Mauaji ya Tupac, kwanini imechukua miaka 27 mtuhumiwa kukamatwa

Mauaji ya Tupac, kwanini imechukua miaka 27 mtuhumiwa kukamatwa

KUFUATIA kukamatwa kwa mtuhumiwa wa mauaji ya Tupac Shakur, Duane Davis hivi karibuni kunaashiria mafanikio makubwa ya haki kutendeka katika tukio hilo la uhalifu ambalo kwa miaka 27 hakuna mtu aliyekuwa amekamatwa katika kesi hiyo.

Davis, 60 ambaye katika ulimwengu wa burudani anajulikana na wengi kama "Keffe D" alikamatwa Ijumaa asubuhi ya Septemba 29 karibu na nyumba yake huko Las Vegas, Marekani na sasa anashtakiwa kwa kesi ya mauaji na kusaidia genge la uhalifu.

Utakumbuka Tupac au 2Pac kwa jina la kisanii alifariki Septemba 13, 1996 kutokana na majeraha aliyoyapata kwa kupigwa risasi siku sita nyuma huko Las Vegas, Nevada, alikuwa na umri wa miaka 25 wakati huo.
Licha ya kuhudumu katika muziki kwa muda mfupi ameuza rekodi zaidi milioni 75 duniani kote, albamu yake ya nne, All Eyez on Me (1996) yenye ngoma kali kama 'How Do U Want It' na 'I Ain't Mad at Cha' ni moja ya albamu za Hip Hop zilizouza zaidi katika historia.

Katika makala haya tutaangalia ni kwa namna gani Davis anahusika katika tukio hilo, kwanini yeye pekee ndiye amekamatwa?, mbona imechukua muda mrefu?, miaka 27 sasa!, na vipi kuhusu washukiwa wengine?.

Akizungumza katika mkutano na Wanahabari wiki iliyopita, Sheriff McMahill kutoka idara ya Polisi huko Las Vegas alisema walianza mara moja uchunguzi wa mauaji ya Tupac tangu usiku wa tukio hilo mwaka 1996.

"Kwa miaka 27, familia ya Tupac Shakur imekuwa ikisubiri haki, uchunguzi ulianza usiku wa Septemba 7, 1996, imechukua saa nyingi, miongo kadhaa ya kazi kwa wanaume na wanawake kufikia hapa tulipo leo." alisema McMahill.
Naye Luteni Jason Johansson alisema mauaji ya Tupac yalikuwa ni "shambulio la kulipiza kisasi" baada ya mzozo kati ya magenge mawili yenye makao yake huko Compton, California.

Kwa mujibu wa Johansson, Tupac na aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Death Row Records, Marion "Suge" Knight, walikuwa na uhusiano na genge la Mob Piru (Knight Blood) huko Compton, huku Davis akishirikiana na genge Southside Compton Crips.

Ikumbukwe Knight ndiye alimsaini Tupac kwenye lebo ya Death Row Records tangu mwaka 1995 na kusimamia albamu zake mbili, All Eyez on Me (1996) na The Don Killuminati: The 7 Days Theory (1996).

Hiyo ni baada ya Knight kumtembelea Tupac gerezani alipokuwa akitumikia kifungo huko New York mwaka 1995 na akajitolea kulipa bondi yake kwa sharti moja la kumsaini Death Row Records. Tupac alikubali na kusaini katika lebo hiyo iliyokuwa na wasanii kama Snoop Dogg kwa wakati huo.

Sasa Tupac alikuwa Las Vegas kushuhudia pambano la Mike Tyson dhidi ya Bruce Seldon kwenye ukumbi wa Hoteli ya MGM Grand, huku wanachama wa genge la Southside Compton Crips, akiwemo Davis na mpwa wake Orlando "Baby Lane" Anderson wakihudhuria hafla hiyo pia.

"Wakati vikundi (magenge) vyote viwili vilipokuwa vinatoka kwenye pambano hilo, wanachama wa Death Row Records (Mob Piru) walimuona Orlando Anderson karibu na lifti ndani ya MGM na kumfuata na kuanza kumpiga mateke na ngumi." alisema Johansson.

Johansson alisema kwa mujibu wa picha za uchunguzi zilizopatikana katika hoteli hiyo, Tupac na Knight walionekana miongoni mwa vijana waliomshambulia Anderson.

"Hakukuwa na mtu yeyote aliyejua kuwa ni tukio hili hapa lingesababisha kupigwa risasi na kuuawa kwa Tupac Shakur." Luteni Johansson aliwaambia Wanahabari.
Johansson alisema vikundi vyote viwili viliondoka kwenye hoteli ya MGM Grand, huku Tupac na wenzake wakielekea kwenye klabu ya usiku karibu na eneo hilo.

Sasa Davis alipopata taarifa kuhusu kushambuliwa kwa mpwa wake Anderson, alianza kupanga mpango wa kupata bunduki na kulipiza kisasi dhidi ya Knight na Tupac. Na hapa ndipo uhusika wa Davis katika mauaji hayo unapoanza kujitokeza.
Baada ya kupata bunduki kutoka kwa mtu wake wa karibu, Davis aliingia kwenye gari aina ya Cadillac nyeupe pamoja na wenzake watatu, Terrence Brown, Deandre Smith na Anderson.

"Kuna muda walipokuwa kwenye gari hilo, Cadillac nyeupe, Davis alichukua bunduki na kuwapa waliokuwa wameketi kwenye kiti cha nyuma cha gari," alisema Johansson.

Nakala ya hati ya mashtaka inasema Anderson na Smith ndio walikuwa wameketi kwenye kiti cha nyuma cha gari hilo ingawa haifafanui ni mtu gani kati yao aliyefyetua risasi hadi kumuua Tupac.

Kundi hilo la kina Davis lilikuta gari aina BMW nyeusi ambalo Tupac na Knight walikuwa wamelipanda, mara moja wakaanza kuwafyatulia risasi kupitia dirishani na kisha wakakimbia eneo hilo.

Inaelezwa Tupac alipigwa risasi nne, alipelekewa katika kituo cha matibabu cha Chuo Kikuu cha Southern Nevada na kuwekwa katika uangalizi maalum ila alifariki baada ya siku sita kutokana na kuvuja damu kwa ndani.

Davis alipata umaarufu akiwa mmoja wa mashahidi wawili walio hai wa mauaji ya Tupac baada ya kuonyeshwa kwenye vipindi maalum vya televisheni na kwenye mitandao kama A&E, USA Network na Fox.

Katika mahojiano yake na BET mwaka 2018, Davis alikiri kuwa kwenye kiti cha mbele cha gari la walioshambulia Tupac na kumhusisha mpwa wake Anderson akisema alikuwa mmoja wa watu wawili walioketi kwenye kiti cha nyuma. Alisema risasi zilifyatuliwa kutoka nyuma ingawa hakumtaja aliyefanya hivyo.


Itaendelea kesho Jumamosi...!






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags