Mawazo mseto Professor Jay kurudi kwenye siasa

Mawazo mseto Professor Jay kurudi kwenye siasa

Baada ya mwanasiasa na mwanamuziki wa hip-hop nchini, Joseph Haule maarufu ‘Professor Jay’ kurudi kwenye siasa kwa mara nyingine baada ya ukimya wa muda mrefu uliotokana na kuugua, baadhi ya mashabiki wamemtaka msanii huyo kupumzika kwanza na kuangalia afya yake.

Kupitia machapisho mbalimbali katika mitandao ya kijamii hususani Instagram, mashabiki wameonesha kuhofia afya ya mwanasiasa huyo huku wengi wao wakimtaka aachane na siasa.

Aidha mashabiki walitoa mitazamo yao kwa njia ya komenti katika chapisho lililowekwa kwenye ukurasa wa Mwananchi kwa kuandika: “Haya mambo mwamba angeachana nayo kwa sasa hana alichopoteza,” ameandika Mudy Ndebo.

Naye Janelli Fashion Store ameandika: “Si kwa ubaya angeachana na haya mambo ya kuanza kupiga makelele majukwaani jamani angejionea huruma kuanza tena kupiga makelele na mapresha ya uchaguzi.”

Kwa upande wa Hamis Yusuph 773, ameandika: “Sidhani kama ana energy ya kutosha kurudi kwenye hizo mambo, kimuonekano tu anaonekana hayuko sawa.”

“Nawaza kama hakupata huo ubunge itakuaje jamani basi acha tumuombee ikawe kheri na afanikiwe ila nilitamani kama mimi angetulia kwanza sijui lakini madaktari wake wanasemaje, Mungu saidia jamani,” ameandika Ronicas Honey.

Mbali na hao, wapo ambao wameunga mkono jitihada za Professor Jay kurudi tena katika siasa huku wakimpongeza kwa hatua hiyo aliyoichukua.

“Life wakuu, hata akipumzika atakula nini? Familia inamtegemea ndugu zangu, hafanyi kwa kupenda ni njaa tu na maisha, halafu katika life sio kila mtu anapenda kuombaomba or kuchangiwa, kuna watu wamezaliwa ku-fights, afu kingine uwe mzima uwe mgonjwa kufa lazima no option. Mwacheni apambane,” ameandika Thet Ruth90.

Naye Amos Muzee ameandika: “Nasoma comments za Watanzania wengi nagundua kwa nini bado Afrika ni maskini. Hatujajikomboa kifikra kabisa kabisa! Hivi hamjui kutumikia watu ni WITO? Haya ndiyo maisha ya Professor Jay aliyoitiwa kuanzia kwenye sanaa amekuwa ni msemaji na mwakililishi wa wananchi hata kabla hajawa mbunge. Yeye amechagua kufa akiwasemea na kuwatumikia wananchi na hiyo ndiyo roho ya Mungu ifanyavyo kazi.”

Mbali na hao walioweka ujumbe kwenye ukurasa wa Mwananchi Mc Gara B aliandika ujumbe wake kwenye chapisho la Professor Jay na kuandika: "Sijui kwa nini nilikua nadhani utaibuka kiroho zaidi na si siasa.. Anyways it’s a free World ishi kusudi lako bro."

Utakumbuka kuwa Professor Jay ambaye alikuwa Mbunge wa Mikumi kwa kipindi cha 2015 -2020, jana kupitia ukurasa wake wa Instagram alichapisha video ikimuonyesha akihutubia ikiwa na ujumbe;

“Leo (jana) tumezindua kampeni zetu za uchaguzi wa serikali za mitaa kwenye Kata ya Mikumi na Ruaha. Leo moto umeungua na maji yameloana, mpaka kieleweke,” ameandika.

Profesa aliugua kwa kipindi cha mwaka mmoja na miezi mitatu huku akifichua sababu ya ugonjwa wake kupitia wimbo wake wa Siku 462 aliomshirikisha Walter Chilambo kwa kudai kwamba katika kipindi chote alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa figo.

Mbali na kuwa mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa kwa jamii pia Professor Jay amewahi kutamba na ngoma kama Zali la Mentali, Kamili Gado, Utanambia nini, Kikao cha Dharura na nyinginezo.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags