Na Masoud Kofii
Miongoni mwa wasanii wenye vipaji vya kuimba muziki ambavyo Tanzania imebarikiwa ni pamoja na Mavokali ambaye amekuwa akifanya muziki kwa namna ya tofauti. Benjamin Paul ndio jina alilopewa na wazazi wake ambao walitengeneza njia ya kijana huyo kuwa mwanamuziki.
Hitmaker huyo wa Commando/Mapopo ameiambia Mwananchi kuwa alianza kupenda muziki kutokana na msukumo kutoka kwa baba yake.
"Kitu kilichonisukuma kufanya muziki ni marehemu baba yangu ambaye alikuwa anapenda kusikiliza muziki wa zamani na alikuwa na ndoto ya kufungua bendi lakini baadaye aliajiriwa Jeshini. Kwaiyo akaachana na muziki baadaye nikaanza kuwasikiliza wasanii wa Bongo Fleva hadi nikiwa msanii," amesema Mavokali
Hata hivyo mapema baada ya Mavokali kuingia kwenye Muziki wa Bongo Fleva na mashabiki kuanza kumtegea sikio alipokea mitazamo mingi ya kufananishwa na nyota wa muziki nchini Diamond Platnumz, kitua ambacho mwanzoni kilimpa changamoto.
"Kusema kweli kwa mara ya kwanza hizi komenti zilikuwa zinanikata ila kwa sasahivi haziwezi nikata maana mtu wanae nifananisha nae sio msanii mdogo ni mkubwa kwahiyo kwangu inaniongezea juhudi na kufanya kazi kwa bidi,"amesema Mavokali
Licha ya msanii huyo kufananishwa na Diamond bado anaelezea yeye ana aina yake ya uimbaji kwenye muziki ambayo inamtofautisha na wasanii wengine na ladha ya muziki wake huwezi ipata kwa mwingine.
"Mimi nina muziki wangu ambao natamani baadaye uwe na nguvu ya kusikilizika ndio maana najitofautisha katika uandishi , ninavyo tayarisha ngoma zangu kwenye sound ni tofauti kabisa na wasanii wengine," amesema Mavokali
Mavokali ambaye alifanikiwa kutengeneza wimbo wa ‘Commando’ ukiwa na matoleo ya aina mbili ya kwanza imetazamwa mara milion 24 kwenye mtandao wa YouTube wa pili akiwa na Rayvanny ukiwa umetazamwa mara milioni 16.
Ukubwa wa kazi hiyo ulimfanya atambulike zaidi Afrika huku wimbo huo ukiingia kwenye rekodi kubwa mbalimbali. kutokana na ukubwa wa kazi hiyo anaelezea ilivyokuwa ngumu kwa msanii kupata hitsong mfululizo.
"Msanii kupata muendelezo wa kutoa hit song sio kwamba inakuwa hamna kabisa inakuwepo, unaweza ukawa na ngoma kubwa ndani ila usiiaminie kumbe ndio hit nyimbo zinazidiana inaweza kusumbua kupata ngoma kubwa kama ile lakini hit zipo mfano tuona hata Rema baada ya wimbo wake wa Calm Down hajapata ngoma kubwa zaidi, " amesema Mavokali
Licha ya mafanikio aliyopata Mavokali kwenye muziki bado anapitia changamoto zinazotaka kumrudisha nyuma ikiwemo kufutiwa video ya wimbo wake wa ‘Densi’ aliopandisha wiki mbili zilizopita kwenye mtandao wa YouTube
" Waliohusika kwenye kushusha video yangu ya ‘Densi’ ni wadukuaji kwa sababu walidukua na mail yangu sasa kama unavyojua email ndio inahusika kwenye YouTube kwa hiyo waliweza kuingia hapo na kufuta video hiyo lakini nimeweza kupambana na IT kila kitu kimekaa sawa shida ni kwamba video ilikuwa imefutwa kwa hiyo tulivyopandisha ilianza mwanzo kuhesabu views," amesema Mavokali
Mavokali anashikilia rekodi ya wimbo wake ‘Commando’ kutazamwa zaidi ya mara bilioni 177 kwenye mtandao wa TikTok na kama haitoshi Chartmetrix ilitaja jina la Mavokali kama miongoni mwa wasanii 10 wakali wa Afrobeat kutokea Afrika ambapo kwenye kundi hilo alikuwa na wakali wengine kama Wizkid, Oxlade, Davido,Ckay, Asake, Shoday, Wande Coal, Ruger, Mavokali, na Tekno.
Leave a Reply