Mfahamu Bondia Hassan Ndonga

Mfahamu Bondia Hassan Ndonga

Kwenye hii dunia bhana kila mmoja ana namna ya kujikomboa kwenye maisha yake na kuhakikisha kwa namna yoyote ile anafikia matanio au azma aliyojiwekea yeye binafsi.

Ni Ijumaa ya burudani leo, namleta kwako bondia mahiri kutoka hapa hapa nyumbani nchini Tanzania, sio mtu mgeni saaana machoni mwako na masikioni hapa na mzungumzia ngumi jiwe, Hassan Mohamed maarufu kama Hassan Ndonga.

Huyu ni kijana anayejihusisha na mchezo wa ngumi ambapo ana takribani miaka 4 sasa tangu alipoanza kuingia ulingoni kupitia mapambano mbalimbali ambayo amewahi kushiriki.

Ndoga ni kijana mwenye umri wa miaka 20 tu ambapo yeye kipaumbele chake kwenye maisha yake ni masuala ya ngumii pamoja na mazoezi yakutosha.

Akizungumza na Mwandishi wa makala hii, Ndoga ameeleza wazi kuwa ngumi sio mchezo wa kujipa ujiko bali ili uwe mpiganaji mzuri mchezo huu unahitaji mazoezi yakutosha.

Vilevile ameeleza kuwa mchezo huo sio lelemama, hauhitaji maneno ili watu wakutambue vizuri, lazima uonyeshe ufundi na uwezo ulionao kwenye kupigana hapo ndipo utakapoufahamu vizuri mchezo huo.

Hata hivyo alisema kuwa mchezo wa ngumi unaugumu wake bhana na ugumu mkubwa uko katika suala la mazoezi, ambapo unafanya mazoezi kwa muda mrefu halafu unakwenda kupambana ndani ya masaa 3 tu hapo ndipo utaona jinsi mchezo huo ulivyotofauti.

“Mimi kigumu ni mazoezi ambapo unajiandaa muda mwingi lakini unakwenda kupigana siku moja, unakuta hata saa 1 moja haimalizi ndiyo maana tunasema mazoezi ni magumu kuliko mechi yenyewe.”

Hata hivyo Hassan anaeleza kuwa siku ya kwanza kupambanishwa kwenye mchezo wa ngumi haikuwa rahisi na alipambanishwa na Isaya Ally na kufanikiwa kutoka sare.

“Kiukweli nilikuwa na hofu wakati niko ulingoni kutokana na kelele za watu matusi, vurugu na ukiwa uko ulingoni aisee hayo mambo huwa yanachanganya kabisa lakini nashukuru Mungu nilipambana kwa uwezo wa kufanikiwa kutoka sare.”

Umahiri wa kijana huyu kwenye kupambana katika mchezo wa ngumi ameeleza kuwa ndiyo umesababisha yeye kupata  heshima kwenye mchezo huo  kwani hakuwahi kupambana na kukosa pambano lolote lile tangu ameanza kushiriki kwenye mchezo wa ngumi.

Hassan amesema kuwa mchezo huo una changamoto nyingi ambazo anakutana nazo lakini mara nyingi anajitahidi kupambana nazo kulingana na mchezo ulivyo.

“Changamoto kubwa ambayo huwa inasumbua sana ni ile ya mashabiki unakuta siku ya kupima uzito unazomewa, zile ndo changamoto zinazosumbua lakini ukishazoea hakuna shida tena ndo challenge yenyewe,” anasema na kuongeza,

“Changamoto binafsi ninazo pia kwani awali nilipokuwa naanza nilikua napata ugumu kwenye vifaa, ukiangalia uwezo wangu ni wa hali ya chini kama zile bugati tunazopigania zile zinaanza 100,000  hadi elfu 70,000, kwahiyo unakuta mtu kama mimi sina lakini kwa sasa changamoto hizo sina kutokana na uongozi niliyokuwa nao.”

Sambamba na hayo, Hassan amelieleza jarida la Mwananchi Scoop kuwa jambo analotamani kufanyiwa kwa sasa ili aweze kufika mbali kwenye mchezo  huo ni kupata support tu, ana uhakika itaweza kumfikisha anakotaka kufika.

Vilevile anasema kuwa binafsi yake hana tabia ya kutamani kupigana na bondia fulani kwa sababu ya ukubwa wa  jina lake, ila yeye anasema bondia yeyote anayeona kuwa anaweza kushindana naye basi yuko tayari kwani hajawahi kukimbia mechi wala kukataa pambano.

“Yeyote atakayekuja akisema anahitaji basi mimi nipo tayari, sijawahi kukataa pambano kabisaa lakini mimi kama mimi sijawahi kusema eti namtaka mtu Fulani, hilo kwangu halipo,” anasema.

Hata hivyo Ndonga anasema kuwa kwa sasa mchezo wa ngumi umebadilika kwa kiasi kukibwa ukilinganisha na hapo nyuma mtu alikuwa akijihusisha na mchezo huo jamii inamchukulia mtu ambaye hana maadili.

“Zamani   mtu anayecheza ngumi alikua anaonekana msela, muhuni, mwizi, lakini hadi sasa ngumi zimesimama vyema ukiangalia vyombo vya habari vinatusupport, wadhamini, makampuni mbalimbali pia hivyo ni heshima kwa sasa.”

Hata hivyo anasema wakati anaanza kujihusisha na mchezo huu mama yake alikua anaupiga vita sana lakini kwa sasa ndiyo mtu wa kwanza anayemuombea na kumpigania katika kila hatua.

Bila shaka msomaji unatamani kumfahamu Hassani Ndonga yeye ni mtu wa aina gani, anapendelea vyakula gani na maisha yake kwa ujumla fuatilia hapa:

“Mimi ni mtu simple sana, mpole, watu wasije kuniogopa eti kwasababu nacheza ngumi, hapana, ngumi mimi mwisho ulingoni tu kitaani niko kawaida Sanaa, mcheshi na napendelea kula Ugali na kachumbari na dagaa, wali pia napenda.”

Ebwanaa eeeh!! Natumaini yapo mengi sana ambayo umeweza kujifunza kupitia kijana huyu mdogo kabisa kwenye mchezo huu wa ndondi. Usikubali kutoka nje ya malengo yako bhanaa! Simama imara na songa mbeleeeee!!!

 

 

 

 

 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Saphinia Suleiman

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, career, skills development and technology.


Latest Post