Mfahamu zaidi Augustine Mrema

Mfahamu zaidi Augustine Mrema

Augustine Lyatonga Mrema mwanasiasa mkongwe nchini Tanzania ambaye wakati fulani alikuwa mmoja wa watu wachache maarufu zaidi ameaga dunia jijini Dar es Salaam katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa amelazwa kwa matibabu akiwa na umri wa miaka 77.

Mrema atabakia katika kumbukumbu za watu wengi hususan alipokuwa katika kilele cha umaarufu wakati wa uchaguzi wa Mkuu wa Tanzania wa mwaka 1995.

Huo ulikuwa uchaguzi wa kwanza baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa. Hii ilikuja kufuatia marekebisho ya ya Katiba ya Tanzania kuanzia Julai 1992, yaliyofuta mfumo wa chama kimoja cha siasa uliokuwa umedumu kwa  miaka 27 kuanzia 1965.

Akiwa mwanachama mgeni katika vyama vya upinzani Mrema alikoleza moto wa siasa baada ya kujiunga na kilichokuwa chama kikubwa zaidi cha upinzani cha NCCR-Mageuzi Februari 1995, kisha kuteuliwa kuwa mgombea wa urais kupitia chama hicho.

Katika uchaguzi huo, Mrema alikuwa mshindani wa karibu wa mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Benjamin Mkapa ambaye akiungwa mkono na muasisi na baba wa wa taifa hilo, Julius Kambarage Nyerere, hatimaye alishinda uchaguzi huo wa Oktoba 29,  kwa kunyakuwa asilimia 61.8 ya kura huku Mrema akiibuka wa pili kwa kupata asilimia 27.7 ya kura zote halali.

Licha ya kushindwa urais, nguvu ya Mrema ilikiwezesha chama cha NCCCR- Mageuzi kunyakua viti 17 vya ubunge Tanzania Bara. Kwa kipimo cha wakati huo hii ilikuwa idadi kubwa ya viti vya ubunge kwa kuzingatia miaka mingi ya nchi kuwa katika mfumo wa chama kimoja.

Miongoni mwa majimbo ambayo NCCR- Mageuzi ilishinda ni: Ubungo, Arusha Mjini, Mbeya Mjini, Iringa Mjini, Hai, Muleba Kaskazini, Vunjo, Urambo, Moshin Mjini, Musoma Vijijini na Bunda.

Hali hii ilionekana kuleta sura mpya katika Bunge lililokuwa na mchanganyiko wa wabunge kutoka vyama vya siasa. Ikumbukwe walikuwepo pia wabunge wa majimbo matatu ya Tanzania Bara: Karatu, Rombo na Kigoma Mjini kutoka chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) pamoja na wabunge zaidi ya 20 wa CUF kutoka Zanzibar

 Mara zote Mrema alikuwa akijinadi na kujenga wasifu wake juu ya uwezo wa ufuatiliaji wa kazi ikiwemo kuzuru maeneo tofauti kwa ghafla hata nyakati za usiku, na  kupambana na rushwa, ufisadi, magendo na ulanguzi wa mali.

Kabla ya kugombea urais alikuwa amehudumu katika serikali ya awamu ya pili ya Rais Ali Hassan Mwinyi akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kuanzia mwaka 1990 na ilipofika 1993 aliongezewa cheo cha Naibu waziri Mkuu ili kumpa nguvu zaidi ya utendani.

Alisifika kwa kuhamasisha umma kujenga vituo vya polisi ili kuimarisha ulinzi pamoja na kufuatilia kwa karibu utendaji kazi wa jeshi la polisi katika kuhakikisha usalama wa raia na mali zao. Pia uongozi wa Mrema ulihamasisha kuanzishwa kwa vikundi vya ulinzi vilivyoundwa na wananchi, maarufu Sungunsungu.

Hata hivyo, vikundi hivyo vya sungusungu mara kadhaa vilishutumiwa kwa kutumia nguvu kupita kiasi na kujichukulia sheria mkononi kwa kuwatesa baadhi ya watuhumiwa wa uhalifu.

Alipobadilishwa kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na kuhamishiwa wizara ya Kazi, Vijana na Michezo, akahamaki akidai mabadiliko hayo yalilenga kumnyamazisha asiendelee kupamba na na rushwa na wizi wa mali ya umma, akitolea mfano wa dhahabu iliyokamatwa uwanja wa ndege wa Dar es Salaam lakini wahusika hawakuchukuliwa hatua yoyote.

Hapo ndipo akahamia upinzani akipoteza kiti cha ubunge wa Moshi Vijijini alichokuwa amekishikilia tangu 1987.    

Hata baada ya kushindwa urais, Mrema aliendelea na harakati za kuchaguliwa kwani Novemba 1996 alichaguliwa kuwa mbunge wa Temeke mkoni Dar es Salaam katika uchaguzi mdogo, baada ya Mahakama Kuu kutengua matokeo ya uchaguzi wa ubunge wa 1995 yaliyompa ushindi Ally Ramadhan Kihiyo wa CCM kwa sababu za udanganyifu.

Baadaye Mrema alikihama chama cha NCCR-Mageuzi na kujiunga na Tanzania Labour Party (TLP). Hatua hii ilikuwa baada ya mgogoro mkubwa wa kiuongozi ndani ya NCCR-Mageuzi kiasi cha kukiyumbisha chama na kukosa wabunge kwa muda mrefu. 

Mrema Aligombea urais kupitia TLP mwaka 2000 na kushika nafasi ya tatu na mwaka 2005 alimaliza wa nne. Ni dhahiri kuwa matokeo hayo na idadi ya kura yalidhihirisha kushuka kwa umaarufu wake kisiasa.

Kwa takriban miaka 10 Mrema alikuwa Mwenyekiti wa bodi ya msamaha kwa wafungwa, maarufu bodi ya Parole, mara ya mwisho aliteuliwa na Rais John Magufuli mwaka 2020.

Agustine Mrema alizaliwa Desemba 31, 1944 katika kijiji cha Kilaracha huko Moshi vijijini mkoani Kilimanjaro, kaskazini Mashariki mwa Tanzania. 

Alisoma shule ya msingi huko kijiji kwao na baadaye kujiendeleza na kufanya mtihani wa sekondari mwaka 1968 wakati huo mitihani ikiandaliwa na chuo kikuu cha Cambridge cha Uingereza.

Mwaka 1970-71 alijiunga kwenye mafunzo maalumu ya siasa na uongozi katika chuo cha Kivukoni Dar es Salaam na mwaka 1980 na 1981 alikwenda Bulgaria mbako alifanikiwa kutunukiwa Diploma ya sayansi ya Ustawi wa jamii na Utawala.

Aliwahi kuhudumu pia kama Mwalimu katikka shule mbalimbali kabla ya kujiunga na Idara ya usalama wa Taifa. Huko amewahi kushika nafasi mbali mbalimbali ikiwemo kuwa Afisa Usalama wa Taifa mkoa wa Dodoma. Pia amewahi kuwa afisa mwanadamizi katika kituo cha Usalama wa Taifa kilichopo wilayani Kahama mkoani Shinyanga.

Atakumbukwa pia kwa kauli tata kadhaa alizowahi kuzitamka katika uwanja wa Siasa. Kwa mfano wakati wa uchaguzi mkuu wa 2010 na yeye akiwa anagombea ubunge wa jimbo la Vunjo, alitamka kuwa anamuunga mkono mgombea wa CCM wakati huo, Jakaya Kikwete huku chama chake cha TLP kikiwa na mgombea urais, Muttamwega Mgaywa.           

Machi 2022 Augustine Mrema alitawala mitandaoni kwa taarifa na picha zake  baada ya kufunga ndoa na Doreen. Watu wengi walizungumzia ndoa hiyo hasa kwa kuzingatia tofauti ya umri kati ya Mrema na mke wake Doreen. 

 

 chanzo bbc






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post