘Twanga Pepeta’, TOT-Plus akarudi Twanga na baadae akaanzisha bendi ya Bambino Sound iliyowaibuka kina Kalala Junior hii ikiwa ni mwanzoni mwa 2000.
Banza hakudumu na bendi hiyo kwani alihamia African Revolution ‘Chipolopolo’ kisha akaenda tena kuifufua Bambino lakini haikusimama na kuamua kurejea Twanga na kukaa kidogo kabla ya kwenda kuungana na Ally Choki aliyeanzisha Extra Bongo, kisha kupita BM.
Baadaye alipata deiwaka na bendi ya Rungwe iliyokuwa na maonyesho mjini Mbeya na shoo ya mwisho ilikuwa Februari 2015 alipoanza kuugua alirejeshwa jijini Dar na kujiuguza hadi alipofariki dunia.

Leave a Reply