Mambo yanayowaharibia vijana sehemu za kazi

Mambo yanayowaharibia vijana sehemu za kazi

Ifahamike kuwa jinsi ya kupata kazi au ajira kwa vijana imekuwa changamoto katika siku hizi za usoni kwa mantiki hiyo basi kijana unapaswa kuwa makini sana pale ambapo unabahatika kupata sehemu ya kuonyesha uwezo ulionao.

Kuna msemo unaosema usichezee kazi, chezea mshahara, mara nyingi msemo huu watu huuchukulia kama dhihaka fulani hivi lakini ndani yake una ukweli mchungu kwani kauli hii inawataka watu kuheshimu kazi, ujuzi hata maarifa waliyokuwa nayo.

Hivyo basi, leo ndani ya Mwananchi Scoop nataka kukueleza kijana mwenzangu pamoja na kuhustle kwako sana na ukabahatika kupata kazi basi achana na mambo haya yanaweza kukuharibia ajira uliyotumia muda mrefu kuipata kuwa makini fuatilia makala haya.

Acha dharau

Hapa sasa vijana wengi wakiwa makazini unakuta mtu anauwezo wa kufanya jambo Fulani ambalo pengine bosi wake hana uwezo nalo unakuta anadharau sana kwakujiona bila ya yeye kazi haziendi.

Kwa kuwa unajua lugha za kigeni unadharau wafanyakazi wenzio ambao hawawezi, kumbuka kuwa tabia hiyo ya kudharau vitu au watu huchangia kudumaza vijana kwa kuwa hujiona wamefika na kushindwa kujiongeza.

Always dharau huvunja ushirikiano kazini na mara nyingi hutengeneza maadui.

Epuka kuwa mfitinishaji

Wapo vijana ambao wanaamini ili wafanikiwe na kupiga hatua  ni lazima wafanye ufitini fulani kuwaharibia wengine, Mara nyingi tabia hii hufanywa kwa malengo ya kumshawishi boss au mteja awaone wao ni bora kuliko wale wanaowafitini. 

Nikujuze tu kwamba ukipata kwa fitina basi utapoteza kwa fitina pia  Umbea na kuwasema watu vibaya ili kupata mafanikio hasa katika mahali pa kazi au biashara hakutakufanya kijana kuwa bora.

Acha majigambo na majivuno

Katika maisha ya kawaida ya kazi ama biashara kuna tabia ya baadhi ya vijana waliofanikiwa kujitukuza au kutaka kuonyesha umwamba kwamba wao ni wao.

Wapo wale wanaojiona kuwa ndiyo wasimamizi, maboss au viongozi wanataka wakizungumza tu kila mtu awaogope, Aina hii ya uhusiano inaua ndoto za vijana wengi hasa pale kwa bahati mbaya wanapoporomoka kutoka kwenye nyazifa zao au hali bora ya kifedha na kufulia.

Kujiona kuwa wewe ndo kila kitu yaani unajimwambafai tambua kuwa unaua kipaji au uwezo uliyokuwanao kwani unatengeneza uhusiano mbaya na wafanyakazi au wafanyabiashara wenzio acha mara moja.

Utovu wa nidhamu

Kuna baadhi ya watu wanahusianisha ujana na utovu wa nidhamu. Baadhi ya vijana wanaonekana wa hovyo kwa sababu ya kukosa nidhamu. Kutokana na nafasi zetu kikazi au kibiashara tumejikuta tukikosa heshima kwa wafanyakazi, wateja au washirika wetu wa biashara. Utovu wa nidhamu huzaa kiburi na chuki. Hufanya watu wakudharau na kukuona wa kawaida sana.

Kijana smati ni yule mwenye nidhamu ya kazi na maisha yake, Nidhamu hufanya kijana makini kuheshimu na kuheshimu wengine bila kujali uwezo au hali zao za kielimu. Kwa kifupi mtu wa namna hii huwa ni “konki wa mafanikio”. 

Kutozingatia misingi ya kitaaluma

Kutokana mambo kuwa mengi katika kipindi ambacho muda ni mchache baadhi ya vijana wamejikuta wakiruka misingi ya taaluma zao na kuchulia kazi au biashara zao kama masuala ya kawaida. Tabia hizi za kukiuka miiko ya kitaaluma inafanya vijana waonekane watu wa hovyo wasiotakiwa kupatiwa madaraka.

Embu jaribu kumtizama kijana wa kiume ambaye ni mwalimu katika shule Fulani ambaye anatabia za kuwatongoza wanafunzi wake, mwalimu wa dizaini hii ni rahisi sana kuharibu mustakabali mzima wa taaluma aliyokuwa nayo ikitokea tu habari zake zikafahamika kwa wahusika wa ngazi za juu ni rahisi kupoteza kazi yake.

Tabia kama hizo za rushwa katika kazi zinafanya vijana waharibu kazi na sifa ya taasisi wanazofanyia kazi, Hautakufa kama utafuata misingi na taratibu za kazi au biashara yako kwa kuingiza fedha halali na kupunguza tamaa.

Ili uweze kukua kikazi au kitaaluma unatakiwa uwe mtunzaji mzuri wa muda. Jiwekee ratiba imara isioterereka isipokuwa tu nyakati za dharura. ishi ratiba hiyo na wafanye rafiki na wafanyakazi wenzio waiheshimu.

Jambo la muhimu kabisa usiruhusu mtu akupotezee muda zingatia hayo, utaona mafanikio na utadumu kwenye kazi yake au ajira uliyokuwa nayo!.

 

 

 

 

 






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Saphinia Suleiman

A digital journalist and writer for Mwananchi Scoop. My stories are around entertainment, career, skills development and technology.


Latest Post

Latest Tags