Maneno yaliyotumika kwenye kibango ya Lavalava yatolewa ufafanuzi

Maneno yaliyotumika kwenye kibango ya Lavalava yatolewa ufafanuzi

Baada ya wadau mbalimbali wa muziki Bongo kutafsiri vibaya baadhi ya maneno katika wimbo wa mwanamuziki Lavalava uitwao ‘Kibango’ kuwa hauna maadili kwenye maneno mfano “Nasikia nyeee nyepesi hii pombe, Nchanganyie Bapa”, Baraza la sanaa la Taifa (BASATA) limetoa ufafanuzi wa wimbo na maneno yalitumika.

Kupitia tovuti rasmi ya Basata imeshare taarifa hiyo ya kuutolea ufafanuzi wimbo huo kwa kuupa daraja WZ18 sawa na daraja A yaani kusikilizwa na watu wenye umri wa miaka 18.

“Baraza la sanaa la Taifa (BASATA) limepitia na kuhakiki mashairi ya wimbo uitwao “KIBANGO” na kuupa daraja WZ18 sawa na daraja A yaani kusikilizwa na watu wenye umri kuanzia miaka 18 na kuendelea na kusikilizwa sehemu maalumu ambako watu chini ya umri huo hawatokuwepo” imeeleza taarifa hiyo

Hata hivyo katika uhakiki wa mashairi ya wimbo huo taarifa imeeleza kuwa ngoma hiyo haina shida yoyote kwani imezingatia vitu vyote kuanzia upangiliaji wa vina pamoja na matumizi ya lugha.

“Wimbo ni mzuri kuanzia kwenye upangaji wa vina na mizani, utumiaji wa lugha ya picha na tafsida kama maneno “Hii party ina vijiti”. Ujumbe wa wimbo huu umelenga zaidi watu wanaotumia vilevi mbalimbali na hii imejidhihirisha katika mashairi kama
“Naskia nyeee nyepesi hii pombe Nchanganyie Bapa”, lakini pia ujumbe mwingine unahusu mapenzi.

Hivyo basi wimbo huu umewalenga watu wenye umri kuanzia miaka 18, kutokana na Sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umri sahihi wa mtu kutumia vilevi na kujihusisha na mapenzi ni kuanzia miaka 18 na kuendela” imeeleza taarifa hiyo

Aidha katika taarifa hiyo Basata imetoa angalizo kwa vyombo vya habari kuzingatia muongozo wa maadili kwenye kucheza wimbo huu na kuzingatia mazingira, muda na aina ya vipindi ambavyo hufuatiliwa na kusikilizwa na watu wenye umri kuanzia miaka 18 na kuendelea ili kuzingatia maadili ya nchi yetu.

Utakumbuka kuwa wimbo wa ‘Kibango’ uliachiwa miezi miwili iliyopita ambapo mpaka kufikia sasa unazaidi ya watazamaji Laki moja elfu hamsini na moja katika mtandao wa YouTube.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Aisha Lungato

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, lifestyle, artist profiles and career.


Latest Post

Latest Tags