Mastaa waliowatungia nyimbo wapenzi wao

Mastaa waliowatungia nyimbo wapenzi wao

HIVI karibuni staa wa singeli Bongo, Dulla Makabila ameachia wimbo ‘Furahi’ kwa ajili ya aliyekuwa mke wake, Zaiylissa ambaye ameolewa na Haji Manara ikiwa ni miezi michache tangu aachane naye.

Katika wimbo huo ulioshika namba moja chati za YouTube kwa Tanzania, Makabila ameeleza machungu yake ya kuachana na Zaiylissa aliyepata umaarufu kupitia tamthiliya ya Jua Kali.

Utakumbuka Makabila na Zaiylissa walifunga ndoa Mei 2023 na kuachana Julai mwaka huo, hiyo ilikuwa ni ndoa ya pili kwa Makabila kuvunjika baada ya ile ya kwanza na mkewe Rahima iliyofungwa Mei 2021.

Hata hivyo, Makabila sio msanii wa kwanza Bongo kutoka wimbo kwa ajili ya mke au mpenzi wake, wapo waliotoa kabla au baada ya kuachana na wapo waliotoa katika nyakati za furaha au huzuni.

Zifuatazo ni nyimbo za wasani wa Bongofleva ambazo walizitoa maalumu kwa ajili ya watu ambao wapo nao au waliwahi kuwa nao katika uhusiano, lengo hasa ni kushukuru kwa yote yaliyotokea kati yao.

 

 

  1. Mawazo - Diamond > Jacqueline Wolper

 

Kipindi Diamond Platnumz ana uhusiano wa kimyakimya na Jacqueline Wolper, kuna siku waligombana ndipo staa huyo wa WCB Wasafi akaandika wimbo ‘Mawazo’ kwa ajili ya Wolper.

Awali wimbo huo alipoundika alimpa mwimbaji kutokea Zanzibar, Baby J ambaye alikuwa rafiki wa Wolper kipindi hicho lakini Baby J hakuvutiwa nao ndipo Diamond akaurekodi na ukajumuishwa katika albamu yake ya pili.

 

  1. Roho Zinawauma - Mr. Blue > Wema Sepetu

Kwa mujibu wa Mr. Blue, kuwa na uhusiano na Wema Sepetu haikuwa kazi rahisi kwani alitumia gharama kubwa kulitumza penzi lao hadi kukaribia kufilisika, anakiri Wema alimkosha hadi kumtungia wimbo, Roho Zinawauma.

Alipoachana na Wema, Mr. Blue alikuja kusikika katika wimbo wa Top Band (TID na Q Chief) ‘Nilikataa’, na wengi wakadai pia wimbo huo ulikuwa maalamu kwa Wema ambaye pia aliwahi kuwa na uhusiano na TID kitu ambacho walikikanusha.

 

  1. Mtoto wa Kigogo - Roma > Nancy

Wimbo wa Roma ‘Mtoto wa Kigogo’ akimshirikisha mshindi wa Bongo Star Search (BSS), Walter Chilambo aliutoa maalumu kwa ajili ya mkewe, Nancy aliyejaliwa naye watoto wawili hadi sasa.

Ikumbukwe wimbo huo ulitoka mwezi mmoja kabla ya Roma na Nancy kufunga ndoa mkoani Tanga hapo Aprili 2016, hii ni sawa na msanii kutokea Kenya, Nameless aliyeandika wimbo maarufu, Nasinzia kwa ajili ya mkewe, Wahu.

 

 

  1. Mtaje - Harmonize > Kajala

 

Baada ya kuandika jumbe nyingi mtandaoni akimuomba Kajala Masanja warudiane bila mafanikio, Harmonize aliingia studio na kurekodi wimbo ‘You’ ukiwa ni wa pili kuimbiwa mrembo huyo baada ya ‘Mtaje na Vibaya’ zilizotoka awali.

Wawili hao ambao waliweka hadharani uhusiano wao Februari 2021 waliachana kwa ugomvi mkubwa ila baadaye Harmonize alianza kampeni ya kumbembeleza Kajala warudiane na ndipo alikuwa anatoa nyimbo hizo hadi akafanikiwa ila hawakudumu sana.

 

 

  1. Kadogo - Alikiba > Aminah

 

Katika wimbo wake ‘Kadogo’ mwanzoni Alikiba anataja ‘code’ 001 ambayo ni ya Mombasa nchini Kenya anapotokea mkewe Aminah, wawili hao walifungua ndoa Aprili 2018 na sasa wamejaliwa watoto wawili.

Hata wimbo wake ‘Mvumo wa Radi’ uliotoka Mei 2018 unahusishwa na Aminah kwani ndio wimbo wa kwanza kwa Alikiba kuachia baada ya kufunga ndoa na mrembo huyo ambaye mwaka uliopita aliibuka na kudai anaipambania talaka yake yake kwa Alikiba.

 

 

  1. Mama Zuri - Nikki wa Pili > Miss Joan

 Baada ya kujaliwa mtoto wao, Zuri (2019), Nikki wa Pili ambaye sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, alitoa wimbo ‘Mama Zuri’ akimshirikisha S2kizzy ikiwa ni sehemu ya pongeza kwa mchumba wake, Miss Joan. Utakumbuka msanii mwingine kutoka Kundi la Weusi, G Nako amefanya kitu kinachoshabiana na hicho baada ya mkewe,Yasinta kutokea kwenye video ya wimbo wake, Mama Yeyoo.

 

 

  1. Lala Salama > Diamond >Wema Sepetu

Wakiwa ndani ya ndege ndipo Diamond aliandika wimbo ‘Lala Salama’, ni wakati ambao penzi lake na Wema likiwa katika kilele cha mafanikio, ulifanya vizuri na kubeba jina la albamu ya pili ya Diamond.

Kipindi cha penzi lao, pia Wema alitokea kwenye video ya wimbo wa Diamond ‘Moyo Wangu’, kabla ya kuachana na mwimbaji huyo kuwa uhusiano na warembo wengine maarufu kama Zari The Bosslady, Hamisa Mobetto na Tanasha Donna.

 

  1. Sina Neno - Jux > Vanessa Mdee

 Muda mfupi baada ya aliyekuwa mpenzi wake Vanessa Mdee kuonyesha ujauzito wake, Jux aliingia studio na kuachia wimbo ‘Sina Neno’ na kumpa ujumbe mzito Vee ambaye tayari alishachumbiwa na Rotimi wakati huo.

Utakumbuka Vanessa na Jux  walikuwa na uhusiano kati  ya mwaka 2014 hadi 2019 na kwa kipindi chote hawakujaliwa mtoto. Kwa sasa Vanessa anayeishi huko Georgia, Marekani na Rotimi tayari ni mama watoto wawili, Seven na Imani.
.
.
.
#MwananchiScoop
#BurudikaNasi






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Asha Charles


Latest Post