MGONJWA, IJUE HAKI YAKO

MGONJWA, IJUE HAKI YAKO

Kufuatia video ya iliyosambaa mtandaoni ikiwaonesha wahudumu wa afya wakizozana kuhusu matibabu ya mgonjwa huku mmoja akipinga kitendo cha vifaa vilivyoisha muda kutumika, jarida lako pendwa la Mwananchi Scoop linakuletea makala kuhusu haki na wajibu wa mtoa huduma kwa mgonjwa.

HAKI ZA MGONJWA.

Mgonjwa afikapo katika kituo cha afya ana haki zake za msingi zinazotakiwa kufatwa na wahudumu za afya, pale zinapokiukwa inabidi kufikishwa katika mamlaka husika.

 1. Mgonjwa ana haki ya kupatiwa matibabu. Matibabu hayo ni pamoja na kinga, tiba, ushauri na huduma shufaa. Wagonjwa wenye mahitaji maalumu na wale wenye uhitaji wa huduma ya dharura ndo hupatiwa kipaumbele.
 2. Mgonjwa ana haki ya kupata taarifa za matibabu yake. Taarifa hizo ni taarifa za ugonjwa, matokeo ya uchunguzi, aina ya matibabu anayopatiwa, faida na hasara au madhara kama yapo ya kupata matibabu hayo. Huduma zinazotolewa, gharama za huduma.
 3. Mgonjwa ana haki ya kumtambua mtoa huduma anayemuhudumia. Mtoa huduma anaweza kuwa daktari, nesi au muuguzi. Mgonjwa ana haki ya kutambua jina lake na cheo chake, pia mgonjwa ana haki ya kumchagua mtoa huduma wa chaguo lake bila kuathiri matibabu na maamuzi ya wagonjwa wengine waliopo.
 4. Mgonjwa ana haki ya kukubali au kukataa matibabu. Kama mgonjwa hajaridhishwa na matokeo ya uchunguzi wa matibabu yake, ana haki ya kukataa matibabu, mtoa huduma anapaswa kumueleza mgonjwa huyo matokeo ya uamuzi wake na kuwekwa kwenye daftari la kumbukumbu. Watu wenye uhitaji maalumu, mfano; watoto, wazee na watu wenye matatizo ya akili hawawezi kufanya uamuzi wa kupatiwa matibabu kivyao, hivyo basi mzazi au mlezi wa mgonjwa huyo ndo atatoa uamuzi wa matibabu ya mgonjwa huyo.
 5. Mgonjwa ana haki ya kutunziwa taarifa za matibabu yake kwa usiri. Taarifa hizo hazitatolewa sehemu nyingine bila kuwa na ridhaa ya kimaandishi ya mgonjwa huyo au pale itakapohitajika na vyombo vya sheria. Pia mgonjwa ana haki ya kuhudumiwa kwenye mazingira ya faragha, kuzingatiwa utu wake bila kuathiri taratibu za matibabu.
 6. Mgonjwa ana haki ya kutoa maoni, malalamiko au pongezi kwa kituo cha afya alichohudumiwa. Pia malalamiko yake inabidi kushughulikiwa haraka ipasavyo bila upendeleo kwa kuchunguzwa na kufatiliwa na mamlaka zinazohusika. Na baada ya hapo mgonjwa kupatiwa taarifa ya hatua zilizochukuliwa. Hii husaidia kuboresha utoaji huduma.

Haki na wajibu wa mtoa huduma.

Mtoa huduma wa afya inabidi azingatie yafuatayo wakati akiwasilisha matibabu kwa mgonjwa;

 1. Mtoa huduma ana haki ya kuheshimiwa na mgonjwa.
 2. Mtoa huduma ana haki ya kutekeleza wajibu wake wa kitabibu bila kuingiliwa na mgonjwa. Hii inaambatana na kujadiliana na wataalamu wenzake na kufanya utafiti kuhusu matibabu ya mgonjwa bila kuvujisha siri za mgonjwa na bila kuingiliwa na mgonjwa.
 3. Mtoa huduma ana haki ya kuwasilisha malalamiko yake juu ya mgonjwa mahala husika na malalamiko hayo kufanyiwa kazi bila kuhatarisha ajira yake.
 4. Mtoa huduma anatakiwa kutoa huduma bora ya afya, kwa kuzingatia kanuni, maadili, umakini na uadilifu bila upendeleo katika mazingira salama yenye kumlinda mgonjwa.
 5. Kufanya kazi pamoja kwa ushirikiano na wahudumu wenzake wa afya katika kutoa huduma bora na kutoa maelezo na ushauri tosha kwa mgonjwa kuhusu afya yake.
 6. Kumkinga mgonjwa asipate maambukizi mapya anapokuwa akipatiwa matibabu na kituo cha afya
 7. Kukataa rushwa kutoka kwa wafanya kazi wenzake au wagonjwa.

Wahudumu wa afya wanaokiuka haki za wagonjwa inabidi waripotiwe na kufikishwa katika mamlaka husika mfano mahakama za afya, vyombo vya usimamizi vya afya ngazi za wilaya na mkoa.

Imeandaliwa na Mark Lewis


Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Detricia Pamba

A Digital Journalist, Content Creation Executive at Mwananchi Communications Ltd and Chief Editor of Mwananchi Scoop. I'm also writes stories around Technology, every Wednesday on Mwananchi Scoop. My other famous segments on Mwananchi Scoop include LISTI and WHO’S HOT.


Latest Post