Mastaa acheni maisha ya kufeki

Mastaa acheni maisha ya kufeki

Na Aisha Lungato

Baadhi ya ‘mastaa’ Bongo wamekuwa wakiamini ‘kufeki’  maisha kwa kupiga picha kali, ‘kuposti’ wakiwa sehemu zastarehe zenye gharama kubwa na majumba ya kifahari ndiyo ‘ustaa’ wenyewe, wanasahau kuwa vitendo hivyo vinawaaminisha mashabiki kuwa maisha yao yapo poa  hayana changamoto zozote.

Kutamba na kulinda ‘brandi’ zao kama watu maarufu nchini siyo shida lakini tatizo ni kwamba maigizo yamekuwa mengi kwenye maisha yao hadi imekuwa ngumu kuamini chochote kuhusu watu hawa, kifupi hili suala limekuwa jipu kwa baadhi ya ‘mastaa Bongo.

Licha ya kufanya maigizo hayo wanasahau kuwa ‘kufeki’ kwao maisha, hufikia mwisho pale wanapopata matatizo kwani  baadhi yao hurudi kwa jamii na kuomba misaada, jambo ambalo hushangaza na kuzua taharuki kwa jamii kwa sababu ‘mastaa’ hao wanayoonesha mitandaoni hayaendani na kuomba misaada kutoka kwa mashabiki na wadau.

Niwarudishe nyuma miaka iliyopita wapo watu maarufu walioshangaza jamii baada ya kutoka hadharani kuomba misaada ya kifedha walipopatwa na matatizo, na siyo hao tu wapo na wengine ambao walizua gumzo mitandaoni baada ya kutokea misiba, mazingira ya nyumbani kwao yalishangaza watu, kwani hayaendani na yale ambayo mashabiki wameyazoea mitandaoni.

 

Kwa matukio hayo tu inaonesha kwa kiasi gani wasanii wamebweteka na umaarufu wa kwenye mitandao ya kijamii lakini maisha yao halisi hayako sawa na hayaendani na yale wanayoweka kwenye mitandao ya kijamii. kama ‘staa’ ni vyema kutobadili mwenendo na matendo yako, ili tu watu watishike na maisha yako ilihali hayapo kwenye uhalisia.

Ni vyema kujikubali na kuishi maisha yaliyo kwenye uwezo wako kama wasemavyo waswahili ‘kujikuna mkono unapoishia’ wala siyo ushamba kufanya hivyo kwani wapo baadhi ya watu maarufu ambao hawajisumbui kuaminisha mashabiki kuwa wana maisha mazuri, bali wanawaonesha uwezo wao kwa kufanya kazi nzuri zenye kupendwa na mashabiki wao.

Kuacha ‘kufeki’ maisha kutasaidia sana hata  kwa mashabiki  ambao wanatamani kuwa kama ‘staa’ fulani, kwa sababu wapo ambao kutokana na mapenzi yao kwa msanii au muigizaji huwa tayari kufanya kila njia ili waishi maisha ya ‘staa’ huyo bila ya kufahamu kuwa yale maisha ni ya mitandaoni tu.

Nikukumbushe wiki mbili zilizopita  mwanamuziki  wa hip-hop Nay wa Mitego aliwazindua akili na kuwaonya vijana  ambao wanapambana huku wengine wakihatarisha maisha yao kuishi kama staa fulani, Nay aliweka wazi kuwa kwa asilimia 90 maisha ya mastaa wengi wa Bongo ni ya uongo.

Wanasema wasanii ni kioo cha jamii, kioo hichi kutokana na kutoonesha uhalisia wa mambo kimekuwa chachu ya vijana wengi hasa mabinti kuingia kwenye maisha hatarishi, wengine wakiuza miili yao ili tu nao waweze kupata fedha za kuishi maisha ya bata na kupendeza kama mastaa wanavyofanya.

Kabla ya kuendekeza uongo kwenye mitandao ya kijamii,   ni vyema kujitafakari kwanza vitu vya ku-post na mchango wake kwa jamii, ni wakati wa kuacha kufanya ‘kufeki’   ni wakati wa kusimamia kwenye ukweli ili kuepukana na aibu zijazo mbele, kama huna ni wewe kama nyumbani pabovu basi rekebisha ili ‘ustaa’ wako uendane na mazingira yako.

Kitu ambacho baadhi ya watu maarufu hawafahamu ni kuwa siku hizi mashabiki na wadau mbalimbali wamechoshwa na maisha ya uongo na janja janja za watu mastaa kwenye mitandao ya kijamii kwa kuthibitishia hilo pita kwenye mitandao ya kijamii na upande wa ‘komenti’ za mashabi.

Kuna mchekeshaji mmoja aitwaye Eliudi, yeye kwa upande wake amekufa akivaa uhalisia wa wakazi wa Mkoani Mbeya kuanzia uongeaji wake hadi matendo yake. Mchekeshaji huyu imekuwa kawaida sana kwake ku-post maisha ya nyumbani kwao kijijini bila ya kujali lolote kwani huo ndiyo uhalisia wa alipotoka.

Si yeye tu pia kuna mwanadada ambaye ni mwanamitindo anayeitwa Jasinta Makwabe , yeye kwa asili anatokea Bukoba, mrembo huyu amekuwa akionesha maisha ya nyumbani kwao ambako ni kijijini kwa uhalisia si jambo  la kushangaza kukuta mrembo huyu akiwa ame-post picha za nyumbani kwao hata kama kukiwa na nyumba ya nyasi, hiyo yote ni kutokana nay eye kuchagua maisha ya uhalisia.

Muigizaji kutoka nchini Kenya Lupita Nyong'o, naye ni kati ya watu maarufu ambao wanaishi maisha yao halisi hayuko kwa ajili ya kujionesha, anafanya kazi kwa ajili ya kukuza jina lake na kipaji chake, hata ukitazama kupitia mitandao yake ya kijamii utagundua kuwa hayuko kwenye kujionesha bali kuwafunza maisha wale wote ambao wanatamani kuwa kama yeye.

Muhimu kwa jamii kutochukua kila kitu wanachokiona kwenye mitandao ya kijamii kwa sababu huko ndiko wamejaa waigizaji, si jambo la kushangaza kukuta mtu amelala njaa lakini muda huo ana-post picha ya pizza kwenye mitandao ya kijamii.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Asha Charles


Latest Post

Latest Tags