Mfahamu tapeli aliyeuza uwanja wa ndege

Mfahamu tapeli aliyeuza uwanja wa ndege

Emmanuel Nwude ni mmoja kati ya watu waliaondika historia kubwa nchini Nigeria kwenye masuala ya utepeli. Taarifa kutoka Daily zinaeleza kwamba Nwude ambaye aliwahi kuwa mkurugenzi wa moja kati ya benki nchini Nigeria alifanikiwa kutapeli zaidi ya Pauni 190 milioni kwa moja ya benki huko Brazil.

Inaelezwa kuwa Nwude alimpigia simu  Nelson Sakaguchi, aliyekuwa bosi wa benki ya  Banco Noroeste  huko nchini Brazil kisha akajifanya kuwa yeye ni Paul Ogwuma aliyekuwa gavana wa benki kuu ya Nigeria mwaka 1994. 

Alimpigia akimwambia kwamba Nigeria ilikuwa ikitaka mkopo wa kujenga uwanja wa ndege mpya na wakisasa  ambapo ilihitaji Pauni 200 milioni. 

Baada ya muda mrefu, kitu cha kushangaza ni kwamba Sakaguchi alikubaliana na ombi la Mr Nwude lakini kwa sharti la yeye kupata mgao wa Pauni 8 milioni katika sehemu ya mapato ya uwanja huo pale utakapomalizika. Nwude akakubali. 

Katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 1995 hadi 1998, benki hiyo kutoka Brazil ililipa kiasi kinachofikia Pauni 190 milioni kwa ajili ya uwanja wa ndege ambao hawakujishughulisha hata kwenda kuufanyia ziara ya kuuangalia.

Lakini ilipofika mwaka 1998, benki hii ilikuwa inauzwa kwenda kampuni ya Santander, hivyo ililazimika kwanza kufanyika mapitio ya matumizi yao kabla ya kuuzwa.

Ofisa kutoka kampuni ya Santander waliohitaji kuinunua benki hiyo aliuliza kwanini karibia nusu ya pesa ya mtaji wao ilikuwa inaonekana ipo nchini kwenye kisiwa cha Cayman.

Cayman kilikua ni kisiwa ambacho Nwude alikuwa akiishi na kufanya mipango yake yote ya utapeli hadi kufanikiwa kujipatia pesa nyingi kiasi hicho. 

Hii ilikuwa ni tofauti na vile ambavyo maofisa wa benki hii walikuwa wakifahamu, wao walijua pesa zao zinatumika nchini Nigeria kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa ndege.

Uchunguzi ukaanza kufanya kuanzia nchini Brazil, Uingereza, Nigeria, Uswiss na Marekani, wakagundua kwamba ni kweli wametapeliwa. 

Wakaaza harakati za kumtafuta Nwude pamoja na aliyeidhinisha pesa Nelson Sakaguchi ambao ilikuwa ngumu kuwapata.

Ilipofika mwaka mwaka 2004 walifanikiwa kumshika Sakaguchi kwenye uwanja wa ndege wa John F Kennedy na akapelekwa nchini Uswiss kwa ajili ya kusimamishwa mahakamani.

Wamiliki wa benki ya Banco Noroeste walilazimika kutoa pesa kwenye mifuko yao kwa ajili ya kuweka kama mtaji ili wafanikishe mchakato wa kuiuza benki hiyo wakati huo wakiendelea na mchakato wa kesi juu ya Nwude. 

Nchini Nigeria, rais wa wakati huo  Olusegun Obasanjo aliagiza kuundwa kwa tume ya uhalifu wa kiuchumi na fedha ambayo iliundwa na Bunge la nchi hiyo mwaka 2002.

Ilipofika mwaka 2004 baada ya msako wa muda mrefu Nwude na washirika wake Amaka Anajemba, Emmanuel Ofolue, Nzeribe Okoli, na Obum Osakwe walikamatwa nchini Nigeria na kufikishwa mahakamani ya juu huko Abuja kwa ajili ya kusomewa mashtaka yao na kupatiwa hukumu, lakini walikataa kuhusika na tuhuma 86 zilizokuwa zinawakabili.

Baada ya hapo ikaibuka skendo kwamba Nwude alikuwa amehonga kiasi cha pesa kwa baadhi ya wafanyakazi katika mahakama hiyo, lakini hakukuwa na ushahidi juu ya hilo.

 

Kesi ikasikilizwa tena mara yapili na Jaji   Lawal Gumi, alitoa uamuzi kwamba kesi hiyo haiwezi kusikilizwa Jijini Abuja kwa sababu tukio hilo halijafanyika huko.

Nwude na wenzake waliachiwa lakini walipotoka tu mahakamani wakakamatwa tena na kusafirishwa hadi Lagos ambako washirika wa Nwude ndio walikuwa wameweka makazi wakati wanafanya tukio hilo. 

Huko nako Nwude akadaiwa kutoa hongo la pesa ya Pauni 60,000 kwa maofisa wa mahakama wakati kesi hiyo inaendelea. 

Mambo yaliendelea na mwisho mmoja kati ya watu alioshirikiana nao kwenye utapeli huo Amaka Anajemba alikiri makosa na kuweka wazi kwamba alimsaidia Nwude kwenye utapeli huo. Amaka akafungwa jela miaka miwili na nusu na kutakiwa alipe fidia ya Dola 25.5 milioni.

Hata hivyo Nwude aliendelea kukataa hadi pale Sakaguchi ambaye ndio aliidhinisha pesa kutoka Brazil aliposimama kama shahidi wa kesi na kuthibitisha yote waliyofanya.

 Nwude alihukumiwa jela miaka 25 kisha akatakiwa kulipa fidia ya Dola 10 milioni kisha mali zake zote zikataifishwa kwenda kwa waathirika. Huku baadhi ya washirika wake wakifungwa miaka minne.

Aliachiwa mwaka 2006 ambapo alifungua kesi na kutaka kuridishiwa baadhi ya mali zake akieleza kwamba zilipatikana kabla ya kudaiwa kuhusika na utapeli huo. Akafanikiwa kurudisha mali zake zenye thamani ya Dola 52 milioni. 

Pia mwaka 2021, Nwude alifunguka kwamba yeye hakuwa anafahamu chochote kuhusiana na kesi aliyohukumiwa nayo ya kwamba ametapeli fedha zinazofikia Dola 242 milioni akidai kwamba timu yake ya wanasheria ndio ilimshauri akubali na baada ya hapo wataangalia namna ya kumsaidia na kupunguza hukumu yake.


Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post