Mambo muhimu anayotakiwa kufanya Gamondi kwa Yanga

Mambo muhimu anayotakiwa kufanya Gamondi kwa Yanga

Hellow!! It’s another weekend nawasalimu kwa jina la burudani na burudani iendelee kama ilivyo kawaida yetu kukujuza wewe mwanetu mambo mbalimbali yanayo happen katika michezo na burudani.

Leo katika burudani tumekusogezea mambo ambayo anayotakiwa kufanya Gamond kocha mpya wa yanga katika klabu hiyo.

Yanga tayari imeshamtangaza kocha wao mpya kuwa ni Miguel Gamondi raia wa Argentina akiwa ndio bosi wa benchi la ufundi kuanzia sasa tayari kwa msimu ujao.

Gamondi anachukua nafasi ya Mtunisia Nasreddine Nabi ambaye aligoma kuongeza mkataba kuifundisha timu hiyo baada ya kuingoza timu hiyo kwa misimu miwili na nusu akiwaachia mataji na kuifikisha timu hatua ya Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, hebu tuyaangalie mambo matano atakayokabiliana nayo kocha huyo.

MASTAA MUHIMU WA KIKOSI ANACHOKIKUTA

Hatua ya kwanza ambayo Gamondi atatakiwa kupambana nayo ni kuwabakisha wachezaji ambao wanatajwa kutaka kuondoka ndani ya kikosi cha Yanga baada ya kumalizika kwa msimu uliopita.

Yanga ina presha ya kuwapoteza mabeki Wakongomani Djuma Shaban, Joyce Lomalisa, kiraka Yannick Bangala na mshambuliaji wao Fiston Mayele baada ya mafanikio ya miaka miwili mfululizo.

Ukiacha juhudi za viongozi wa Yanga wanazofanya kutuliza wimbi hilo Gamondi pia anaweza kutumia saikolojia yake kuwabakisha wachezaji ambao watawahitaji kusalia ili asibomoe sana timu yake na kuanza upya kujenga kikosi chake.

WAPYA ATAKAOWAONGEZA

Yanga chini ya Gamondi lazima itahitaji kuiboresha timu hiyo kwa kuleta wachezaji wapya, ambao watakuja kuungana na wale ambao atawaona anaweza kusalia nao ili kuipa mafanikio klabu hiyo.

Kocha huyo anahitaji kutulia ili mastaa hao waje kumpa heshima kwa mchango wao ambapo kama atashindwa kuleta watu bora wanaweza kuja kushusha heshima yake ndani ya mkataba wake na Yanga.

MTIHANI KWA AZAM NA SIMBA

Baada ya Yanga kusumbua kwa miaka miwili mfululizo, wapinzani wao hasa katika mbio za ubingwa watani wao Simba na Azam hizo sio taarifa njema kwao na kuanzia kipindi hiki watakuwa kwenye harakati za kujenga vikosi vyao ili kuja kuwapokonya mataji hayo mabingwa wa ligi.

Azam tayari itakuwa na kocha mpya Youssouph Dabo raia wa Senegal ambaye ataanza msimu ujao kazi lakini pia Simba itakuwa chini ya Mbrazil Robert Oliveira 'Robertinho' ambaye naye licha ya kuwa tayari mwenyeji lakini msimu wake kamili atauanza msimu ujao kuanzia mwanzo baada ya kuingia katikati ya msimu wakitarajiwa kuanza kushindana wote watatu kuanzia mwanzo.

Makocha hao wawili kama wataharibu afya ya Yanga ya mataji yanayoshikiliwa na Yanga hiyo itakuwa presha kubwa kwa Gamondi ndani ya timu hiyo.

MAFANIKIO YA NABI

Gamondi anaipokea Yanga ikiwa na afya kubwa wakichukua taji la ligi, ngao ya jamii, kombe la Azam (ASFC) yote wakiyachukua mara mbili mfululizo lakini kama haitoshi wakacheza fainali ya shirikisho wakiwa chini ya Nabi.

Mafanikio haya ya Nabi yatakuwa ni sehemu ya presha kwake, endapo Gamondi atayabakiza mataji hayo pia kisha kuifikisha Yanga mbali angalau hatua ya makundi au robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika anaweza kukikimbia kivuli cha Nabi kwa akili kubwa, mtego ambao mashabiki wa timu yake na viongozi wake wanasubiria kuona

KIPI KIPYA KWA UTAWALA WAKE

Ushabiki wa Tanzania uko tofauti, tayari mashabiki wa Simba wameshaanza kuwakejeli wenzao wa Yanga kwamba kocha waliyemleta hana taji lolote kama kocha mkuu na wenzao wanajibu wakiringia hatua ya kocha huyo kucheza ngao za juu nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kuongioza timu kucheza Super cup ya Afrika.

Kejeli hizo hazitaishia hapo ambapo mashabiki wa klabu yake watasubiri kuona kocha huyo atakuwa na mwanzo wa namna gani ndani ya kikosi chao kama atashindwa kuwa na mwanzo mzuri hili linaweza kumharibia na kujikuta anaingia kwenye presha dhidi ya watu wake.

APEWE MUDA

Mashabiki wa Yanga na viongozi wao wanatakiwa kujiandaa kwamba kocha mpya lazima atakuja na mabadiliko kwenye timu yao, kitu bora wanachotakiwa kufanya ni kumpa muda aweze kutengeneza mwanzo wake mzuri hata kama ikitokea ameanza vibaya.

Wanatakiwa kukumbuka hata Nabi aliyeonekana kufanikiwa hakuanza na kasi kubwa ya kushinda kuanzia mwanzo alipepesuika kisha baadaye kutulia na akafanya mambo mazuri aliyoyafanya, endapo nao wataingia kwenye mtego wa wa kumjaza presha watakuwa wameshiriki kuibomoa timu yao na kumharibia Gamondi pia.

Nasemaje!! Kivumbi na jasho huko jangwani Gamondi ajipange kuendeleza furaha ya mashabiki wa klabu hiyo.






Comments 0


Leave a Reply

Author

Hello, I'm
Asha Charles


Latest Post

Latest Tags